Tuesday, 8 October 2013

Wapinzani wasitisha maandamano

  

 
Na Raymond Kaminyoge

Posted  Jumanne,Oktoba8  2013  saa 17:45 PM
Kwa ufupi
Profesa Lipumba alisema baada ya kuzungumza na Rais kuhusu muswada huo, ndipo watakapotoa uamuzi.
Vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vimeahirisha maandamano ambayo yalitakiwa kufanyika keshokutwa (Alhamisi).
Vyama hivyo vilipanga kuandamana nchi nzima ili kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete asisaini muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwa una kasoro nyingi ikiwamo Zanzibar kutoshirikishwa katika mchakato.
Viongozi wa vyama hivyo wamesitisha uamuzi huo baada ya Rais Kikwete kusema yuko tayari kufanya nao mazungumzo kujadili suala hilo.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema hayo Jumanne mara baada ya kukutana na viongozi wenzake katika Ofisi za NCCR-Mageuzi, Ilala Dar es Salaam.
Mbele ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Profesa Lipumba alisema viongozi wa vyama hivyo wametafakari na kuona ni busara kumsikiliza Rais Kikwete kwanza kabla ya kuamua kuendelea na uamuzi wao au la.
“Lengo la kuandaa maandamano ni kuhakikisha kwamba tunapata Katiba bora isiyo na kasoro, ndiyo maana tunaona kwa kuwa Rais ameonyesha nia ya kuzungumza na sisi tumeona ni bora tukakutana naye kwanza,” alisema.
Profesa Lipumba alisema baada ya kuzungumza na Rais kuhusu muswada huo, ndipo watakapotoa uamuzi.
Alisema bado hawajapata taarifa rasmi kutoka Ikulu kuhusu lini watakutana na Rais na kwamba taarifa hizo wamezipata kupitia vyombo vya habari.
Jana, vyombo vya habari vilikariri taarifa kutoka ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, ikisema Rais Kikweta anatarajia kukutana na viongozi wa vyama hivyo kati ya Oktoba 13 na 15 mwaka huu.
Rais Kikwete katika hotuba yake ya kila mwezi Ijumaa iliyopita, alisema hoja na kauli za wanaopinga muswada huo zinazungumzika ili kutafuta mwafaka badala ya kufanya maandamano.
Katika kikao cha Bunge kilichopita, wabunge wa vyama hivyo walitoka nje ya ukumbi wakipinga Muswada usijadiliwe kwa kuwa una kasoro nyingi.
Miongoni mwa kasoro hizo ni kutoshirikishwa kwa Serikali ya Zanzibar, madaraka ya Rais ya kuteua wajumbe wa Bunge maalumu la Katiba na kuvunjwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kuwasilisha rasimu ya pili kwenye Bunge la Muungano badala ya kuwepo hadi katika kura ya maoni.

SOURCE: MWANANCHI