Tuesday, 17 September 2013

CAG akagua ubadhirifu fedha Halmashauri Bukoba Mjini


 
Na Patricia Kimelemeta

Posted  Jumanne,Septemba17  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Msaidizi wa CAG, Fransic Mwakapalila alisema ukaguzi huo utaanza mwezi huu, ambao utahusisha kukagua miradi mbalimbali iliyoainishwa kwenye hadidu za rejea.


Dar es Salaam.Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) ameanza ukaguzi maalumu katika Halmashauri ya Bukoba Mjini kuhusu ubadhirifu wa fedha mbalimbali za miradi ya maendeleo zilizokuwa zinatumika kwenye halmashauri hiyo.
Uamuzi wa CAG umekuja baada ya Kamati Kuu ya CCM kumtaka CAG kufanya ukaguzi katika halmashauri hiyo baada ya kuwepo kwa taarifa za ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo zinazodaiwa kuidhinishwa na Meya wa Halmashauri hiyo, Anatory Aman.
Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa upimaji wa viwanja vya Mji wa Bukoba, ukarabati wa soko na ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ambayo inadaiwa kuwa na harufu ya ufisadi.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Msaidizi wa CAG, Fransic Mwakapalila alisema ukaguzi huo utaanza mwezi huu, ambao utahusisha kukagua miradi mbalimbali iliyoainishwa kwenye hadidu za rejea.
Alisema kutokana na hali hiyo, wakaguzi watafika kwenye halmashauri hiyo mwisho wa mwezi huu kwa ajili ya kufanya ukaguzi huo.
“Tayari tumepewa hadidu za rejea kwa ajili ya kufanya ukaguzi maalumu wa Halmashauri ya Bukoba mjini, hivyo basi wakaguzi watafika katika halmashauri hiyo mwisho wa mwezi huu,” alisema Mwakapalila.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, muda wa kukamilika kwa ukaguzi huo utatokana na kukamilisha kwa shughuli hiyo, jambo ambalo linaweza kubaini ukweli kuhusu uhalali wa matumizi ya fedha hizo au la.

SOURCE; MWANANCHI