Kwa ufupi
Namshauri Rais (Jakaya Kikwete), kuhakikisha
kwamba haki za wanyonge zinawafikia, asije akafikiri hili lililotokea
kwa Sheikh Ponda ni suluhisho, ni vyema kufanya mazungumzo ili kuweka
mabadiliko.
Dar es Salaam. Katibu wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema
alichanganyikiwa kiasi cha kushindwa kujielewa kwa muda baada ya
kupigwa risasi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi
kwenye wodi binafsi ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi)
alikolazwa jana, Sheikh Ponda alisema kutokana na hali hiyo hakumbuki
matukio yaliyofuata baada ya hapo.
“Sikumbuki hata nilipata huduma ya kwanza
hospitali gani kwa sababu sikuwa katika hali ya kawaida. Mambo mengine
yaliyotendeka kabla ya kujeruhiwa ninayakumbuka vizuri,” alisema Ponda
ambaye inasadikiwa kwamba alipigwa risasi ya begani, Ijumaa iliyopita
mjini Morogoro.
Alisema alihutubia katika Kongamano la Waislamu
kwa muda mfupi akizingatia muda uliokuwa umetolewa kumaliza mkutano huo
na baada ya hapo alishuka na kupanda kwenye gari binafsi ambalo
lilizingirwa na polisi ndipo akaamua kushuka na kuanza kutembea kabla ya
kujeruhiwa.
Mahojiano maalumu na Sheikh Ponda
Swali: Je, watu waliokupa huduma ya kwanza mara baada ya kujeruhiwa walikuta risasi iliyokujeruhi?
Jibu: Nilipigwa risasi kwa nyuma ikatokea mbele
kwa hiyo haikubaki mwilini wala haikuonekana ilipoangukia kwa wakati huo
maana kulikuwa na purukushani.
Swali: Ulipata wapi huduma ya kwanza?
Jibu: Kwa kweli kwa sasa siwezi kukumbuka
nilihudumiwa wapi kwa sababu mara baada ya kujeruhiwa sikuwa katika hali
yangu ya kawaida, nilichanganyikiwa.
Swali: Utathibitisha vipi kama ulipigwa risasi?
Jibu: Bahati nzuri ni kwamba tukio hili lilitokea
kweupe wapo wengi walioshuhudia, kwa hiyo wanaweza kusaidia kuthibitisha
na ushahidi mwingine ni jeraha hili.
Swali: Nini msimamo wako baada ya tukio?
Jibu: Nitaendelea kuzungumzia haki za Waislamu na siwezi kurudi
nyuma. Pamoja na kwamba wananiona mimi ni mtu mchochezi lakini wanaeneza
chuki dhidi yangu kwa njia wanazojua wao. Nitaendelea, risasi
haitaninyamazisha.
Swali: Umehusishwa kufanya uchochezi Zanzibar, unalizungumzia vipi hilo?
Jibu: Zanzibar nilichozungumza ni kuhusu kesi
dhidi ya viongozi wa Kundi la Uamsho. Watu wamewekwa ndani kwa miezi
tisa sasa, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, kesi wanayoshtakiwa ina
dhamana, sasa nikauliza kwa hao viongozi, kwa nini hawazingatii sheria?
Kesi zina muda mrefu hazitolewi uamuzi, nikawasisitiza wazingatie
misingi ya sheria kwa kuwa hivyo wanavyowatendea wananchi wajue kwamba
hawastahili kupewa tena ridhaa ya kuongoza nchi, nilifikisha ujumbe
wangu.
Swali: Kuna tukio la kumwagiwa tindikali mabinti
wawili wa Uingereza lililotokea Zanzibar, ambalo wewe pia unahusishwa,
hili unalizungumziaje?
Jibu: Sijaona huo ushahidi ambao wanahangaika
kunihusisha na tukio hilo, nahusishwa vipi? Matukio ya kumwagiwa
tindikali yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara huko kabla sijakwenda
kuhutubia. Vyombo vya dola vifanye kazi yake vyema ili kubaini ukweli wa
jambo hili.
Pia Mwananchi ilizungumza na mke wake, Sheikh Ponda, Hadija Ahmad ambaye alikuwa ameketi pembeni ya kitanda alicholazwa mumewe.
Swali: Unazungumziaje tukio hili la kujeruhiwa kwa mumeo?
Jibu: Hili ni dhumuni la Serikali, lililenga moja
kwa moja kumdhuru ili kunyamazisha harakati zake za kutetea wanyonge. Ni
tukio la kupangwa, halijatokea bahati mbaya. Serikali inamfuatilia sana
hivyo ililenga kumnyamazisha.
Namshauri Rais (Jakaya Kikwete), kuhakikisha
kwamba haki za wanyonge zinawafikia, asije akafikiri hili lililotokea
kwa Sheikh Ponda ni suluhisho, ni vyema kufanya mazungumzo ili kuweka
mabadiliko.
Alivyowaponyoka polisi
Mtu wa karibu wa Sheikh Ponda alisimulia jinsi
walivyomsafisha kiongozi huyo kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam na
kukwepa vizuizi vya polisi ambao walikuwa wakiendelea kumsaka.
“Msafara ulikuwa na magari mawili. Moja lilitumika kwa
uangalizi, lingine lilimbeba Sheikh Ponda. Tulipofika Chalinze tulikuta
kizuizi tukakikwepa kwa kupitia Msata kisha Bagamoyo hadi Dar es Salaam
na kumfikisha Muhimbili,” alisema.
Waigomea polisi
Msemaji wa familia ya Sheikh huyo, Isihaka Rashid
alisema hawaitambui tume iliyoundwa na polisi kwa kuwa jeshi hilo ndilo
linalotuhumiwa.
“Tunachofanya hivi sasa ni kukusanya ushahidi
wetu, kwa bahati nzuri tayari tumepata mkanda wa tukio lenyewe ambao
utatuwezesha kumbaini aliyemshambulia Sheikh Ponda.
“Hatuwezi kuhitaji majibu ya hiyo tume yao na hata
leo kuna maofisa wa polisi kutoka Makao Makuu na Kituo cha Kati, Dar es
Salaam walifika wakitaka kumhoji eti kuhusu uchochezi lakini alikataa
kuzungumza hadi mwanasheria wake awepo, wakaondoka,” alisema Rashid.
chanzo: Mwanachi
chanzo: Mwanachi