Na Bakari Kiango, Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba9 2013 saa 15:45 PM
Posted Jumatano,Oktoba9 2013 saa 15:45 PM
Kwa ufupi
Dar es salaam. Polisi Kitengo
cha Kudhibiti Dawa za Kulevya juzi limewaachia kwa dhamana watuhumiwa
wawili wanaodaiwa kukutwa na maiti iliyokuwa na dawa tumboni
zinazodhaniwa ni za kulevya.
Mkuu wa Kitengo hicho, Kamanda wa Polisi
Godfrey Nzowa, aliliambia gazeti hili jana kuwa katika upelelezi wao
wameshindwa kuwabaini moja kwa moja watuhumiwa hao kama wanahusika na
tukio hilo au la.
“Watuhumiwa hawa wapo nje kwa dhamana na kwamba
kama upelelezi wetu ukikamilika watu hawa wakakutwa na hatia basi
watafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Nzowa.
Tukio hilo lilitokea Septemba 22 mwaka huu jioni
maeneo ya Tabata ambapo maiti huyo aliyejulikana kwa jina la Rajabu
Kidunda (43) alikutwa amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha
akiwa amelala kwenye godoro liliotandikwa sebuleni nyumbani kwa
watuhumiwa hao.
Inadaiwa kuwa, Kidunda alifika kwenye nyumba hiyo
akiwa mgonjwa akitokea wilayani Newala mkoani Mtwara alikokwenda
kuchukuliwa na watuhumiwa hao kisha kuletwa Dar es Salaam.
Baada ya kupata taarifa hizo za kifo hicho cha
utata makachero wa polisi walimchukua maiti huyo na kumfanyia uchunguzi
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) ambapo aligundulika kuwa na
pipi 33 aina za Heroin zenye uzito wa gramu 561.
Kwa mujibu wa Kamanda Nzowa, taarifa za awali
zilizothibishwa na Mganga Mkuu kutoka katika moja Hospitali wilayani
Newala, zinaeleza kuwa baada ya kupata ahueni Kidunda alichukuliwa na
watuhumiwa ambao mmoja kati yao anadaiwa kuwa ni mkewe.
Aliongeza kuwa, watuhumiwa hao wamepewa masharti
ya kuripoti kwenye kituo cha polisi husika kwa muda waliopangiwa huku
polisi wakiendelea kufanya upelelezi ikiwamo kubaini marehemu
alikozitoa dawa hizo.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI