KUNDI
la waasi wa M23, linalopambana na Jeshi la Serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limetajwa kuwa chanzo cha kuisambaratisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kauli hiyo imetolewa juzi na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, katika
mahojiano yake na kituo cha redio cha Clouds.
Membe amesema
kinachosababisha Tanzania itengwe na baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya
ya EAC, ni hatua yake ya kupeleka majeshi katika mji wa Goma ulio
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa ajili ya
kupambana na waasi wanaoipinga Serikali ya Rais Joseph Kabila.
Amesema
hatua hiyo ya Tanzania ilizikera baadhi ya nchi wanachama wa EAC, zenye
maslahi ya moja kwa moja na kundi hilo na kusisitiza kuwa hata kama
itatengwa, kamwe haitaondoa vikosi vyake DRC na badala yake vitaendelea
kupambana.
“Najua sababu za wenzetu kuharakisha shirikisho la
kisiasa na kuamua kufanya vikao vya siri vya kuitenga Tanzania, ni
uamuzi wetu wa kupeleka vikosi vya kijeshi Congo, wanalalamika kwamba ni
kwanini tumefanya hivyo na kudai kuwa maamuzi yetu hayo yatauvunja
umoja wetu, sisi tukawaambia hatuwezi kuacha kuleta amani Kongo, hiyo
ndiyo sababu,” alisema Membe.
Aliitaja sababu nyingine
inayotishia uhai wa jumuiya hiyo kuwa ni uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete
kukataa suala la ardhi kuingizwa katika mambo ya pamoja ya jumuiya.
“Sisi
ni nchi kubwa, tuna kila kitu, tuna ardhi kubwa, hatuendeshi nchi yetu
kwa muungano wa makabila, wenzetu wanatuonea wivu, wanaitaka ardhi yetu,
Mzee Kikwete amekataa, wanaamua kututenga, niwahakikishie Watanzania,
hatuna hofu hata chembe na suala hili.
“Hawa jamaa pia wanakerwa
na hatua yetu ya kuwepo kwenye Jumuiya ya SADC, wanaona kama tunafaidi
sana, lakini niwaambie kwamba hatuwezi kutoka SADC, mbona wao wako
COMESA,” aliongeza Membe.
Aidha Membe aligusia ujio wa viongozi
wa Kimataifa nchini Tanzania kuwa moja ya sababu za nchi wanachama wa
EAC kuitenga Tanzania, kwa madai kuwa inafanya mambo yake yenyewe.
Kwa
miezi kadhaa kumekuwa na jitihada zinazofanywa na marais wa Rwanda,
Kenya na Uganda za kutaka kuunda shirikisho la kisiasa la Afrika
Mashariki pasipo kuishirikisha Tanzania.
Tayari marais hao
wamekwishaanzisha mipango ya pamoja ya kiuchumi na kuimarisha
miundombinu ya reli na bandari, ambapo mwezi Agosti mwaka huu walikutana
mjini Mombasa kwa ajili ya uzinduzi wa gati namba 19 la kuingiza na
kutoa mizigo katika Bandari ya Mombasa.
Taarifa nyingine za hivi
karibuni kutoka nchini Rwanda zimeeleza kuwa nchi hizo tatu
zimekwishaunda kikosi kazi kilichopewa jukumu la kuandaa rasimu ya
Katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki.
SOURCE: Mtanzania