Posted Jumatano,Septemba11 2013 saa 12:1 PM
Kwa ufupi
Badala yake, Ndugai akatumia jazba, akimtaka
Mbowe akae chini na alipokaidi, akaita polisi waje kumtoa nje, hapo
ndipo vurugu zikaanza.
Mambo yaliyotokea bungeni mjini Dodoma wiki moja
iliyopita hayawezi kupita bila kujadiliwa. Mengi yamezungumzwa ikiwamo
chanzo cha vurugu kiasi cha baadhi ya wabunge kuburutwa kama vibaka
ndani ya ukumbi huo.
Kwangu mimi naona kuna ukosefu wa busara kwa
viongozi wetu kiasi cha kuwa sababu ya vurugu za mara kwa mara ndani ya
ukumbi huo. Ninamzungumzia na hata kutofautiana na Naibu Spika, Job
Ndugai ambaye mara nyingi hapendi kusumbuka pale utata unapojitokeza
katika vikao, bali huishia kuita polisi. Siku ya tukio hilo, baada ya
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuomba nafasi ya
kuzungumza baada ya kura kupigwa na wabunge wa CCM kushinda, ilitakiwa
busara kidogo ili kuepusha zahma ile.
Badala yake, Ndugai akatumia jazba, akimtaka Mbowe
akae chini na alipokaidi, akaita polisi waje kumtoa nje, hapo ndipo
vurugu zikaanza.
Hivi ingekuwaje kama Mbowe angeachwa azungumze, kisha Ndugai akamjibu kulingana na hoja yake?
Mbowe naye kama mwanasiasa angekaa chini,
kuheshimu kanuni, asingeweza kulalamika kwa kutumia kanuni hizo
zilizopo, angekosa nini na kwa nini hakufanya hivyo? Najiuliza, Ndugai
angeweza kuahirisha hoja hiyo aijibu katika kikao kingine. Hapo
zisingetokea vurugu zozote. Ingekuwaje kama mbunge wa CCM kama vile,
Waziri William Lukuvi ambaye pia ni Mnadhimu wa chama hicho, naye
angeitiwa polisi? Au, angekuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesimama
anahitaji ufafanuzi fulani angekaripiwa vile?
Sikatai kwamba kazi ya polisi ni kulinda amani na
utawala wa sheria, lakini haimaanishi kwamba mwenye mamlaka wakati
wowote ni kutumia nguvu tu. Busara ya hali ya juu inahitajika kuendesha
Bunge letu.
Nasema hivyo kwa sababu Spika wa Bunge letu na
naibu wake ni makada wa CCM tena wanahudhuria vikao vya juu vya chama,
kwa hiyo uwezekano wa kufanya upendeleo ni mkubwa. Kwa hiyo,
linapotokea suala lenye masilahi ya CCM, wanaweka kando masilahi ya
wananchi, wanatetea chama kwanza. Ndicho alichokifanya Ndugai, japo yeye
ni mhimili wa Bunge anatumia nguvu nyingi kuitetea Serikali ambayo ni
mhimili mwingine.
Hata hivyo, kama askari nao wangekuwa na busara
wasingeingia kichwa kichwa, kufanya walichofanya, bila shaka tusingeona
aibu kama hiyo. Busara ya kuendesha vikao kwa kutoa nafasi sawa kwa
wabunge na wakati mwingine kuziba mianya ya vurugu bila hata kuita
polisi.
Labda kama mapendekezo ya Rasimu ya sasa ya Katiba
Mpya yatakubalika ambayo yanataka spika wa Bunge asiwe mwanachama wa
chama chochote cha siasa. Kwa hali ilivyo sasa, inamlazimu mno kiongozi
wa Bunge kutumia busara za hali ya juu kuendesha vikao.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI