Na Tausi Ally, Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni ile inayohusu kutakatisha fedha haramu takriban Sh6 bilioni kati ya mwaka 2009/10.
Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kutakatisha
fedha haramu zaidi ya Sh6 bilioni, inayomkabili aliyekuwa mfadhili wa
mgombea urais wa Kenya, Raila Odinga, Donbosco Gichana (34) bado
haujakamilika.
Hayo yalielezwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi,
Tumaini Kweka alipokuwa akiiomba mahakama iridhie mshtakiwa huyo
achukuliwe kwenda kuhojiwa polisi kwa muda wa siku saba.
Kweka alimweleza Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Ilvin Mugeta kuwa, anaiomba mahakama iruhusu
mshtakiwa Gichana kupelekwa polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na
shtaka hilo linalomkabili.
Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Hakimu Mugeta
aliridhia mshtakiwa huyo kuchukuliwa kwa muda wa siku saba kwa ajili ya
mahojiano.
Gichana alipanda kizimbani kwa mara ya kwanza
mwanzoni mwa mwaka huu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi,
Emilius Mchauru.
Mshtakiwa huyo alifikishwa kwa mara ya kwanza
mahakamani hapo, mwanzoni mwa mwaka huu na kusomewa mashtaka mawili ya
kutakatisha fedha haramu.
Katika shtaka la kwanza, Gichana anadaiwa kukutwa
akiwa na washtakiwa wengine ambao hawajulikani kati ya Novemba 2009 na
Agosti 2010 jijini Nairobi, Kenya, Arusha na Dar es Salaam wakila njama
ya kutakatisha fedha haramu.
Wakili wa mshtakiwa huyo, Semu Anney alidai mteja
wake alikuwa mfadhili mkuu wa Raila Odinga katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2007, Kenya na ndiye aliyempa gari aina ya Hammer kwa ajili ya kufanyia
kampeni wakati huo.
Inadaiwa mshtakiwa alifanya kosa hilo kinyume cha
kifungu namba 12 cha sheria ya kuzuia utakatishaji fedha haramu namba 12
ya mwaka 2006.
Katika shtaka la pili, Gichana anashtakiwa kuwa
kati ya Novemba 2009 na Agosti 2010 kwa kupotosha ukweli wa chanzo cha
fedha alizokuwa nazo, alihamisha Dola za Marekani 4.9 milioni na
kuziweka katika akaunti namba 02J1036325000 inayomilikiwa na Moyale
Precious Germs Enterprises.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa alihamisha tena kwa
kutumia hundi kutoka tawi la Benki ya CRDB Tawi la Meru mkoani Arusha
kwenda Makao Makuu ya benki hiyo Dar es Salaam kwa nia ya kufanya
utaratibu wa kuzitoa huku akijua hundi hiyo ni ya kughushi.
Mshtakiwa huyo hakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI