Kwa ufupi
Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wa Mizigo
Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay anasema Serikali imechukua uamuzi wa
busara kushusha ushuru kwani malori ya Tanzania ni mengi kuliko ya
Rwanda.
Kama hali ingebaki kama ilivyokuwa,
msafirishaji angepandisha bei ya kusafirisha mzigo na kusababisha bidhaa
kuuzwa kwa bei ya juu zaidi madukani.
Hali ya biashara kati ya Tanzania na Rwanda
imekuwa katika hali ya wasiwasi tangu ilipoamua kupandisha ushuru mara
tatu zaidi mpaka kufikia dola 500 za Marekani sawa na Sh800,000 kwa
malori ya Tanzania.
Wasiwasi huo umesababisha Mawaziri wa Fedha wa
nchi hizo kukutana kumaliza tatizo hilo kwa kurudisha viwango vya awali.
Pamoja na kwamba ushuru umerejeshwa katika hali ya kawaida,
umesababisha malori takribani 300 kuwa katika hali ngumu mpakani mwa
Tanzania na Rwanda katika eneo la Rusumo.
Awali ushuru huo ulikuwa Dola 152 za Marekani sawa
na Sh243,200, lakini madereva wa Tanzania walipigwa butwaa ghafla
walipotakiwa kulipa Dola 500 za Marekani sawa na Sh800,000 na
kusababisha malori takribani 200 kukwama mpakani hapo kutokana na
kushindwa kulipa kiwango hicho.
Kutokana na malori hayo kuwa mengi foleni ilifikia kiasi cha kilometa 20 kutoka Rusumo mpaka Benaco.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Dk Charles Tizeba
alilazimika kuzungumza na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Profesa Silas
Rwakabamba na walikubaliana kuongeza wiki moja ili malori hayo ya
Tanzania yapite kwa kutumia ushuru wa zamani wakati yakisubiri ushuru
mpya kuanza.
Tatoa wanasemaje?
Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wa Mizigo
Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay anasema Serikali imechukua uamuzi wa
busara kushusha ushuru kwani malori ya Tanzania ni mengi kuliko ya
Rwanda.
Anasema Tanzania ina wastani wa malori 200 hadi
300 yanayofanya safari zake nchini Rwanda wakati Rwanda ina malori
yasiyozidi 20 ambayo yanafanya safari zake Tanzania kwa hiyo Tanzania
bado ina nafasi kubwa kibiashara.
Lukumay anasema makubaliano ambayo yamefikiwa kati
ya nchi hizo, ni mwanzo mzuri kwa kuwa matatizo kama hayo yapo katika
mpaka kati ya Tanzania na Zambia.
“Tusisubiri mambo yaharibike huku ndipo tuanze kuhangaika, yashughulikiwe sasa.
“Serikali ikae na wasafirishaji kwa ajili ya
kutatua matatizo haya mapema na tuhakikishe hayajitokezi
tena,”anatahadharisha Lukumay.
Lukumay anasema sekta ya usafirishaji inatoa ajira kwa watu
zaidi ya milioni 1 nchini, na uzuri wake ni kwamba watu wengine
tunaowapa ajira ni wale ambao hawana elimu kubwa.
Anasema kuna watu wanaonufaika katika sekta ya
usafirishaji kupitia sekta hiyo kwa mfano, gereji na biashara za mama
lishe ambazo hufanyika sehemu mbalimbali ambako malori yanasimama kwa
muda.
Anaenda mbali zaidi na kubainisha kwamba katika
Pato la Taifa (GDP), sekta ya usafirishaji imechangia kwa kiasi kikubwa
kwani mwaka jana ilichangia asilimia 5.3 ya pato lote la taifa sawa na
mwaka 2011.
Madereva wa Tanzania
Dereva wa malori, Iddi Mgaya akizungumza kutoka
Goma nchini DRC anasema licha ya gharama za ushuru kushuka, lakini
wanaona kama kuna kudorora kwa uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo
tangu Tanzania ilipotangaza oparesheni ya kuondoa wahamiaji haramu
mpakani mwa Mkoa wa Kagera na Rwanda. Jumla ya wahamiaji 6,000
walirejeshwa Rwanda hivi karibuni.
Dereva mwingine aliyejitambulisha kwa jina la
Anorld ambaye yupo Rusumo anasema hali ya mpakani hapo inawapa wakati
mgumu kwani wamekuwa wakitaabika na msongomano wa malori.
Anabainisha kwamba hivi sasa utaratibu wa kuvuka mpakani umekuwa mrefu tofauti na siku zilizopita.
Anorld anasema hajaridhishwa na kitendo cha
Tanzania kushusha ushuru kwani kuna tofauti kubwa ya umbali wa kilometa
kutoka Dar es Salaam mpaka Rusumo na Rusumo hadi Kigali.
Dereva mwingine anayefanya safari kati ya nchi
hizo mbili, Mwalimu Twaha anasema Serikali hizo kama zisingekubaliana
kungetokea athari kubwa kiuchumi kwa madereva, wasafirishaji, wamiliki
wa malori na wananchi wa nchi zote mbili.
“Kama hali ingebaki kama ilivyokuwa, msafirishaji
angepandisha bei ya kusafirisha mzigo jambo ambalo lingesababaisha
kuuzwa kwa bei ya juu zaidi madukani.
“Kazi zetu madereva zingepungua kwa sababu ya
ukubwa wa gharama na sisi madereva tungekosa kazi,” anasema Twaha ambaye
amekuwa akifanya kazi hiyo kwa miaka 13 sasa,” anabainisha.
Twaha anaweka wazi kwamba wasafirishaji wengi wa
mizigo wanapenda kwenda Rwanda kuliko nchi nyingine kwa sababu ni karibu
(kuna umbali wa kilometa 1,460 kutoka Dar es Salaam hadi Kigali),
lakini pia hakuna usumbufu.
CHANZO: MWANANCHI
“Rwanda ni njia ambayo siyo ngumu tofauti na nchi nyingine
unaweza kwenda Rwanda hata mara nne ndani ya mwezi mmoja, ni rahisi
unapofika ukishusha mzigo unaweza ukageuka na kurudi Dar es Salaam siku
hiyohiyo,” anasema.
Chama cha wasafirishaji
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanexa, Mtemi Naluyaga
anasema sakata la Rusumo limesababisha hasara kwa baadhi ya
wasafirishaji wa bidhaa kutokana na malori mengi kukwama kwenye mpaka
huo, kwani wafanyabiashara ni watu wanaopanga hesabu lini bidhaa zao
zitafika mahali husika na kuuzwa.
Naluyaga anasema mpaka wa Rusumo siyo kwa ajili ya
bidhaa zinazopelekwa Rwanda pekee bali hata nchi ya Jamhuri ya
Demokrasia ya Kongo (DRC).