Na Daniel Mjema, Mwananchi
Posted Alhamisi,Septemba19 2013 saa 13:5 PM
Posted Alhamisi,Septemba19 2013 saa 13:5 PM
Kwa ufupi
419 Idadi ya tembo waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini.
1,645Mbao zilizokamatwa baada ya kuibwa katika hifadhi nchini
Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) ni
moja ya hifadhi 16 nchini ambayo imefanikiwa kudhibiti vitendo vya
ujangili wa tembo ambao wamekuwa wakiuawa na wahalifu wanaotafuta
vipusa.
Takwimu zilizotolewa na Mhifadhi Mkuu wa Shirika
la Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa), Mtango Mtahiko zinaonyesha kati ya
2009 hadi 2012, wanyamapori 15,227 waliuawa ndani ya hifadhi hizo.
Kati ya wanyamapori hao, 419 ni tembo waliouawa
katika hifadhi mbalimbali huku hifadhi ya Ruaha ikiongoza kwa tembo 131
kuuawa ikifuatiwa na Serengeti 92, Tarangire 53, Katavi 36 na Mikumi 30.
Mkuu wa Idara ya Ulinzi na Uokoaji Kinapa,
Sebastian Gambares anasema ujangili wa tembo umepungua kwani mwaka
2012/2013 hakukuwa na tukio la kuuawa kwa tembo ndani ya hifadhi hiyo.
“Hata matukio ya nyuma ya kuuawa kwa tembo
yalihusisha matukio ya kuuawa nje ya hifadhi, Kinapa tumekuwa makini
sana katika kudhibiti Majangili,”anabainisha mhifadhi huyo.
Anasema wanapobaini kuwapo kwa tembo katika eneo
fulani hasa tembo wanaotoka Hifadhi ya Amboseli nchini Kenya, basi
kikosi cha kupambana na ujangili kinakuwapo karibu na maeneo hayo.
Naye Mkuu wa Hifadhi ya Kinapa, Kanda ya Kaskazini
Magharibi, Imani Kikoti anasema moja ya mikakati iliyosaidia udhibiti
wa ujangili ni kubadilishana taarifa za kiitelejensia kwenye maeneo ya
mipakani.
Kikoti anasema Kinapa imeamua kudhibiti ujangili
wa tembo kwa kuwa wanaweza kutoweka kama udhibiti makini hautakuwapo
katika maeneo waliopo.
Kwa mujibu wa Kikoti, katika kipindi cha 2009
hadi 2012, idadi ya majangili wanaokamatwa imekuwa ikipungua kutoka 320
mwaka 2009 hadi majangili 278 mwaka 2012/2013.
Anasema mikakati ya kukabiliana na ujangili
inahusisha pia ujangili wa mazao ya misitu, kuwasha moto kwenye hifadhi
na uingizaji mifugo kwenye maeneo ya hifadhi kwa uharibifu huo
unaathiri vyanzo vya maji.
Kikoti anasema kushuka kwa idadi ya mbao na nguzo
zinazokamatwa ni dalili tosha kwamba vitendo vya ujangili wa mazao ya
misitu ndani ya hifadhi vimekuwa vikidhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI
CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI