Kwa ufupi
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
ofisini kwake, Jaji Jundu alikanusha tuhuma hizo akisema kuwa majaji na
mahakimu wamekuwa wakitoa uamuzi kwa kuzingatia ushahidi na misingi ya
kisheria.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu imewatetea majaji na
mahakimu dhidi ya tuhuma zilizotolewa kwao kuwa waliwaachia kwa dhamana
washtakiwa wa dawa za kulevya kinyume cha sheria na kuwafanya watoroke.
Jaji Kiongozi, Fakih Jundu amesema mahakama
haipaswi kubebeshwa lawama katika hilo, bali ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP) kutokana na kutokutimiza masharti ya kisheria
wanapofungua kesi mahakamani.
Kauli ya Jaji kiongozi imekuja baada ya shutuma
zilizotolewa dhidi yao baada ya chombo kimoja cha habari (jina tunalo)
kuandika habari kwa kuwataja kwa majina baadhi ya majaji na mahakama
kuwa wamekuwa wakiwalinda washtakiwa wa dawa za kulevya katika kesi
ambazo wamekuwa wakizisikiliza.
Shutuma hizo zilihusiana na tukio la hivi karibuni
ambapo raia wawili wa Pakistani waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya dawa
za kupewa kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu na zimekuwepo taarifa
kuwa wametoroka nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, ofisini
kwake, Jaji Jundu alikanusha tuhuma hizo akisema kuwa majaji na mahakimu
wamekuwa wakitoa uamuzi kwa kuzingatia ushahidi na misingi ya kisheria.
“Kuna wakati huwa tunawaeleza DPP kuwa kuna
madhaifu katika kesi mbalimbali wanazofungua. Hivyo huwa tunawaeleza
kuwa ni vyema muwe mnajipanga sawasawa kabla ya kuzileta,” alibainisha.
Jaji Jundu alisema miongoni mwa dosari hizo ni
pamoja na kesi za dawa kufunguliwa bila kuwa na hati ya kiapo cha
kamishna wa dawa za kulevya, inayoonyesha thamani ya dawa hizo.
Alifafanua kuwa ni kweli kwamba Sheria Na. 9 ya
kudhibiti dawa za kulevya ya mwaka 1995, inazuia mtu yeyote aliyekamatwa
na dawa zenye thamani kuanzia Sh10 milioni asipewe dhamana.
Hata hivyo,alisema sheria hiyo hiyo, katika
kifungu Na. 27 (1) (b) kinamtaka, DPP kuambatanisha katika hati ya
mashtaka kiapo kinachoonyesha thamani halisi ya dawa za kulevya
alizokamatwa nazo mshtakiwa.
Kiapo hicho Jaji Jundu aliongeza kuwa kwa mujibu
wa sheria hiyo ni lazima kithibitishwe na kamishna wa Tume ya Taifa ya
Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya.
source: Mwananchi
source: Mwananchi