Na Suzy Butondo,
Kwa ufupi
Hata hivyo, baada ya kutoa maelezo, si
mshtakiwa wala mdhamini wake aliyehudhuria mahakamani hapo licha ya kesi
hiyo kusikilizwa mara mbili bila ya taarifa yoyote kabla ya hakimu huyo
kutoa hukumu hiyo jana.
Shinyanga. Hakimu wa Mahakama
ya Mwanzo iliyopo eneo la Nguzo Nane, Kata ya Kambarage Mjini Shinyanga,
Satto Nyangoha amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu katika shavu lake la
kushoto baada ya kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa baiskeli.
Kitendo hicho kinadaiwa kufanywa na mlalamikaji
katika kesi hiyo, Emmanuel Izengo (28), mkazi wa Tambukareli, Shinyanga
baada ya kutokuridhishwa na hukumu iliyotolewa bila ya mshtakiwa, Daniel
Makelezia, mkazi wa Lubaga Shinyanga na mdhamini wake, Marko Nkelezia
kuwepo mahakamani.
Katika hukumu yake, Hakimu Nyangoha alisema
mshtakiwa atakapopatikana atatumikia kifungo cha miaka miwili jela baada
ya kupatikana na hatia ya wizi wa baiskeli hiyo aina ya Neria yenye
thamani ya Sh150,000.
Awali, ilielezwa kwamba baada ya tukio hilo la
wizi lililotokea Agosti Mosi, mwaka huu katika eneo la Nguzo Nane,
mshtakiwa alikamatwa na kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi namba 460
ya 2013 kabla ya kuachiwa kwa dhamana Agosti 23, mwaka huu huku kesi
yake ikiendelea na pande zote mbili zilitoa maelezo.
Hata hivyo, baada ya kutoa maelezo, si mshtakiwa
wala mdhamini wake aliyehudhuria mahakamani hapo licha ya kesi hiyo
kusikilizwa mara mbili bila ya taarifa yoyote kabla ya hakimu huyo kutoa
hukumu hiyo jana.
Kushambuliwa
Baada ya hukumu hiyo mlalamikaji alitoa shukrani na kuwashika mikono wote waliokuwamo mahakamani humo na kutoka nje.
Ilidaiwa kuwa baada ya dakika 15, Izengo alirudi
mahakamani hapo na kudai kuwa ameleta risiti ya kumwonyesha hakimu
thamani ya baiskeli yake alipoingia ndani ndipo kelele za Mshauri wa
Baraza, Mary Wamba zikaanza kusikika akisema: ‘Njooni jamani hakimu
kavamiwa anapigwa’.
Baada ya watu waliokuwa karibu kuingia katika
ofisi ya Mahakama hiyo walikuta hakimu ameshacwhomwa kisu katika shavu
la upande wa kushoto huku akivuja damu nyingi huku mtuhumiwa huyo
akiendelea kumshambulia. Baada ya tukio hilo, wasamaria wema walimpeleka
hakimu huyo katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambako alilazwa kwa
matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Shinyanga, Evarist Mangala alisema mtuhumiwa alikamatwa mara baada ya
tukio hilo kusubiri hatua za kisheria dhidi yake.
CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI
CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI