MBUNGE
wa Arusha mjini Godbles Lema amewaomba viongozi wa dini nchini
kuwaombea viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na
kuliombea taifa katika kipindi hiki kigumu cha mchakato wa katiba mpya
ambayo imeanza kuleta shida.
Lema
alitoa ombi hilo juzi mjini hapa katika harambee iliyofanyika katika
Kanisa la Mtakatifu Frandis Ksavery Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Parokia
ya Olosipa, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
“Naomba
mtuombee kwani tumedhamiria kuwapigania wanyonge ndani na nje ya Bunge
na hatujali majina yoyote tutakayoitwa kwa kuwa tunaamini lengo letu ni
kuwakomboa Watanzania hivyo kama tutaitwa majina mabaya kwa lengo hilo
basi na tuitwe,” alisema Lema.
Katika Harambee hiyo, jumla ya sh milioni 43, zilipatikana ambapo Lema na marafiki zake walichangia sh milioni 10.
Fedha
hizo zilizopatikana ni sehemu ya sh milioni 120 zinazohitajika kwa
ajili ya ujenzi wa nyumba ya padri wa kanisa hilo ambaye hivi sasa
anaishi katika nyumba ya kupanga.
Awali
akizungumza kabla ya kuanza kwa harambee hiyo, Kaimu Askofu Mkuu wa
Jimbo Katoliki, Arusha Padri Simoni Tengesi, alisema mbali ya ujenzi wa
nyumba hiyo, kanisa lake lina mpango wa kujishughulisha na huduma za
kijamii ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali na huduma nyingine za
wananchi wote bila kujali madhehebu yao.