Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac),Zitto Kabwe amevilipua vyama vya
siasa kwa uvunjaji wa sheria na kusimamisha ruzuku ya kila mwezi hadi
vitakapowasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha za umma tangu mwaka 2009
kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Pia kamati hiyo itawaweka kitimoto makatibu wakuu
wa vyama vya siasa vinavyopata ruzuku ili wajieleze ni kwa nini
hawajawasilisha taarifa hiyo hadi sasa.
Alisema hayo jana wakati kamati hiyo ilipokutana na Msajili wa Vyama vya Siasa katika Ofisi ndogo za Bunge.
Zitto alisema tangu mwaka 2009 vyama tisa vya
siasa vinavyopewa ruzuku na Serikali vilipata jumla ya Sh67.7 bilioni
lakini havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ruzuku kwa msajili
kama vinavyopaswa kufanya hivyo kisheria.
“Ninaagiza msajili kuanzia sasa ruzuku isitolewe
kwa chama chochote cha siasa hadi hapo kitakapowasilisha ripoti ya
ukaguzi wa hesabu tangu mwaka 2009 hadi sasa na makatibu wataitwa ili
wajieleze kwa nini hawajafanya hivyo,” alisema.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nauye alipoulizwa jana alisema: “Ninahitaji muda
kuangalia kama kweli taarifa hiyo haijawasilishwa na sheria inasemaje
kuhusu suala hilo,” alisema.
Alisema baada ya siku mbili za kazi atakuwa na majibu ya kuridhisha kuhusiana na suala hilo.
Viongozi wengine wa vyama vya siasa vinavyopata
ruzuku, hawakupatikana kuelezea hali hiyo. Zitto aliongeza,“ Hivi ni
vyama vya siasa ambavyo wakati ukifika vinaweza kuja kuongoza Serikali,
lakini inashangaza ni kwa nini vinatumia fedha za walipakodi bila
kukaguliwa, huu ni uvunjaji wa sheria.”
Kwa mujibu wa Zitto, vyama hivyo na fedha za
ruzuku walizopata kwenye mabano tangu mwaka 2009 ni CCM (Sh50.9
bilioni), Chadema (Sh9.2 bilioni) na CUF (Sh 6 bilioni).
Vingine ni NCCR-Mageuzi(Sh677 milioni),UDP (Sh333
milioni), TLP (Sh217 milioni), APPT-Maendeleo (Sh217 milioni), DP (Sh3.3
milioni) na Chausta (Sh2.2 milioni).
Zitto alisema ingawa jukumu la ukaguzi wa fedha za
umma ni la ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali lakini
hakufanya hivyo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.
Alisema vyama vya siasa viliagizwa kufanya ukaguzi
kwa kutumia kampuni binafsi kama vilivyokuwa vikifanya zamani hadi hapo
ofisi ya CAG itakapopata fedha.
SOURCE: MWANANCHI
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa msajili kuviagiza vyama vya siasa kutenga sehemu ya fedha za ruzuku kwa ajili ya ukaguzi.
Alisema viongozi hao waone kwamba suala la ukaguzi
wa fedha za ruzuku ni muhimu ili kuleta uwazi katika matumizi ya fedha
za umma.
“Sasa kamati imeshindwa kuendelea na kazi kwa sababu hakuna hesabu zilizokaguliwa, nendeni tutawaita siku nyingine,” alisema.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi alisema vyama hivyo vimekuwa vikidai kwamba havina
ruzuku ya kufanya ukaguzi kwa kutumia kampuni binafsi.
“Kwa hiyo siwezi kuchukua fedha nikavipa vyama vya siasa kwaajili ya ukaguzi wakati hazijatengwa katika bajeti,” alisema.
Hata hivyo,Zitto alimwelekeza Mutungi kwamba fedha
za ukaguzi ziko kwenye ruzuku wanazopewa na kwamba hiyo siyo sababu ya
kuhalalishwa kutokaguliwa kwa hesabu zao.
SOURCE: MWANANCHI