Na Raymond Kaminyoge na Fidelis Butahe,Mwananchi
Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Zasema zitalazimika kusitisha matumizi ya gharama za shughuli nyingine, ili kupata fedha za kuwapa mikopo wanafunzi
Dar es Salaam. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), zitawapa
mikopo wanafunzi 1,107 kutoka katika bajeti zao, baada ya wanafunzi hao
kulalamika kukosa mikopo.
Bodi kuanzia leo, itawaita wanafunzi hao wanaochukua masomo ya vipaumbele yakiwamo ya Hisabati na Sayansi, ili kujaza fomu upya.
Hata hivyo kuna wanafunzi wengine waliokosa mikopo
kutokana na kushindwa kujaza fomu za kuomba, lakini masomo yao si ya
kipaumbele na hivyo kuachwa katika uamuzi huo.
Takriban wiki mbili zilizopita, zaidi ya wanafunzi
100 waliochaguliwa kujiunga katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa
mwaka huu, waliandamana kwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa
lengo la kukutana na waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Dk Shukuru
Kawambwa, baada ya kukosa mikopo.
Wanafunzi hao walisema wamenyimwa mikopo bila kupewa maelezo ya msingi licha ya kuilalamikia bodi ya mikopo.
Uamuzi huo wa jana, umekuja baada ya Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, kuzibana wizara na bodi, ikitaka
kujua kilichosababisha wanafunzi hao kukosa mikopo.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Philipo Mulugo, alisema jana kuwa baada ya kutafakari suala hilo, uamuzi
umefikiwa kuwa wanafunzi hao waitwe kujaza tena fomu za kuomba mikopo.
“ Kilichoamuliwa ni kwamba wizara na bodi
zitatakiwa kutafuta fedha kwenye matumizi mengine, ili kuwapa mikopo
wanafunzi hawa,” alisema.
Naibu Waziri huyo alisema, “Bodi itatakiwa
kutafuta fedha hizi kutoka kwenye matumizi mengine (OC), itabidi
wajinyime wasisafiri na kuachana na matumizi yasiyo ya lazima. Pia
watumie fedha za marejesho ya mikopo kugharimia wanafunzi hawa,” alisema
Mulugo.
Wanafunzi watakaofaidika na idadi yao kwenye
mabano ni wale wanaochukua masomo ya ualimu wa hisabati (20), ualimu
sayansi (164), udaktari tiba (111) na uhandisi umwagiliaji (7).
Wengine ni ualimu (617), sayansi kilimo (20), uhandisi (70) na sayansi ya jamii (98).
Mulugo alisema jumla ya Sh3.1 bilioni zinahitajika
kuwalipia wanafunzi hao na kwamba bodi itatoa Sh 2 bilioni na wizara
yake itatoa Sh1.1 bilioni.
Alisema kiasi hicho cha fedha kitakuwa kwa ajili ya chakula na
malazi, vitabu viandishi na mafunzo kwa vitendo na mahitaji maalumu ya
vitivo.
Mulugo alisema fedha kwa ajili ya ada za wanafunzi
hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa
Sifuni Mchome, atawaandikia wakuu wa vyuo wanakokwenda kuomba kuwa
Serikali itawalipa kwenye bajeti ya mwakani katika bajeti ya 2014/15.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI