Na Peter Saramba, Mwananchi
Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 11:21 AM
Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 11:21 AM
Kwa ufupi
- Kampuni kubwa za kibiashara zinatumia udhaifu wa taasisi za serikali kukwepa kulipa ushuru sahihi.
- Miongoni mwa nchi zinazotumia udhaifu wa taasisi za serikali ni; Visiwa vya Cayman, Switzerland, Luxembourg, Bermuda na Visiwa vya Jersey.
- Mjumbe
wa kamati ya PAC wa Uganda, Ssewungu Gonzaga anasema tabia ya wabunge
wengi kuweka mbele itikadi za vyama vyao badala ya umma ni kikwazo cha
maendeleo.
Kushusha thamani bidhaa na malighafi za
Bara la Afrika ukilinganisha na bei halisi ya soko ni mbinu inayotumika
zaidi kuiba theluthi mbili ya fedha na rasilimali zinazotoroshwa na
wageni.
Mkutano wa 10 wa wabunge wajumbe wa kamati za
hesabu za serikali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa
Afrika, (Sadc), umekwisha jijini Arusha huku washiriki wakibainisha
sababu kadhaa zinazokwamisha vita dhidi ya wizi, ufisadi na uporaji wa
rasilimali za umma kutoka nchi zinazoendelea, likiwamo Bara la Afrika.
Pamoja na sababu kadhaa, nchi zilizoendelea katika
Bara la Ulaya na Marekani pia zinadaiwa kuchochea wizi wa fedha na
rasilimali za umma kwa kukubali kuzihifadhi baada ya kuibwa kwenye
mataifa maskini barani Afrika.
Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)
kutoka nchini Sudan Kusini, Goc Mukleac Mayol, amewatuhumu wahisani
kwamba ni walimu wa wizi na uporaji wa fedha na rasilimali katika nchi
za Afrika.
“Kama kweli hawa wenzetu (Ulaya na Marekani),
wanaotufundisha kuthibiti fedha na rasilimali zetu wana nia njema na
Afrika, basi kwanza wakatae kupokea fedha zetu zinazoibwa na kuhifadhiwa
kwenye mabenki zao na wawataje ili wajulikane kwa umma badala ya
kuwakumbatia,” anasema Mayol.
Mayol anasema tabia ya wizi na ufisadi siyo sehemu
ya utamaduni wa Mwafrika bali ni mafundisho kutoka kwa baadhi ya
watawala wa kikoloni wanaoendelea kutumia uwezo wa kiuchumi wa nchi zao
kupora fedha na rasilimali za Bara la Afrika.
“Hadithi zetu za kale zinatufundisha kuwa kijana mdogo hawezi kuwa mwizi bila kufundishwa na kaka yake mkubwa.
Tunapozungumzia wizi na ufisadi wa fedha na
rasilimali za umma barani Afrika, lazima tukubaliane kuwa ni mafundisho
kutoka kwa kaka zetu (Ulaya na Marekani), ambao huwalinda wanaotuibia na
kuhifadhi fedha zetu kwenye benki zao,” anabainisha Mayol.
Anataja baadhi ya miji mikuu ambako fedha na
rasilimali zinazoibwa Afrika zimefidhiwa kuwa London, Switzerland na
miji mingine mikubwa ya Ulaya na Marekani.
“Wezi wa fedha za Afrika wanalindwa na serikali za
nchi hizo ambazo kila siku zinatuimbia nyimbo na ngonjera za kudhibiti
wizi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma,” anasema.
Mwenyekiti wa PAC Tanzania, Zitto Kabwe anasema
tatizo la wizi na utoroshaji wa fedha na rasilimali za umma kutoka nchi
zinazoendelea kwenda nchi zilizoendelea ni janga kubwa linalohitaji
kushughulikiwa kikamilifu.
Zitto anasema kati ya mwaka 2000-210 zaidi ya dola
844 bilioni za Kimarekani zilitoroshwa kutoka nchi zinazoendelea kwenda
nchi za Ulaya na Marekani. Asilimia 69 ya fedha hizo, sawa na dola 582
bilioni za Marekani zimetoroshwa kutoka barani Afrika, ndani ya kipindi
hicho.
Kwa mujibu wa Zitto, miongoni mwa mbinu
zinazotumika kutorosha fedha na rasilimali za nchi za Afrika, ikiwamo
Tanzania ni wizi, rushwa, bakshishi kupitia mikataba (Ten Percent),
ukwepaji kodi na kushusha thamani za bidhaa au maligafi kutoka Bara la
Afrika.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI