Na Joseph Zablon na Elizabeth Edward, Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Anastazia Saro ambaye ni mama mzazi wa Mwandishi wa ITV, Ufoo Saro aliuawa kwa kupigwa risasi mwishoni mwa wiki.
Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji jana
walimiminika Kibamba nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya
kuaga mwili wa Anastazia Saro ambaye ni mama wa Mwandishi wa ITV, Ufoo
Saro, aliyeuawa kwa kupigwa risasi mwishoni mwa wiki.
Wakati hayo yakijiri nyumbani, hali ya Mtangazaji
Ufoo Saro aliyepata majeraha baada ya kupigwa risasi na mzazi mwenzake
imeendelea kuimarika huku ndugu, jamaa na marafiki wakizuiwa kumwona.
Mwandishi huyo wa habari yuko kwenye uangalizi
maalumu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kile kilichoelezwa kuwa
anahitaji mapumziko ya saa 72 kabla ya kuanza kuonana na watu.
Akizungumza jana nyumbani kwa marehemu, Msemaji wa
familia, Allelio Swai alisema shughuli za kuaga zimechelewa kutokana na
taratibu za polisi na pia upasuaji ulikuwa mgumu na marehemu alitolewa
risasi tano.
Mwili wa mama yake Ufoo, ulitolewa katika chumba
cha kuhifadhia maiti saa 7 mchana na kupelekwa nyumbani kwake Kibamba
kwa ajili ya kuagwa.
Naye fundi seremala, Leonard Kiondo alisema siku
ya tukio alisikia milio ya risasi na baadaye alimwona Ufoo akiwa na
shumizi ya kulalia akikimbia huku akivuja damu kabla ya kumuhifadhi na
baadaye kumuwahisha hospitali kwa usafiri wa bodaboda.
Iliwachukua polisi saa moja nzima kabla ya kufika
eneo la tukio. Mwili wa Anastazia ulisafirishwa jana jioni kwenda
Machame, Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro kwa maziko yatakayofanyika
leo.
Swai alisema maziko hayo yatafanyika baada ya ibada itakayofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Uraa.
Katika hatua nyingine, ndugu, jamaa wa mzazi
mwenzake Ufoo marehemu walikutana kwa mara nyingine jana kwenye Hoteli
ya 92, kupanga taratibu za maziko ya ndugu yao Antery Mushi aliyejiua
kwa kujipiga risasi.
Kaka wa marehemu, Andrea Mushi alisema jana kuwa
wanakutana kupanga taratibu hizo kabla ya kuusafirisha mwili wa marehemu
kwenda Moshi kwa mazishi yatakayofanyika kesho.
Hospitali ya Taifa Muhimbili
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Aminiel Aligaesha alibainisha kuwa hali ya Ufoo inaimarika
ukilinganisha na mara ya kwanza alipofikishwa hospitalini hapo.
“Nimezungumza na daktari anayemshughulikia anasema maendeleo
yake kiafya ni mazuri ingawa haruhusiwi mtu yeyote kwenda kumuangalia
kulingana na tiba anazokabiliana nazo”alisema Aligaesha.
Hata hivyo, Aligaesha alikataa kuzungumzia ripoti
ya daktari kuhusiana na idadi ya risasi zilizotolewa katika mwili wa
Ufoo kwa madai kuwa hiyo ni siri ya mgonjwa.
“Sina chochote cha kusema zaidi ya anaendelea
vizuri mambo mengine ni siri ya mgonjwa na daktari atakapoamua mwenyewe
atawaambia lakini sina jukumu hilo.”
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI