Na Fredy Azzahi, Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Dk Msonde alisema kuwa, likizo ya Dk Ndalichako ilianza Oktoba Mosi mwaka huu na itamalizika Septemba mwakani.
Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani Nchini (Necta),Dk Joyce Ndalichako, ameanza likizo ya mwaka
mmoja kwa kile kilichoelezwa kuwa anafanya utafiti juu ya uendeshaji wa
mitihani nchini.
Akizungumza na Mwananchi jana, Dk Charles Msonde
ambaye ndiye anayekaimu nafasi ya Katibu Mtendaji wa Necta, alisema Dk
Ndalichako amechukua likizo ya mwaka mmoja kwa ajili ya kufanya utafiti
huo.
Dk Msonde alisema kuwa, likizo ya Dk Ndalichako ilianza Oktoba Mosi mwaka huu na itamalizika Septemba mwakani.
“Amechukua sabbatical leave, kwa wanataaluma ama
watu walio kwenye ngazi kama zetu wanaweza kuchukua likizo kama hii.
Yeye atakuwa anafanya utafiti unaohusu uendeshaji wa mitihani hapa
nchini na pia ataangalia mambo ya matumizi ya alama za maendeleo za
mwanafunzi (continuous assessment – CA),” alisema Dk Msonde:
“Utafiti huo utakuwa na manufaa kwa shirika na kwa
kuwa yeye ni Rais wa Mabaraza ya Mitihani Afrika atapata nafasi ya
kuangalia wenzetu wanafanya nini, kwa hiyo utafiti wake ataufanya ndani
na nje ya nchi. Utafiti huu utakuwa na manufaa kwa baraza na nchi
nzima.”
Agosti mwaka huu Mwananchi ilifanya mahojiano
Maalumu na Dk Ndalichano ambapo alizungumzia vitu mbalimbali ikiwamo
kile alichosema ni tishio kwa Necta.
Alisema kuwa,kitu ambacho anaona ni tishio kwa baraza hilo ni mitizamo ya watu ambao kwa kiasi kikubwa wanakataa ukweli.
“Suala la ukweli unataka lisiwe kweli, mimi naona
hiyo ni hatari mbaya zaidi, huwezi kutibu tatizo bila kujua ukweli, ili
tuweze kuboresha elimu lazima tukubali ukweli na kujirekebisha,” alisema
Dk Ndalichako.
Alizungumzia pia ubora wa mitihani na kusema, mitihani inayotungwa na Necta ubora wake upo juu pamoja na usahihishaji wake.
Alisema mfumo wa kila mwalimu anasahihisha swali
lake ni wa kipekee na Tanzania ni moja kati ya nchi za mwanzo kutumia
mfumo huo.
“Kuna nchi mtu anapewa burugutu la mitihani ya
watoto anaenda nayo nyumbani kusahihisha akishamaliza analeta majibu
kisha watoto wanatangaziwa. Sisi mfumo wetu ni bora na sijui kwa nini
watu wanakuwa na mtizamo hasi na Necta, sifa kubwa ya baraza lolote lile
la mitihani ni kutoa majibu yanayofanana na hali halisi ya elimu
ilivyo” alisema.
“Kwetu sisi tunachotaka siku zote kuona mtu
anapewa kile anachostahili, watu wengine wanasema mitihani inayotungwa
na kupewa watoto wote siyo sawa kwa sababu kuna baadhi ya shule walikuwa
hawana walimu au vitabu, sasa swali la kujiuliza nani alitakiwa kutoa
hivyo vitabu?” alisema Dk
Ndalichako.
SOURCE: MWANANCHI
Ndalichako.
SOURCE: MWANANCHI