Na Frederick Katulanda, Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba23 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba23 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Mwanza. Muumini mmoja wa Kanisa la Gilgal
Christian ameuawa na wengine wawili wamejeruhiwa vibaya kwa kukatwa na
mapanga sehemu mbalimbali mwilini baada ya watu wasiofahamika kuvamia
kanisa hilo usiku wa manane kwa lengo na nia isiyojulikana.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 22 mwaka huu saa 7
usiku, eneo la Pasiansi wilayani Ilemela mkoani Mwanza. Aliyeuawa katika
tukio hilo lililowasikitisha wengi, ametajwa kuwa ni Elias Meshack.
Aidha, upande wa waliojeruhiwa wametajwa kuwa ni
Elias Msakuzi ambaye alitibiwa na kurejea nyumbani baada ya kujeruhiwa
kichwani pamoja na Tumsifu Pungu ambaye bado amelazwa Hospitali ya Rufaa
ya Bugando akiendelea kupata matibabu na hali yake imeelezwa kuendelea
vizuri.
Kwa mujibu wa Askofu Eliabu Sentozi, alisema kwa
mwonekano na sura ya tukio hilo, halionyeshi kuwa na nia ya ujambazi
kutokana na wavamizi hao kutokuiba chochote ndani ya kanisa hilo na
hivyo kuitaka Serikali kuangalia kwa makini mfululizo wa matukio haya
yanayotokea kanisani.
“Sidhani kama hili ni tukio la ujambazi, maana
malengo ya jambazi huwa ni kusaka fedha ama vitu sasa hapa hakuna
kilichoibwa,” alisema.
Alisema kinachowafanya kuamini kwamba wahusika
hawakuwa na nia ya wizi ni kutokana na kutochukua kitu chocote ingawa
ndani ya kanisa kulikuwa na vitu vingi vyenye thamani.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ernest Mangu
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwa sasa jeshi lake
limeanza uchunguzi wa tukio hilo.
“Nitatoa ufafanuzi baadaye, kwa sasa tupeni nafasi
ya kuchunguza hili jambo. Hatuwezi kujua nia hasa ilikuwa nini, lakini
baada ya uchunguzi taarifa zitatolewa,” alieleza kamanda huyo wa polisi.
Mpaka sasa bado hakuna mtu yeyote aliyetiwa nguvuni.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI