Na George Njogopa
Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Mwandishi Sang aliiambia mahakama kwamba kesi iliyofunguliwa dhidi yake inalenga kumkwamisha asiwe mtangazaji bora duniani.
Serikali ya Tanzania, imeiomba Mahakama ya
Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuruhusu Makamu wa Rais wa Kenya, William
Ruto kutohudhuria baadhi ya mashauri ya kesi yake ili kuweza kutimiza
majukumu mengine ya kiserikali.
Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Jaji Fredrick Mwita
aliandika barua kwenda ICC Jumatatu wiki hii akitetea hoja ya Ruto
kutaka asihudhurie baadhi ya vikao vya kesi hiyo.
Katika barua yake, Jaji Werema alisema kuruhusu
Ruto kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi kutaimarisha ushirikiano
baina ya ICC na washirika.
Hata hivyo, maombi hayo yanayotaka Ruto kuruhusiwa
kutohudhuria kesi hiyo binafsi yamesimamishwa baada ya mwendesha
mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda kuyawekea pingamizi na sasa yanasubiri
uamuzi wa majaji.
Hii ni mara ya pili kwa Tanzania, kuwasiliana na
ICC kwani iliwahi kuwasilisha ombi la kutaka kesi hiyo ya kina Ruto
isikilizwe Tanzania au Kenya.
Hata hivyo, mpango huo ulikwama baada ya majaji kuupinga kwa kura za hapana.
Mwandishi Sang ajitetea
Mwandishi wa habari wa kituo cha KASS FM Joshua
Arap Sang, amekamilisha ungwe ya kwanza ya utetezi wake kwenye Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na kueleza kuwa hakuhusika kwa namna
yoyote kuchochea machafuko yaliyojiri baada ya uchaguzi nchini Kenya.
Sang aliwasilisha utetezi wake katika hali ya
kujiamini huku akionyesha sura yenye matumaini na kuiambia mahakama
kuwa, kesi inayomkabili imetengenezwa ili kukatiza ndoto yake ya kuwa
mtangazaji bora duniani .
Mwandishi huyo ambaye anatetewa na mawakili
wanaoongozwa na Wakili Katwa Kigen, alipangua hoja zilizowasilisha na
upande wa mashtaka kwa kutumia historia ya maisha yake aliyoyaelezea
kuwa ni ya kumcha Mungu na uadilifu.
Kama ilivyo kwa washtakiwa wengine, Rais Uhuru
Kenyatta na Naibu wake William Ruto, Sang anadaiwa kuratibu na kupanga
mashambulizi na kusababisha zaidi ya watu elfu moja kupoteza maisha.
Pia anadaiwa kuendesha kampeni ya uchochezi kupitia vipindi mbalimbali vya redio baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2007.
Mbele ya jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo, Sang alisema
historia ya maisha yake inaeleza vyema namna alivyokuwa msaada kwa
jamii, ikiwamo kushiriki kikamilifu shughuli za kanisa hivyo kutuhumiwa
kuwa alihusika kwenye mauwaji ni dhihaka kubwa kwake.
“Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu ambaye kwake
yeye nimepata nguvu na kusimama hapa. Nafahamu fika ipo siku mahakama
hii itasimama katika haki na kuniachia huru. Itamwachia huru mwandishi
wa habari.
“Lakini pia napenda niiarifu mahakama hii kuwa
mimi ni kiongozi wa kwaya tena nategemewa sana na wenzangu, sasa
kuambiwa kuwa nimeratibu mauaji ya raia ni jambo linalonisononesha sana
tena limenivuruga mno,” alieleza Sang.
Katika kile kilichoonekana kama njia ya kuupa
nguvu utetezi wake, Sang mbali ya kuelezea uzoefu wa kazi yake lakini
alirudia mara kadhaa kutamka maneno yaliyotafsiri hisia zake dhidi ya
kesi hii.
“Kusema kweli haya mashtaka yamenisononesha na
kunivuruga. Mimi ni mzazi na pia ni mume mwema, itakuwaje sasa nithubutu
kufanya jambo hili la kuua wenzangu, haiwezekani. Nimesikitika na
kusononeka sana”.
Uzoefu wake
Baadaye aligeukia kipengele kilichohusu uzoefu wa
kazi yake ambapo alitetea utendaji wake akisema; wakati wote alikuwa
akifanya kazi kwa kuzingatia miiko na madili.
“Mimi ni mtangazaji wa siku nyingi tena nimefanya
kazi hii katika vituo zaidi ya vitatu ambavyo vyote ni vya kidini, sasa
huko kote nisifanye hilo la kuchochea mauaji nije kulifanya hapa Kass
FM. Hiyo siyo kweli kabisa na hii kesi imeletwa kwa ajili kunivurugia tu
safari yangu ya kuendelea kuwa mtangazaji.
Aliongeza: “Potelea mbali najua Mungu yupo na
ataendelea kunipigania. Natambua kuwa mimi nilizaliwa kuwa mtangazaji na
hadi leo nitabakia kuwa hivyo.”alisema
Aliiambia mahakama hiyo kuwa kazi ya utangazaji
alianza kuipenda alipokuwa kijana mdogo na wakati fulani alilazimika
kufuatilia matangazao yaliyokuwa yakirushwa na kituo cha BBC kwa ajili
ya kujifunza na kupata taarifa za dunia.
“Waheshimiwa majaji mimi ni msikilizaji mzuri wa
redio na kituo nilichokuwa nikikifanyia kazi Kass FM kinasikika
kimataifa, hata hapa Netherland mimi nasikiliza redio hii, hivyo nina
ufahamu wa kutosha wa kazi hii.
Napenda tu niseme haya mashtaka hayana ukweli wowote kabisa,”alisema.
Kuhusu vipindi alivyokuwa akiviendesha ambavyo vinadaiwa
kupendelea kambi ya ODM, Sang alipuuza hoja hiyo kwa kueleza kuwa,
wakati wa kampeni vyama vya siasa ndivyo vinavyolipia matangazo kwa
ajili ya kutangaza sera zao.
“Pale Kass FM mimi ni mtu mdogo kabisa, sina uwezo
wa kuamua jambo lolote lile mbali ya kufuata utaratibu uliowekwa na
mmiliki wa kituo, lakini pia kusema mimi nilipendelea kambi ya ODM kwa
kuwapa vipindi vingi hili siyo kweli kabisa, lazima tujue kwamba wakati
wa kampeni vituo vingi huuza muda kwa wanasiasa ili watangaze sera zao
ndivyo ilivyokuwa kwetu,” alieleza.
Sang pia alikanusha tuhuma za kuendesha vipindi
vya redio vinavyodaiwa kurushwa kwa kipindi cha siku tatu kuanzia
mwanzoni mwa Januari, 2008 vilivyokuwa vikiwahimiza wananchi wa kabila
la Kilinjini kuanzisha machafuko.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI