Wednesday, 25 September 2013

Hali tete Nairobi: Kenyatta asema askari sita waliangukiwa na ukuta na upoteza maisha

Askari wa Kenya wakiwa juu ya jengo la Westgate jana kuwasaka magaidi walioteka watu tangu Jumamosi. Picha ya AFP  

Ghorofa kuanguka
Pia Rais Kenyatta alitangaza kuwa maofisa sita wa usalama walifariki dunia jana jioni baada ya kuangukiwa na ukuta baada ya kudondoka kwa ghorofa tatu za jengo ambalo magaidi wamejichimbia.

Alisema watu hao walifukiwa na ukuta wakati vikosi vya usalama vikiendelea na operesheni ya kuwasambaratisha magaidi hao.
Rais Kenyatta alieleza kuwa haijajulikana mara moja chanzo cha kuanguka kwa ukuta huo na kwamba wanachunguza jambo hilo.
Hali hiyo inafanya idadi ya watu waliokufa kufikia 67. Kati yao, 61 wakiwa ni watu wa kawaida na sita ni maofisa wa usalama, huku 175 wakiwa wamejeruhiwa.
Siku tatu za maombolezo
Rais Kenyatta alitangaza siku tatu kwa ajili ya maombolezo kutokana na shambulizi hilo la magaidi.
Alisema bendera za Kenya zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo ili kuwakumbuka watu waliopoteza maisha katika tukio hilo.
“Maombolezo haya ni kwa ajili ya kuwakumbuka wenzetu waliopoteza maisha kutokana na kitendo hiki cha kikatili cha watu waoga,” alisema Rais Kenyatta.
Amshukuru Rais Kikwete
Pamoja na kuwashukuru wananchi wa Kenya, pia Rais Kenyatta alimshukuru Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine wa Afrika Mashariki kwa kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.
“Ninaomba kuwashukuru Marais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Paul Kagame wa Rwanda, Salva Kiir wa Sudan Kusini na Pierre Nkuruzinza wa Burundi kwa kutuunga mkono katika kipindi hiki kigumu,” alisema Rais Kenyatta na kuongeza:
“Viongozi hawa wamekuwa wakiwasiliana nami kila wakati kujua tunavyoendelea na operesheni.”
Pia Rais Kenyatta aliwashukuru wananchi wa Kenya kwa kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki na kujitolea kwao kwa hali na mali.

SOURCE: MWANANCHI