KESI ya Bibi Titi na wenzake saba iliendeshwa kwa siku 127 mwaka 1970 na walihukumiwa kifungo cha maisha jela.
Wakati mmoja, Rais Mwalimu Nyerere kwa kujiamini alisema: “Ni mtu kichaa pekee ambaye anaweza kufikiria kuipindua serikali yangu au kujaribu kudhuru uhai wangu.”
Wananchi kadhaa waliyahusisha majigambo hayo na nguvu za kishirikina wakiamini nguvu hizo zilimpa kinga.
Na kweli Mwalimu Nyerere aliweza kudumu madarakani muda mrefu, kwa kuheshimiwa na kuogopwa, pengine kuliko kiongozi yeyote barani Afrika.
Kama nilivyoeleza awali, Bibi Titi alikuwa rafiki mkubwa wa Rais Julius Nyerere, hivyo alitumikia kifungo kwa miaka miwili tu kwani Aprili 1972 aliachiwa huru.
Lakini kuachiwa kwake huru kulisababisha aogopwe na rafiki zake wengi na hata mumewe aliachana naye, akawa mpweke.
Lakini 1991, wakati nchi inasherehekea miaka 30 ya uhuru, Bibi Titi alitajwa kuwa ni Shujaa wa Kupigania Uhuru.
Alifariki dunia Novemba 5, 2000 katika Hospitali ya Net Care jijini Johannesburg alikokwenda kutibiwa.
Kwa ajili ya kumbukumbu ya mama huyo, upo mtaa maarufu katikati ya Jiji la Dar es Saalam umepewa jina la Bibi Titi Mohammed.
Lakini Nyerere hakumsamehe Oscar Kambona aliyeunganishwa katika kesi hii ya Bibi Titi kwa kudaiwa kuwa alihusika kufadhili mpango wa kupindua serikali yake.
Wote tujiulize Kambona alifanya dhambi gani kubwa kiasi cha kutosamehewa na rafiki yake huyo na akakaa uhamishoni nchini Uingereza kwa miaka 25? Nelson Mandela Rais Mstaafu wa Afrika Kusini alimzidi Kambona kwa mwaka mmoja alipotupwa gerezani na makaburu. Swali lingine hivi inawezekanaje marafiki wawili walioshibana wakafikia kufarakana kwa kiasi tulichokishuhudia?
Kumbukumbu zinaonesha kuwa Nyerere na Kambona walikuwa marafiki kiasi cha Kambona kumfanya Nyerere kuwa ‘mpambe wake’ kwenye harusi iliyofanyika London, Uingereza.
Urafiki wao ulianzaje? Majibu utayapata katika mfululizo wa makala haya.
SOURCE: GPL