15th September 2013
Dawa
za kuchochea uchungu kwa wajazito zikiwamo ‘misoprostol’ , ‘oxytocin’ ,
`Mifecon-Mkit’ kupatikana kiholela kwenye maduka ya dawa kumechochea
utoaji mimba kufanyika bila hofu wala kipingamizi.
Utoaji mimba wa kutumia dawa hizo na njia
nyingine za kienyeji unafanyika kwenye mazingira duni, kwa kutumia
vifaa vichafu wanavyotumia wauguzi ‘vishoka’ .
Hali hiyo inasababisha mabinti na wanawake
kuambukizwa maradhi ya mfumo wa uzazi mfano (PID), Ukimwi na VVU na
wengine kuharibu mfuko wa uzazi na kusababisha ugumba.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili, uligundua
kuwa vidonge hivyo hupatikana kwa urahisi kwenye maduka ya dawa muhimu
na hivyo wanawake huzipata kwa urahisi wanapotaka kuharibu mimba.
Baadhi ya wateja wanaeleza kuwa wahudumu kwenye maduka hayo wanawaelekeza na kuwapa ushauri wajawazito wanaotaka kutoa mimba.
Walisema dawa hizo hupatikana kwa bei
kubwa mfano Mifecon-Mkit huuzwa kwa Sh. 30,000 hadi 50,000 wakati
‘misoprostol’ inapatikana kuanzia Sh. 10,000 na zaidi kutegemeana na
mahali zinapopatikana na soko lilivyo wakati huo.
Wauza dawa hizo hupandisha bei ili
kuwahadaa wajawazito hao kwa ajili ya kupata faida zaidi licha ya kwamba
maeneo mengine dawa hizo zinaweza kupatikana kwa bei ya chini.
DAWA ZINAZOTUMIWA
Misoprost -200 maarufu kama ‘miso’ ni
vidonge vinavyotumiwa vibaya sehemu nyingi jijini Dar es Salaam kwa
kutoa mimba kwa maelekezo yanayotolewa na wahudumu wa maduka ya dawa,
wahudumu wa afya wasio na maadili na madaktari ‘vishoka’ mitaani.
Wanadaiwa kuwaelekeza wateja kuweka
vidonge chini ya ulimi ili viyeyuke na vingine huingizwa sehemu za siri
karibu na shingo ya uzazi.
Aidha dawa hiyo ya aina moja hutolewa
maelekezo tofauti huku wengine wakitoa dozi kubwa zaidi, alisema
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ualimu cha Dar es Salaam (DUCE).
Vidonge hivyo hupanua shingo ya kizazi na
kusababisha hewa kupita kwenye nyumba ya uzazi na kubomoa ukuta wa tumbo
la uzazi na kuharibu mimba.
Kwa upande wa ‘mkit’ ambalo katika
mahojiano na baadhi ya mabinti wanaofanyabiashara ya ngono Buguruni,
jijini Dar es Salaam, walisifia kwa kuipa jina la ‘kubwa la maadui’
walidai inatoa mimba yenye umri wowote hata pale ‘miso’ inaposhindwa .
Baadhi ya wauzaji waliitaja kuwa ni bingwa na wanawapatia wateja wao hasa wenye mashaka na dawa nyingine.
‘Mkit’ kwa mujibu wa wataalamu inatumiwa
kuharakisha uchungu kama ilivyo kwa ‘miso’ lakini inatumiwa vibaya pale
inapomezwa ili kuharibu mimba.
Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya
juu walikiri kuwa dawa hii inawasaidia lakini wengine walisema si wakati
wote kwani wapo waliodai waliitumia lakini badala ya kuharibu ilikuza
mimba.
Tembe nyingine zinazotumiwa ni ‘arzithromycin-500’ ambazo huingizwa sehemu za siri na nyingine humezwa.
Mmoja wa madaktari ambaye hakupenda jina
lake liandikwe gazetini alisema kuwa dawa hii si ya kuharibu mimba bali
inatumika kutiba maradhi mbalimbali kama kifua, magonjwa ya ngono na
kukausha vidonda vilivyotokana na kushambuliwa na vimelea .
Kwa upande wa ‘oxytocin’ watumiaji hununua na kuchomwa sindano kisha kurudi nyumbani kusubiria mimba kuharibika.
UTOAJI MIMBA KIENYEJI
Baadhi ya mabinti hutolewa mimba kwa
kutumia kijiti cha jani la mhogo na miti ya mbaazi, vyuma vya baiskeli
(spoku) , sindano, majani ya aloivera, mwarubaini, kunywa chai ya rangi
yenye majani mengi, kemikali zikiwamo shabu inayotumiwa kusafishia maji
na hata kuingiziwa dawa za kienyeji sehemu za siri.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi
inayojishughulisha na kukuza, kuendeleza haki na maendeleo kwa watoto,
vijana na wanawake (Kiwohede), Yusta Mwaituka, ambaye pia ni muuguzi na
mkunga anasema utoaji mimba kienyeji umeshamiri sehemu nyingi.
Anaeleza kuwa utoaji mimba unafanywa
kienyeji kwa kutumia spoku, miti ya kisamvu ama vijiti vya mbaazi
ambavyo mabinti na wanawake huvipitisha sehemu za siri na kutoboa mfuko
wa uzazi na wakati mwingine sindano zenye dawa au maji dawa hutumika.
Mwaituka anasema tatizo la utoaji mimba
kienyeji hukuzwa na uwapo wa wataalamu `feki' mitaani ambao
wanafahamika na jamii lakini hawachukuliwi hatua na wameendelea
kuneemeka.
Mwaituka anaeleza kuwa wakati mwingine
wazazi wanachangia kusababisha mabinti kupata na kuharibu mimba kutokana
na kuwaelekeza kushiriki ngono.
“Mzazi anamwambia binti yake umekuwa
mkubwa baba yake hawezi kununua losheni na nguo za ndani tafuta
mfadhili. Malezi hayo husababisha wasichana kufanya ngono mapema, kupata
ujauzito na kutolewa mimba kienyeji mitaani.”
MAENEO MAARUFU
Zipo sehemu mbalimbali zinazojihusisha na
utoaji mimba zikiwamo hospitali za umma, binafsi na zahanati bubu
zinazojulikana kwa kazi hiyo.
Jijini Dar es Salaam baadhi ya madaktari
wa hospitali za umma na binafsi wanatajwa kufanya kazi hiyo, wakati
wanafunzi wa vyuo vikuu vya tiba nao wanatuhumiwa.
Zipo zahanati maarufu kwa ajili ya utoaji
mimba na zinazojulikana baadhi zipo karibu na mabweni ya wanafunzi wa
taasisi za elimu ya juu. Baadhi ya wakazi wa meneo ya Kinondoni
Mkwajuni, Yombo Kilakala, Dovya , Tandika na sehemu za Tabata walieleza
kuwapo uhalifu huo.
MAELEZO YA MSD
Ili kujua sababu za dawa zinazochangia
utoaji mimba kuuzwa madukani gazeti hili liliwasiliana na Bohari ya Dawa
(msd) kupata ufafanuzi na kufahamishwa kuwa dawa kama ‘misoprostol’
zinaagizwa na kuuzwa nchini kisheria.
Kwa mujibu wa Meneja Manunuzi wa Msd,
Nichodemus Frederick, dawa hizo hutumika kuzuia kutokwa damu nyingi
baada ya kujifungua ama kuchochea uchungu mjamzito anapokawia
kujifungua.
Frederick ambaye kitaaluma ni daktari, alisema dawa hizo hutolewa kwa kipimo maalumu na kwa maelekezo ya wataalamu.
Kuhusu ‘ oxytocin’ ambayo hujulikana kama
maji ya uchungu kwa mujibu wa Frederick, inatumiwa kama sindano ili
kuongeza kasi ya uchungu kwa mjamzito.
Katika muongozo wa tiba wa taifa
unaotolewa na Wizara ya Afya, dawa hiyo ni ya sindano na kwamba hutolewa
kupitia dripu ambayo mjamzito hulishwa .
“Dawa hizo kuuzwa kwenye maduka ni
utaratibu unaokubalika kisheria kwa kuwa lengo lake ni kuwasaidia
wanaozihitaji kwa mujibu wa malekezo ya wataalamu na siyo kutoa mimba,”
alisema Frederick.
Aliongeza kuwa kuzitumia kuharibu mimba ni
matumizi mabaya na kusisitiza kuwa vidonge hivyo vinaagizwa na msd kwa
ajili ya kufungashwa kwenye fungashio la mama mjamzito kwa ajili ya
kuzuia kutokwa damu nyingi baada au kubla ya kujifungua au kumuongeza
uchungu.
MADHARA
Frederick anataja athari za utoaji mimba
kwa kutumia dawa hizi kuwa ni pamoja kuharibu taratibu za kimaumbile
kwenye kizazi na kusababisha ugumba.
Zikitumiwa vibaya husababisha kutoka damu nyingi na kupoteza maisha kutokana na kukosea maelekezo ya wataalamu.
Anataja madhara ya kisaikolojia na kusononeka kutokana na moyo kujuta kutokana na kutoa mimba.
Mwaituka anataja tatizo la kupata magonjwa sugu ya via vya uzazi yanayoathiri shingo ya kizazi na mirija ya mayai.
Wanaotumia arzithromycin-500 wanaweza
kujisababishia vidonda sehemu za siri na kwamba ni makosa kuzitumbukiza
sehemu hizo pia kuna uwezekano wa kupata saratani maeneo ya uzazi kwa
vile tembe hizi ni za kunywa.
SHERIA
Utoaji mimba ni kosa kisheria kwa
Tanzania kwa mujibu wa sura ya 16 kifungu cha 150 – 152 cha kanuni za
adhabu watuhumiwa watatu wanaweza kufungwa kutokana na kosa la utoaji
mimba ambao ni mjamzito, daktari anayemtoa na anayetoa vifaa au
kugharamia kazi hiyo.
Anayetoa mimba anaweza kufungwa miaka 14
au hata maisha , anayeomba kutolewa mimba anaweza kufungwa miaka saba na
anayetoa vifaa au dawa kugharamia utoaji huo anafungwa miaka mitatu.
Kwa ujumla kutaka kutolewa mimba,
kushiriki kuitoa na kugharamia ni kosa la jinai ni halali tu iwapo
mimba inatolewa kwa idhini ya madaktari ili kuokoa maisha ya mama au
kumkinga na madhara ya kiafya .
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI