Thursday 10 October 2013

Lipumba, Mbowe, Mbatia kutinga Ikulu Jumanne

10th October 2013
  JK, Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF wapongezwa
Wenyeviti vyama vya Siasa Nchini Tanzania
Rais Jakaya Kikwete na wenyeviti wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, sasa watakutana kwa ajili ya mazungumzo kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013, unaodaiwa na vyama hivyo kuwa una kasoro, Ikulu, Jumanne wiki ijayo.

Makubaliano ya kukutana siku hiyo, yamefikiwa na pande mbili hizo, saa chache baada ya wenyeviti hao (Profesa Ibrahim Lipumba-CUF), Freeman Mbowe-Chadema na James Mbatia-NCCR-Mageuzi) kutangaza kukubaliana na suala hilo na kuahirisha maandamano na mikutano ya hadhara iliyokuwa ifanyike nchi nzima leo.

 Maandamano na mikutano hiyo iliandaliwa na vyama hivyo kwa lengo la kudai ushirikishwaji wa pande zote mbili za Muungano kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya nchi na kupinga mchakato huo kuhodhiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Ushirikiano wa Vyama hivyo, Julius Mtatiro, aliliambia NIPASHE jana kuwa mawasiliano kati ya Ikulu na vyama hivyo yameshaanza.

Mtatiro alisema katika mawasiliano hayo, ambayo yamefanyika kwa njia ya simu, pande mbili za viongozi hao zimekubaliana kukutana kwa ajili ya mazungumzo hayo Jumanne ya Oktoba 15, mwaka huu, saa 4:00 asubuhi. “Viongozi wamekubaliana mazungumzo yawe Jumanne tarehe 15 Oktoba. Tunasubiri barua rasmi kwa mujibu wa mawasiliano na makubaliano hayo,” alisema Mtatiro.

“Hivyo, Ikulu bado haijatufikishia barua na wanasema barua zitakuja kati ya Ijumaa au Jumatatu. Lakini  appoitment (miadi-ya kukutana siku hiyo) iko confirmed (imethibitishwa).”

Rais Kikwete alianzisha mawasiliano na viongozi wa vyama vya siasa kwenye hoja kuhusu muswada huo uliopitishwa karibuni na Bunge kwa nia ya kuandaa mkutano kati yake na viongozi wa vyama hivyo.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari Jumatatu wiki hii ilisema mawasiliano hayo yalianza siku hiyo kufuatia maelekezo ya Rais Kikwete kwenye Ofisi ya Katibu wa Rais.

Ilisema kufuatia matukio yaliyotokea bungeni wakati wa kujadiliwa na kupitishwa kwa muswada huo mwezi uliopita, maneno na kauli mbalimbali, ambazo zimetolewa na wabunge wa vyama vya upinzani na wadau wengine kufuatia kupitishwa kwa Muswada huo na Bunge, Rais Kikwete katika hotuba yake kwa wananchi Ijumaa iliyopita alisema hoja na kauli za wanaopinga muswada huo zinazungumzika kwa nia njema ya kutafuta mwafaka katika mchakato wa kutafuta Katiba mpya.

Wabunge wa vyama hivyo, walisusia Bunge na kutoka nje wakati wa kujadili na kupitishwa kwa muswada huo wakidai kuwa ulikuwa na kasoro kadhaa.

Kasoro hizo ni kutoshirikishwa kwa Zanzibar, madaraka ya Rais ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kuvunjwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kuwasilisha Rasimu badala ya kuendelea kuwapo hadi kura ya maoni.

KAULI YA  BAKWATA:
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaad Mussa, alisema Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya upinzani wamefanya jambo la kheri na la manufaa kwa taifa. “Mnapokaa mezani na kuzungumza mnapata rehema kwa Mwenyezi Mungu, kugombana na kulumbana ni kukaribisha shetani. Hivyo, kitendo hicho ni cha kiungwana na kinapaswa kuigwa,” alisema Sheikh Alhaad.

LHRC yanena:
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema kitendo hicho ni chanya na ni kizuri kuigwa na kiongozi yeyote.
Alisema nia kubwa ya nchi ni kupata katiba iliyo bora na kueleza kuwa mwafaka ni kuelewana.

 Dk. Bisimba alisema kuitwa kwa viongozi wa upinzani ni demokrasia nzuri inayoonyesha Rais kutohitaji nchi kuingia katika machafuko.

KAULI YA ICD
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Habari kuhusu Ulemavu Tanzania (ICD), Fredrick Mkatambo, alisema ni jambo zuri na la busara alilolifanya Rais Kikwete kukutana na viongozi hao.

Aliwashauri viongozi wa vyama hivyo kuitumia nafasi hiyo vizuri kwa kumshauri Rais kuondoa na kuweka vipengele vizuri vyenye manufaa kwa umma na siyo maslahi yao binafsi.

PROF. BAREGU
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Profesa Mwesiga Baregu, alisema ni kitendo cha busara kilichoonyeshwa na viongozi hao pamoja na Rais kukutana na kuzungumza.

BASHIRU ALLY

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Bashiru Ally, alisema ni hatua muhimu iliyofikiwa baina ya viongozi hao wa siasa na Rais.

Alishauri Rais kukutana na makundi mengine kama vile wanaharakati, asasi zisizo za kiserikali, wanahabari na wasomi kujadili jambo hilo na siyo vyama vya siasa peke yake.

KAULI YA CCT

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mapesa John, alisema hatua hiyo ya Rais kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ni jambo jema na la hekima.

Alisema CCT kama jumuiya inayohubiri amani nchini imependezwa na hatua iliyofikiwa na pande hizo mbili.

TANGA
Wakazi wa jiji la Tanga na viunga vyake walitoa maoni tofauti, baadhi walipongeza na wengine kuupinga uamuzi huo wakidai kuwa ni udhaifu wa vyama hivyo na kujipendekeza kwa Rais Kikwete. Rose Andason alidai hatua ya viongozi hao kusitisha maandamano itawafanya wananchi kufikisha wanayoyataka kwa Rais na siyo vikao vya mezani kwa kuwa serikali siyo sikivu.

MOROGORO

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, ambaye kwa sasa yupo mkoani Morogoro, Joel Mmasa, alisema uamuzi huo wa Rais Kikwete, ni wa busara.

Alisema pia kitendo cha viongozi wa upinzani kusitisha maandamano yao ni cha kupongezwa kwani wameonyesha hawana nia ya kufanya vurugu na kuhatarisha amani, bali wanataka kutetea maslahi ya Watanzania.

Mwanasheria wa Kituo cha Haki za Binadamu na Utetezi wa Watoto na Wanawake, Aman Mwaipaja, alisema hatua ya viongozi wa upinzani kukubali kukutana na Rais Kikwete ni ukomavu wa kisiasa na inaonyesha wazi wana uchungu na nchi.

ARUSHA
Mwanasheria na wakili wa kujitegemea, Emmanuel Saringe, alisema jana kuwa wapinzani walitaka kufanya majadiliano hayo iwapo Rais angekataa kukutana nao. Lakini akasema baada ya Rais Kikwete kukubali kukutana na kuzungumza nao, hawakuwa tena na sababu ya msingi ya kufanya maandamano.

Imeandikwa na Muhibu Said na Gwamaka Alipipi, Dar; Ashton Balaigwa, Morogoro; Dege Masoli, Tanga na John Ngunge, Arusha.
 
CHANZO: NIPASHE