Msanii
maarufu wa muziki nchini Uganda, Joseph Mayanja, maarufu kama, Jose
Chameleon, hivi karibuni alitwaa tuzo ya msanii bora wa kiume wa
kimataifa nchini humo. Chameleon ametwaa tuzo hiyo baada ya kuibuka
mshindi katika kinyang’anyiro cha Msanii Bora wa Kiume wa mwaka katika
tuzo za Africa Entertainment Awards, zilizofanyika jijini Kampala, hivi
karibuni.
Ushindi wa tuzo hiyo unazidi kumpa nafasi mwanamuziki huyo kuendelea
kung’ara katika tasnia ya muziki ndani na nje ya Uganda, na hata katika
ukanda wa nchi za Afrika.
Baada
ya kupokea tuzo hiyo, Chameleon aliwashukuru mashabiki wake akisema
kuwa bila wao yeye asingeweza kutwaa tuzo hiyo, ambayo alisema kuwa
kwake anaiona kama kitu muhimu zaidi kinachodhihirisha maendeleo yake
kimuziki.
Lengo la tuzo za African Entertainment Awards ni kuonesha thamani ya muziki na urithi wa utamaduni kwa wanamuziki wa Afrika.
Kadhalika,
lengo la tuzo hizo ni kuwatia moyo wasanii ambao wametumia sanaa na
utamaduni wa Mwafrika katika kuonesha utaalamu wao kubuni mitindo
mbalimbali katika taaluma ya burudani.
Mbali
ya utoaji wa tuzo, tamasha hilo lilitawaliwa na burudani kutoka kwa
wasanii mbalimbali wa nchini Uganda. Mwaka 2002 Chameleon alipata
mwaliko wa kutumbuiza katika michuano ya Olimpiki katika Jiji la London,
Uingereza.
Kadhalika,
msanii huyo amekuwa katika maelewano mazuri na kampuni ya AS
Entertainment ya Afrika Kusini, ambayo pia ilimpa mchongo wa kufanya
maonesho wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika
Kusini.
Hivi
karibuni, ametoa wimbo mpya wenye jina la Badilisha ambao tayari
umekubalika katika soko la Afrika Mashariki. Kutokana na umahiri wake
katika kushambulia jukwaa, wapenzi wake wamembatiza jina kwa kumuita
Dokta wa Muziki.
SOURCE: JAMUHURI MEDIA
|