16 Septemba, 2013 - Saa 11:32 GMT
Mji wa Ujiji ulioko Magharibi
mwa Tanzania una historia ndefu miongoni mwa miji ya kale ya Afrika
Mashariki na Kati ukihusishwa na biashara ya watumwa kutoka Burundi,
Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Ni katika eneo hilo la Ujiji ndiko mvumbuzi wa
kimataifa, Dr David Livingstone, alipofikia akiwa katika safari zake
zilizomtoa pwani ya Afrika mashariki hadi Kongo. Kwa sasa kuna
makumbusho maalum kwa heshima yake na kumbu kumbu ya vizazi vijavyo.Kwenye kituo cha makumbusho ya Dr David Livingstone katika eneo la Mnazi Mmoja-Kabondo Ujiji ni eneo ambalo kuna majengo mazuri yenye vyumba kadhaa vilivyobeba alama za ujio wa Mvumbuzi huyo aliyechangia kukomeshwa kwa biashara ya utumwa, lakini pia kumbukumbu za asili za vitu na watu wa mji huo.
Kufifia kwa umaarufu wa eneo kongwe la Ujiji kulichangiwa na sababu nyingi, ikiwemo kuanzishwa kwa mji mpya wa Kigoma. Kurejea kwa Ndiyunze Msherwampamba aliyekuwa kiongozi wa watu wa kabila la wagoma kutoka Kongo kuliibua jina la mji mpya Kigoma.
Alhaj Mikdad bin Ibrahim Tawfiq Malilo mwenye miaka 79 mkaazi maarufu wa Ujiji, ameiambia BBC kuwa Msherwampamba alipokelewa pamoja na wafuasi wa kabila lake na wakapewa eneo la kujitawala ambalo wakati huo lilikuwa likiitwa Rusambo , na sasa ndilo linaloitwa Kigoma.
Sasa wenyeji warundi ndiyo wanajiita wajiji wakawa wanakwenda kuwatembelea wanasema 'tugende kubagoma,' likaendelea likabadilika ndiyo ikawa Kigoma basi ndiyo kitovu cha mahala kuitwa Kigoma asili Rusambo”
Kwa miaka mingi nguvu za kiuchumi za wakazi wa mji huo imekuwa ikitegemea Ziwa Tanganyika kwa uvuvi na usafiri wa kwenda na kutoka maeneo mbali mbali ya mwambao wa ziwa hilo zikiwemo nchi jirani za Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Pamoja na kupoteza uimara wake, Mji wa Ujiji na Kigoma kwa ujumla umeibuka upya katika miaka ya karibuni kwa kutoa watu waliojipatia umaarufu mkubwa katika eneo lote la Afrika Mashariki na kati ikiwa ni pamoja na wasanii wa muziki wakiwemo Naseeb Abdul anaejulikana zaidi kama Diamond, Wanasoka wastaafu Kitwana Manara, Kassim Manara, Edibily Lunyamila na hata nahodha wa sasa wa Timu ya Taifa ya Tanzania Juma Kaseja .
Tangu enzi za Ukoloni watu kutoka maeneo mbalimbali ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Rwanda na Zambia waliingia mji wa Ujiji hasa kipindi cha utawala wa biashara ya watumwa.