15th September 2013
Baada ya kufanikiwa kuwadhibiti wasafirishaji dawa
za kulevya katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JK Nyerere jijini Dar
es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema sasa
atakabiliana na waajiriwa haramu katika uwanja huo.
Akizungumza jana na wafanyakazi wa Wakala
wa Ndege za Serikali, Dk. Mwakyembe alisema baada ya kupata malalamiko
ya kuwepo na wafanyakazi ambao ni wahamiaji haramu na kuajiriwa katika
ofisi mbalimbali uwanjani hapo, anatarajiwa kufanya msako wa kushitukiza
ili kuwabaini.
“Nawashukuru sana kwa kunipa taarifa ya
kuwepo wafanyakazi haramu, lakini naomba Jumatatu nipate taarifa kamili
ili niweze kufanya msako wa kushitukiza kuwanasa…hawa ndio
wanaosababisha kuwepo na wahamiaji haramu wengi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Dk. Mwakyembe alisema hayo wakati
akizungumza na wafanyakazi hao alipokuwa akimtambulisha Katibu Mkuu mpya
wa wizara hiyo, Dk. Shaban Mjaka.
Awali akizungumza mbele ya waziri, mmoja
wa wafanyakazi wa wakala wa ndege hizo za serikali, alisema pamoja na
juhudi za Mwakyembe kudhibiti usafirishaji dawa za kulevya uwanjani
hapo, lakini bado tatizo la uingizaji wahamiaji haramu unafanyika kwa
kasi kubwa.
“Wapo watu wengi wanaingia hapa nchini
kupitia uwanja huu pasipo kufuata taratibu za nchi kutokana na baadhi ya
wafanyakazi walioajiriwa katika nafasi nyeti nao kutokuwa na sifa za
kuishi nchini kihalali,” alisema mmoja wafanyakazi hao.
Kufuatia madai hayo ya wafanyakazi ambayo
yalionekana kumshtua Dk. Mwakyembe, alisema kuanzia wiki ijayo baada ya
kupata taarifa kamili atafanya msako wa kuwanasa watu hao ambao
wanachangia bila aibu kuingiza watu wengine bila kufuata taratibu za
nchi.
Awali akiwa katika Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) kuzungumza na wafanyakazi wa mamlaka hiyo kwa lengo la
kumtambulisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo na kupata majibu ya maagizo
yake aliyoyatoa Desemba 21, mwaka jana katika madai 17 ya wafanyakazi.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI