Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya utafiti imebaini
kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wenye elimu ya darasa la saba na wale
wasiosoma, ndiyo wanaokubaliana na utendaji kazi wa Rais Jakaya Kikwete.
Ripoti ya utafiti huo iliyopewa jina la ‘Namna
Watanzania wanavyouangalia utendaji kazi wa Bunge na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania’ ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Asasi ya
Afrobarometer, inaonyesha kuwa asilimia 77 ya waliokosa elimu ndiyo
wanamuunga mkono Rais Kikwete.
Afrobarometa ni Asasi ya Kimataifa inayojumuisha
taasisi tatu za Institute for Democracy ya Afrika Kusini, Ghana Centre
for Democratic Development ya Ghana na Political Science Department ya
Chuo Kikuu cha Michigan cha Marekani.
Mtafiti Msaidizi wa Afrobarometer, Stephen
Mwombela akisoma ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam, alisema asilimia 72 ya wale walioishia darasa la saba ndiyo
wanamuunga mkono Rais.
Wakati asilimia 23 ya watu wasiosoma ndiyo
hawamkubali Rais na asilimia 28 ya wale walioishia darasa la saba, pia
hawaridhishwi na utendaji wa kiongozi huyo.
Mwombela, hata hivyo, alisema utafiti huo
uliohusisha watu 2,400 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaonyesha
kuwa idadi kubwa ya wasomi wa kiwango cha sekondari na kuendelea
wanaunga pia mkono utendaji wa Rais, lakini siyo kwa kiwango cha juu
kama wale ambao hawajasoma.
“Asilimia 60 ya waliosoma elimu ya sekondari na
kuendelea wanaunga mkono utendaji wa Rais, lakini 40 hawakubaliani na
utendaji wake,” ilisema taarifa ya matokeo ya utafiti huo uliofanyika
kati ya Mei hadi Juni mwaka jana.
Matokeo ya utafiti huo yanatofautiana na yale ya
mwaka 2008, ambayo yalionyesha kuwa wasomi walikuwa wanamuunga mkono
Rais kwa asilimia 92.
Pia katika matokeo ya utafiti huo wa mwaka 2008, ulionyesha kuwa wasiosoma walimuunga mkono kiongozi huyo kwa asilimia 92.
Imani ya wananchi kwa Rais
Ripoti hiyo ilisema pia imani ya wananchi kwa
utendaji wa Rais imeshuka hadi kufikia asilimia 74 kwa mwaka jana,
tofauti na asilimia 94 ya mwaka 2005 wakati aliposhika wadhifa huo.
SOURCE: MWANANCHI
Pia utafiti huo uliodhaminiwa na Taasisi ya Utafiti kuhusu
Kuondoa Umaskini (Repoa) umebainisha kuwa imani ya wananchi kwa Rais
imeshuka kutoka asilimia 88 mwaka 2008 hadi asilimia 74, huku idadi ya
watu wasiokubaliana kabisa na Rais ikiongezeka kutoka asilimia 11 mwaka
2008 hadi asilimia 26 mwaka 2012.
Imani kwa Bunge
Wananchi wengi pia wameonyesha kutokuwa na imani
na mwenendo wa Bunge, kwa kulipa asilimia 76 mwaka 2012, idadi yao
ikishuka kutoka asilimia 83 ya mwaka 2008.
Imani ya wananchi kwa Bunge imeshuka katika
kipindi hiki ambalo liko chini ya Spika Anne Makinda, ambaye alichukua
uongozi mwaka 2010 wakati mwaka ule wa 2008 lilikuwa chini ya Samuel
Sitta imani ilikuwa juu. Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa watu wanaoishi
vijijini ndiyo wanaoridhishwa zaidi na Bunge kwa kupata asilimia 63,
ikilinganishwa na wakazi wa mijini ambao ni asilimia 60.
Pia imebainika kuwa wananchi wa Zanzibar
wanaridhishwa zaidi na utendaji wa Bunge kwa asilimia 64, tofauti na
wananchi wa Tanzania Bara ambao wanaridhishwa kwa asilimia 61.
“Watu waliokuwa wanakubaliana na utendaji wa Bunge
mwaka 2003 walikuwa asilimia 31, lakini mwaka 2012 idadi iliongezeka
hadi asilimia 61,” alisema Mwombela wakati akiwasilisha matokeo ya
utafiti huo unaofanyika kwa mara ya tano nchini Tanzania.
Hata hivyo, Mwombela alisema kuwa wananchi wengi
bado wanafurahishwa na utendaji wa Mahakama, lakini idadi yao imepanda
kutoka asilimia 73 kwa mwaka 2008 na kuwa asilimia 74 mwaka 2012.
Akichangia baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa, Dk
Abel Kinyondo, alisema kuwa matokeo ya utafiti huo hayajaonyesha
kuporomoka kwa imani kwa Rais badala yake yameonyesha uhalisia.
“Inawezekana imani kwa Rais haijashuka, badala
yake imekaa katika hali yake, kwa sababu kitu gani alikifanya 2008 watu
wakampenda sana, ambacho leo hii hajakifanya hadi wasimpende?” alihoji
Kinyondo. Kinyondo alionekana kushangazwa na namna Rais alivyoweza
kupata asilimia 71 wakati nchi inapita katika kipindi kigumu cha rushwa
na ufisadi.
Mwakilishi kutoka Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Victor Kimesera alisema utafiti huo una kasoro
kadhaa ikiwa ni pamoja na kumtaja Rais kuwa ndiye mwakilishi pekee wa
Serikali wakati kuna viongozi wengine wengi. “Kwa upande wa Rais
walitakiwa kuhoji viongozi wengi zaidi kwa sababu Rais siyo kiongozi
pekee yake katika Serikali,” alisema.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya
Fedha, Dk Jonas Kipokola alisema kama utafiti huo ungefanyika Mei hadi
Juni mwaka huu, huenda matokeo yangekuwa tofauti. “Siwezi kusema
yangekuwaje, lakini yasingekuwa hivyo yalivyo,” alisema Kipokola.
SOURCE: MWANANCHI