Wednesday, 16 October 2013

Mtoto wa Nyerere avunja ukimya-2


Mtoto wa kwanza wa Hayati Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere 


Posted  Jumatano,Oktoba16  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Leo tunaendelea na mahojiano ya mtoto wa sita wa Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere ambaye anazungumzia mambo mbalimbali ya kitaifa na familia ya Mwalimu Nyerere...Endelea

Tatizo mojawapo liliibuka wakati tukishiriki mijadala ya kuandaa muswada wa sheria lilikuwa umiliki wa hotuba za Mwalimu Nyerere. Kwa mujibu wa wawakilishi wa Serikali ni kuwa hotuba zote ambazo Rais aliye madarakani anazitoa ni mali ya Serikali. Na wawakilishi wa Serikali katika ile kamati walichukua huo msimamo kwa kuzingatia kipengele kimojawapo cha Sheria ya Usalama wa Taifa.
Nakumbuka walisema mambo mawili: Kwanza, kuwa nyaraka yoyote yenye nembo ya Serikali inayotumika kuandikia suala lolote ni mali ya Serikali. Pili, kuwa nyaraka yoyote anayeiandaa mtumishi wa Serikali akiwa madarakani ni mali ya Serikali. Kwa mantiki hii, Rais anayeandika (au kuandikiwa) hotuba akiwa madarakani hamiliki hizo hotuba. Hizo ni mali ya Serikali.
Kama hii ndiyo fasiri sahihi ya sheria hii mimi naona ina hitilafu kubwa. Nakubali kuwa karatasi aliyotumia Mwalimu Nyerere kuandikia hotuba zake ni mali ya Serikali, lakini sikubali kuwa mawazo yake yanaweza kuwa mali ya Serikali. Unawezaje kumiliki mawazo ya kiongozi yeyote yule?
Tukijadili kipindi cha utawala wa Serikali ya Tanzania kati ya 1961 hadi 1985 alipostaafu, ni nadra kuzungumzia ‘mawazo ya Serikali ya Tanzania’ lakini tunazungumza kila wakati kuhusu ‘mawazo na fikra za Mwalimu Nyerere’.
Kwa mujibu wa Serikali kama haya ‘mawazo na fikra za Mwalimu Nyerere’ yameandikwa kwenye karatasi yenye nembo ya Serikali na iwapo yalitolewa yeye akiwa Rais, basi vyote hivyo ni mali ya Serikali. Zaidi ya hayo kuna matukio ambayo ambayo yanaleta mkanganyiko zaidi kuhusu huu msimamo wa Serikali. Akiwa madarakani, kampuni ya Oxford University Press ilichapisha hotuba zake na Mwalimu Nyerere alilipwa mrabaha kutokana na mauzo ya vile vitabu vyenye hotuba zake. Baada ya Mwalimu kufariki Oxford University Press waliilipa familia mrabaha, kama warithi wake, kutokana na mauzo ya hotuba hizo hizo.
Sasa tukikubali hoja kuwa hotuba zile ni mali ya Serikali kuna kasoro kisheria kwa Mwalimu kuweza kuchapisha zile hotuba akiwa madarakani na kulipwa mrabaha, na vilevile kuna kosa kisheria kwa familia yake kulipwa mrabaha na Oxford University Press.
Tunaweza kuamini kuwa kwa sababu Mwalimu Nyerere alichapisha hotuba zake akiwa madarakani, ilihitaji ujasiri mkubwa kumfahamisha kuwa alikuwa anavunja sheria.
Sasa hivi hayuko madarakani na ni rahisi sana kwa Serikali kutamka rasmi kuwa alifanya kosa na kuwa hata familia yake haikustahili kupokea malipo toka Oxford University Press. Tukiwa kwenye ile kamati tuliomba Serikali itamke hivyo, lakini mpaka leo bado haijatoa tamko.
Lakini hata ikitamka itakuwa bado kuna tatizo lingine. Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, katika mfululizo wa vitabu vilivyochapishwa na Mkuki na Nyota Publications, amechapisha hotuba zake nyingi alizotoa akiwa madarakani (1995 – 2005). Sidhani kama Mkuki na Nyota wanailipa Serikali ya Tanzania mrabaha kutokana na mauzo ya vitabu hivyo: Uwazi na Ukweli 1 – 5.
Hotuba na maandishi ya Mwalimu Nyerere vimekuwa mali ya kila mtu siku hizi, suala ambalo mimi naona si sahihi. Tupo warithi wake na tunastahili angalau kuombwa ruhusa kutumia hizo hotuba na maandishi.
Nafikiri wakati umefika kuangaliwa tena hili suala na kubainisha kasoro zinazojitokeza kwenye msimamo wa Serikali kuhusu umiliki wa hotuba za Mwalimu Nyerere. Hatusemi kuwa hotuba zote ni mali ya Mwalimu Nyerere ila tunaamini kuwa sehemu kubwa ya hotuba alizotoa akiwa madarakani na baada ya kung’atuka ni mali yake.
Mwananchi: Katika muktadha mzima wa uhusiano wa familia ya Mwalimu Nyerere na Serikali, ni wakati gani shughuli za Makumbusho ya Mwalimu Nyerere zinatofautina na shughuli za familia hasa katika makumbusho yaliyopo Butiama?

Madaraka: Kimsingi kazi wanayofanya Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere na malengo ya familia hayatofautiani sana kwa sababu nia ni kutunza/kuhifadhi na kuendeleza kumbukumbu za Mwalimu Nyerere. Inawezekana kuwa Makumbusho wanayo majukumu ya ziada, lakini lengo la msingi linafanana.
Mwananchi: Kwa jinsi siasa za nchi yetu zinavyoendeshwa, wewe binafsi una matarajio yoyote ya kuingia kwenye siasa kwa maana ya kuogombea nafasi ya ubunge au urais kama wananchi watakuhitaji?
Madaraka: Kwanza Sina mawazo ya kugombea urais. Pili ukichukulia kama uongozi ni wajibu niko tayari kushiriki chaguzi za ubunge, lakini ukichukulia uongozi kama fursa ya kuitwa “mheshimiwa” na kupata mshahara na posho ya uhakika huko sitajitokeza.
Wajibu unaoweza kunisukuma mimi kuomba ubunge ni iwapo wale wanaojitokeza kama wagombea kwenye jimbo ni watu ambao nikijipima nao naona kuwa naweza kuwa kiongozi bora kuliko wao.
Lakini nasikia kuwa kampeni za ubunge zinagharimu pesa nyingi, ambazo mimi sinazo. Kwa hiyo uamuzi wa kujiingiza kwenye kampeni za aina hii unaibua maswali mengine mengi. Nikope pesa kugombea ubunge? Siwezi. Niombe pesa kugombea ubunge? Kwa nani? Kwa masharti gani? Kuna mtu atatoa pesa bila kutarajia faida fulani?
Nikipata msukumo wa huo wajibu, na nikipata majibu yenye kuridhisha ya baadhi ya haya maswali (na mengine ya aina hiyo) nitaingia kwenye pirikapirika za siasa.
Mwananchi: Unavitazama vipi vyama vya upinzani nchini, unadhani kwa jinsi vinavyoendeshwa ni ipi nafasi yao katika chaguzi zinazokuja kwa maana ya kupata nafasi ya kuongoza nchi (urais)?
Madaraka: Vyama vya upinzani vina jukumu kubwa la kimfumo la kukihangaisha, kwa kukosoa sera na utendaji, CCM na inapowezekana kukiondoa madarakani kupitia chaguzi ili wale wanaokuwa na fikra kuwa kuongoza serikali ni suala la kudumu watafakari vyema wanapochukuwa uamuzi unaoathiri maisha ya wananchi.
Mara nyingi wanaokaa madarakani muda mrefu hufikia kujisahau, hasa pale vyama vya upinzani vinapokosa nguvu ya kisiasa.
Lakini katika chaguzi za 2010 tumeona kuwa Chadema kimepata nguvu kubwa kuliko ambavyo imewahi kutokea kwa chama cha upinzani tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi.
Iwapo Chadema na vyama vingine vya upinzani vinataka kuongeza mafanikio katika uchaguzi unaokuja, basi hawana budi kushirikiana katika kukikabili Chama Cha Mapinduzi.
Lakini iwapo vyama vya upinzani vitafanikiwa dhidi ya Chama Cha Mapinduzi kutategemea pia wagombea wa urais ambao watateuliwa kuwakilisha vyama vyao.

Kuna viongozi ambao wanahusishwa na upungufu katika uadilifu, na uteuzi wao kama wagombea kwa upande wa CCM unaweza kuongeza nguvu ya vyama vya upinzani. Kwa kifupi, siyo rahisi kuzungumza sasa kuhusu yanayoweza kutokea kwa kuwa masuala mengi hayajajulikana.
Kwa nyongeza, mimi naamini baadhi ya viongozi wa upande wa upinzani wanapaswa kuonekana kuwa ni viongozi ambao wanastahili kukabidhiwa nchi kuongoza. Kwa mfano, iwapo yule mbunge aliyetolewa kwa nguvu bungeni ameteuliwa kuwa waziri mwaka 2015, baada ya chama chake kushinda Uchaguzi Mkuu, pale anapotofautiana mawazo na rais au waziri mkuu wake tutegemee kuwa ataendelea kuonyesha tofauti zake za mawazo kwa njia ya vitendo, na siyo kwa kujenga hoja?
Kwa mtindo huo Baraza la Mawaziri litahitaji mabaunsa. Lakini nikisema hivi wala sidharau nguvu ya chama chake.
Natoa hisia tu ambazo naamini wapigakura wengi wanaweza kuwa nazo na ambazo zinaashiria kuwa labda ni vyema kurekebisha utaratibu wa kukabiliana na upinzani wa kisiasa.
Kwa kusema “kurekebisha utaratibu wa kukabiliana na upinzani wa kisasa” namaanisha kuwa wale wanaoona kuwa nguvu ndiyo suluhisho la kutoelewana waanze kutumia hoja zaidi kusisitiza yale ambayo wanaamini yanakiukwa na wapinzani wao. Wawaelimishe na kuwashawishi wapigakura ili watambue hizo hitilafu na hatimaye wale wanaodhaniwa hawazingatii misingi ya haki na usawa katika harakati za ushindani wa siasa waweze kuondolewa madarakani kwa njia ya kura.
Kuna hatari ya mifano ya aina hii kupenyeza katika maisha ya kila siku ya wananchi ambao wataona kuwa njia pekee ya kutafuta haki ni kutumia nguvu.


SOURCE: MWANANCHI