Friday, 27 September 2013

Watu 15 wafariki dunia Ziwa Tanganyika


Na Mussa Mwangoka

Posted  Ijumaa,Septemba27  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Alisema miili ya marehemu hao iliopolewa na wananchi wa Kijiji cha Kasanga, lakini majina yao hayajafahamika.


Sumbawanga. Watu 15 wakiwamo watoto 13 wamefariki dunia na wengine kadhaa wakihofiwa kufa, baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kutoka Kijiji cha Kapele, mwambao wa Ziwa Tanganyika, wilayani Kalambo, mkoani Rukwa kupigwa na dhoruba na kupinduka.
Taarifa zilizopatikana jana mjini hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, zinasema ajali hiyo ilitokea juzi mchana, eneo la kati ya Bandari ya Kasanga na Kijiji cha Kipwa.
Inadaiwa watoto hao walikuwa wakitoka Kijiji cha Kapele kupata huduma ya chanzo ya kujinga na maradhi mbalimbali, iliyotolewa kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano.
Mwaruanda alisema chanzo cha ajali hiyo ni upepo uliombatana na mawimbi makali, ulisababisha mtumbwi huo kupinduka.
Alisema miili ya marehemu hao iliopolewa na wananchi wa Kijiji cha Kasanga, lakini majina yao hayajafahamika.
Alisema kazi ya kutambua maiti inaendelea.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo, walisema mtumbwi huo ulianza kupoteza uelekeo baada ya mawimbi kuwa makali yakiambatana na upepo.
Walisema baada ya kupinduka na kusababisha vifo hivyo, upo uwezekano wa idadi ya watu waliokufa kuongezeka kutokana na kudaiwa kuwa ulikuwa umebeba idadi kubwa ya watu.
Kumekuwa na matukio ya vifo Ziwa Tanganyika kutokana na mawimbi makali.

SOURCE: MWANANCHI