Thursday 26 September 2013

Al -Shabaab ina uhusiano na Al Qaeda?


Wanamgambo wa Al-Shabaab wakiwa mazoezini. Picha na Mtandao 
Na George Njogopa, Mwananchi

Posted  Jumatano,Septemba25  2013  saa 14:49 PM
Kwa ufupi
Historia inaonyesha kuwa, Kundi la Al-Shaabab ambalo pia hutambulika kama ‘vijana’ lina uhusiano wa karibu na aliyekuwa mwasisi wa Kundi la Al-Qaeda, Osama bin Laden.Wakati Osama alipotimuliwa nchini mwake, Saudi Arabia, alisafiri hadi Somalia na kuweka makazi katika Mji wa Mogadishu.

Mbinu zao za mapambano zinafana. Pia mwasisi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden aliwahi kuishi Somalia. Hata Al Shabaab walipata mafunzo huko Afganistan alikokuwa Osama.
Mapambano ya mara kwa mara yanaweza kuifanya Afrika ififie katika uchumi na siasa za kimataifa. Bara hili linakumbana na vikwazo vingi vya kimaendeleo kutoka madola makubwa, huku ikiandamwa na makundi haramu yanayosababisha vifo na mateka wa kila aina.
Wakati wa vuguvugu la kupambana na ukoloni wa nchi za Magharibi nchi za Afrika zilizalisha watu wa aina mbalimbali – wapo viongozi wazalendo na wanamapinduzi waliofichua hila za walowezi.
Hawa walikuwa mstari wa mbele kupigania haki na uhuru wa watu wao. Wakiwa na shabaha ya kuziokomboa nchi zao na kuanzisha enzi mpya iliyotoa fursa kwa wote.
Vilevile kulijitokeza mgawanyiko wa fikra za kiitikadi uliosababisha kuzaliwa kwa makundi yanayopingana na ustarabu unaokubalika na wengi. Kutokana na makundi haya ustarabu wa kuendesha shughuli za dola kwa kufuata misingi mama na kanuni za kusikilizana ulianza kupingwa. Kiu ya kujitenga ilirejea tena Afrika,  yakazaliwa makundi ya wanamgambo na matabaka ya kikabila, kama hili la Al –Shabaab.
Hofu na shaka imerejea Afrika. Mizizi ya kundi la Al -Shaabab imesimikwa katika misingi na fikra za kujitenga na kuogopesha. Kiutendaji Al-Shabaab haijitofautishi na misingi inayosimamiwa na Al-Qaeda
Ni kundi linalopigania kuwapo kwa taifa lenye kufuata taratibu na itikadi za kidini. Linataka Somalia itambulike kama dola inayosimamia misingi inayoegemea kanuni za Kiislamu – sharia
Uhusiano na Osama bin Laden
Historia inaonyesha kuwa, kundi la Al-Shabaab ambalo pia hutambulika kama ‘vijana’ lina uhusiano wa karibu na aliyekuwa mwasisi wa Kundi la Al-Qaeda, Osama bin Laden.
Wakati Osama alipotimuliwa nchini mwake, Saudi Arabia, alisafiri hadi Somalia na kuweka makazi katika Mji wa Mogadishu.
Baadaye alishiriki vuguvugu la siasa zilizomaliza utawala wa muda mrefu wa Siad Barre aliyeondolewa madarakani mwaka 1990 na baadaye alielekea nchini Afghanistan. Al-Shabaab ambayo iliasisiwa rasmi mwanzoni mwa miaka 1990 ilianza kupata nguvu baada ya kuanguka kwa utawala wa Barre.
Idadi kubwa ya wapiganaji wake ambao wengi wao walikuwa vijana walipekelekwa Afghanistan kuungana na kundi kwa Taliban kwa ajili ya kushiriki vita vya msituni. Huko ndiko walikopata uzoefu na mbinu za vita, zinazohusishwa na mbinu za Osama bin Laden.

Walilazimika kukimbilia Afghanistan kupata uzoefu wa kivita baada ya kutimuliwa na vikosi vya Ethiopia vilivyosaidiwa na askari wa Somalia.
Ethiopia ilijiingiza kwenye mzozo wa Somalia kama sehemu ya kulinda mipaka yake baada ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotishia kusambaa hadi katika nchi za jirani.
Kimsingi, Al- Shaabab iliundwa na kundi la watu wachache waliopata elimu katika nchi zilizoko eneo la Mashariki ya Kati. Walirejea nyumbani wakiwa na misimamo mikali na kuanzisha harakatiza siasa kali.
Walishiriki kwenye operesheni za kivita na hatimaye kufanikuwa kuliteka eneo la kusinu mwa Somalia na baadaye ilitanuka hadi katika eneo la kati. Mipango mingi ya mashambulizi pamoja na matukio ya utekaji meli iliratibiwa kutoka mji wa Kismayo ambako ndiko ilikokuwa ngome yao kuu.
Kuna wakati kulizuka mtafaruku mkubwa miongoni mwa kundi hilo kuhusu na kile kilochoelezwa “Mgongano wa fikra na shabaha ya usoni”. Kulijitokeza kundi la askari wakongwe waliotaka kuanzisha tawi la kisiasa na kuingia moja kwa moja kwenye siasa za Somalia na kundi la vijana ambalo lilipigania kuendelea na agenda za kuhimiza siasa kali.
Operesheni iliyoanzishwa na Umoja wa Afrika kupitia vikosi vyake Amison, ndiyo ulilozorotesha nguvu ya kundi hilo ambalo sasa limeanzisha maficho mapya. Katika kile kilichotazamwa kama jaribio la kuzionya nchi zilizopeleka majeshi nchini humo, kundi hilo lilishambulia baadhi ya maeneo nchini Kenya na Uganda.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo katika eneo la Pembe ya Afrika wanasema kuwa, al Shaabab imeanza kujipambanua upya kama kundi linalotetea maslahi ya Somalia dhidi ya utamaduni wa nje.
Kundi hilo ambalo mwelekeo wake unafanana pia na ule wa kundi la Boko Haram la nchini Nigeria, limetumbukia kwenye lawama kutokana na mashambulizi dhidi ya raia.
Inavyoonekaana sasa al Shaabab ambayo imepoteza udhibiti katika ngome zake muhimu ikiwemo mji wa Bandari Kismayo kutokana na mashambulizi ya majeshi ya Kenya yaliyoko Somalia, inaanza kuchanga karata upya kwa kutuma ujumbe katika jumuiya ya Kimataifa kuwa bado ina uwezo wa kuendesha operesheni zake lakini katika hali ya kuvizia.
Kwa kiasi kikubwa vikosi vya Umoja wa Afrika (Amison) vimeshikilia maeneo yote muhimu na kufanikiwa kurejesha hali ya utulivu katika Mji Mkuu Mogadishi. Lakini hata hivyo kukosekana kwa dhana za kisasa pamoja na ufinyu wa askari wa kimataifa kunaweza kutoa mwanga kwa wanamgambo wa al Shaabab kujikusanya upya na kuzusha hali ya sintafahamu.


SOURCE: MWANANCHI