Monday 14 October 2013

Vyama visivyo na wabunge vyafuata nyayo za Lipumba, Mbowe, Mbatia

14th October 2013
Rais Jakaya Kikwete
Vyama  16 vya siasa vyenye usajili wa kudumu visivyokuwa na uwakilishi bungeni vimeomba kukutana na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya nchi.

Vyama hivyo ni UMD, NLD, UPDP, NRA, Tadea, Demokrasia Makini, Chausta, DP, APPT-Maendeleo, Jahazi Asilia, Sau, AFP, CCK, ADC na Chaumma.

Hatua hiyo imefikiwa na vyama hivyo, siku chache baada ya Rais Kikwete kuvialika Ikulu vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, ambavyo vina uwakilishi bungeni, kwa ajili ya mazungumzo kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013, uliolalamikiwa na vyama hivyo kuwa una kasoro.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wakuu wa vyama hivyo jana, Hashim Rungwe kutoka Chaumma, alisema tayari wamekwishawasilisha Ikulu barua ya kuomba kukutana na Rais Kikwete kwa ajili hiyo, tangu Oktoba 11, mwaka huu.

Rungwe, ambaye aliwahi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kwa tiketi y NCCR-Mageuzi, alisema ombi lao limezingatia busara alizonazo Rais Kikwete za kupendelea meza ya mazungumzo kumaliza hitilafu zao.

"Mheshimiwa Rais vyama hivi vimeona ni busara kukuomba uvipe fursa ya kuonana na wewe hasa kwa kuzingatia busara zako ambazo umekuwa ukitufunza kila siku za kupendelea meza ya mazungumzo kumaliza hitilafu zetu, tunakupongeza sana na tuna imani utatupa fursa hiyo ya kukutana na wewe," ilieleza sehemu ya barua iliyosainiwa na viongozi wakuu wa vyama hivyo.

Mbali na kuomba kukutana na Rais, vyama hivyo pia vimependekeza mambo matatu, ambayo Rungwe alisema yamo katika orodha ya mambo watakayozungumza na Rais; ikiwamo la kutaka kila chama chenye usajili wa kudumu kipewe nafasi katika Bunge Maalumu la Katiba zisizopungua tatu.

Mapendekezo mengine, vyama hivyo vinataka vyama vya CCM, CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi havistahili nafasi hizo tatu, majina matatu kwa vyama stahili yatangazwe na Rais kwa upendeleo wa chama husikana na jambo lolote litakalohitajika kupigiwa kura ndani ya Bunge hilo lipitishwe kwa theluthi mbili ya wajumbe kwa Tanzania Bara na theluthi mbili kwa Zanzibar.

Rais Mtendaji wa APPT-Maendeleo, Peter Mziray, alisema vyama hivyo 15 havipaswi kubezwa kwa kutokuwa na wabunge, kwani bado vina uwakilishi katika serikali za mitaa na kwenye udiwani, ambako ndiko nchi inakoendeshwa.
CHANZO: NIPASHE