Monday 14 October 2013

Wasomali jela miaka 42 kwa kuingia kinyemela

14th October 2013
Baadhi ya Rai wa Somalia wakiwa wamekamatwa baada ya kugundulika wakaisafirishwa katika Malori ya mizigo.
Mahakama ya Mkoa wa Lindi, imewahukumu raia watano wa Kisomali kifungo cha jumla ya miaka 42 jela baada ya kupatikana na makosa mawili likiwamo la kukutwa wakimiliki kinyume cha sheria silaha mbalimbali za kivita kwenye Bahari ya Hindi.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Dustan Ndunguru, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Wasomali waliohukumiwa adhabu hiyo ni Mahmoud Hassani Warsame, Ismail Abdallah Shekh, Abubakary Mohamed Abdillahi, Ally Abdullah Ahmed na Hassan Ally Nur.

Washtakiwa walipewa fursa ya kujitetea ambapo kila mmoja kwa nyakati tofauti aliiomba mahakama imuonee huruma kwa madai kuwa siyo raia wa Tanzania na walikuwa wakipita tu kuelekea Afrika Kusini.

Kuhusu kukutwa na silaha walidai kuwa zilikuwa ni kwa ajili ya kujihami na vita vinavyoendelea nchini kwao Somalia.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Juma Maige, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa hao kwa kuwa silaha walizokamatwa nazo ni za hatari.

Hakimu Ndunguru aliwahukumu kwa kosa la kwanza la kukutwa na silaha za kivita kifungo cha miaka saba jela kila mmoja na miaka saba kwa kosa la pili la kukutwa na risasi bila ya kibali na hivyo kufanya jumla ya kifungo cha miaka 42 jela. Mwanzoni ilidaiwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali Juma Maige, kuwa washtakiwa wote kwa pamoja walikamatwa Aprili 18, mwaka jana kisiwa cha Mkuza wilayani Kilwa, mkoani Lindi katika Bahari ya Hindi.
Alidai kuwa washtakiwa walikutwa wakiwa na silaha za aina mbalimbali za kivita.

Alizitaja silaha hizo kuwa ni bunduki nne aina ya SMG, risasi (64), mabomu (47) ya kutupa kwa mkono na  silaha mbili za kubomolea vifaru.

Washtakiwa hao tayari wameshatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana na hatia ya kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria.
 
CHANZO: NIPASHE