Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba9 2013 saa 18:22 PM
Posted Jumatano,Oktoba9 2013 saa 18:22 PM
Kwa ufupi
Wadau wa habari nchini wameamua kutotangaza
wala kuandika habari zinazomhusu Waziri wa Habari Dk. Fenela Mukangara
pamoja na Mkurugenzi wa Maelezo Assah Mwambene kama sehemu ya kupinga
hatua ya serikali kuvifungia vyombo vya habari.
Dar es Salaam. Wadau wa habari
nchini wametangaza msimamo wa kutotangaza wala kuandika habari
zinazomhusu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela
Mukangara pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Habari(Maelezo), Assah
Mwambene kama sehemu ya kupinga mwenendo wa serikali wa kuvifungia
vyombo vya habari.
Wadau hao kutoka taasisi mbalimbali za habari
wamesema kuwa pamoja na kilio cha muda mrefu cha kuitaka serikali kufuta
Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, lakini hakuna jambo lolote
lililofanyika mbali ya kuendelea kuviandama vyombo hivyo.
Katika taarifa yao, wadau hao wamesema pia
wamesikitishwa na tabia iliyoonyeshwa na Dk Mukangara na Mwambene
kuchukua uamuzi wa kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania bila
kuyasikiliza na kupotosha umma juu ya jambo hilo.
“Kwa msingi huo, wadau tumeamua kwamba tutasitisha
kuandika, kutangaza na kupiga picha shughuli zozote zitakazowahusisha
au kuratibiwa na Dk Mukangara na Mwambene hadi hapo itakapotangazwa
vinginevyo. Adhabu hiyo inaanza mara moja kuanzia leo,” imesema sehemu
ya taarifa hiyo.
Aidha taarifa ya wadau hao imesema kuwa
wataendelea kupinga Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kwa kutumia njia
mbalimbali ikiwemo kuongeza nguvu ya kisheria mahakamani kwenye kesi
iliyofunguliwa na Kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd, mwaka 2009
inayopinga sheria hiyo.
Taasisi zilizoshiriki kwenye uamuzi huo ni pamoja
na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat), Jukwaa la Wahariri
(TEF), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika-tawi la Tanzania
(Misa-Tan) na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Nyingine ni Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari
Tanzania (UTPC), Klabu ya Waandishi wa Habari ya Dar es Salaam (DCPC) na
Tanzania Human Rights Defenders (THRDC).
SOURCE : MWANANCHI
SOURCE : MWANANCHI