Na Kalunde Jamal, Mwananchi
Posted Septemba14 2013 saa 13:15 PM
Posted Septemba14 2013 saa 13:15 PM
Kwa ufupi
Majuto anasema kuwa baada ya kutoka Kenya alirejea
nchini mwaka 1987 na kujiunga na Kundi la DDC Kibisa. Hata hivyo
hakudumu muda mrefu na kundi hilo kwani aliugua Kifua Kikuu na
kulazimika kukaa nje ya ulingo kwa mwaka mzima. Kabla ya kurejea
alijiunga na Kundi la Muungano Cultural Troupe, alikwenda Kundi la
Makutano.
Majuto anasema kuwa baada ya kutoka Kenya
alirejea nchini mwaka 1987 na kujiunga na Kundi la DDC Kibisa. Hata
hivyo hakudumu muda mrefu na kundi hilo kwani aliugua Kifua Kikuu na
kulazimika kukaa nje ya ulingo kwa mwaka mzima. Kabla ya kurejea
alijiunga na Kundi la Muungano Cultural Troupe, alikwenda Kundi la
Makutano.
Anasimulia kuwa alipoondoka Makutano alijiunga na
Kundi la Super Mama lililokuwa na makazi yake Morogoro kabla ya kujiunga
na Kundi la TOT mwaka 1993, lakini mwaka 1994 alijitoa kwenye kundi
hilo baada ya kuona maslahi madogo.
Kuanzia hapo Majuto alianza kujitegemea kufanya kazi binafsi na kupata mikataba kwa watu na kampuni mbalimbali.
Anakumbuka Redio ya Abood ya mjini Morogoro kuwa
ndiyo ilikuwa ya kwanza kumpa mkataba uliokuwa wa mwaka mmoja, ambapo
alicheza mara moja kwa wiki na kila alipocheza alilipwa Sh200,000 na
kutumia vifaa vya ofisi hiyo.
“Kazi hii ilinilipa sana, kwani hata bati
nilizoezekea nyumba yangu nilizinunua huko. Abood ilinilipa vizuri na
nilishirikisha familia kwa kipato changu. Mke wangu na wanangu walikuwa
wakiigiza pamoja nami, hivyo kila kilichopatikana mimi ndiyo nilikuwa
nakipangia matumizi na yalikuwa ya kifamilia,”anasema Majuto.
Kuanza kurekodi kanda za vichekesho
Anabainisha kuwa mwaka 1999 aliamua kurudi
nyumbani kwao mkoani Tanga na kuanza kufanya maonyesho yake kwenye kumbi
mbalimbali, ambapo alikutana na mtu aliyemtaja kwa jina moja la
Ramjuuni (marehemu kwa sasa) na huyo ndiye aliyeanza kurekodi na kutoa
mikanda ya vichekesho vya Majuto.
“Nilikuwa mtu wa kwanza kutoa vichekesho katika
mikanda na ilikuwa ni analojia, haikuwa katika ubora unaotakiwa, lakini
ndiyo nilizidi kuwa maarufu kupitia mikanda hii,”anasema Majuto.
Anasema kuwa nyingine iliyomfanya afahamike zaidi ni Vitimbi Mitaani, ambayo ilifanya kila mtu afahamu uwezo wake.
Kitu ambacho sintokisahau
Anasema kuwa baada ya kufanya kazi na watu wengi,
aliingia mkataba na Kampuni ya Al- Riyami, iliyo chini ya Abdallah
Riyami wenye thamani ya Sh20 milioni, bahati mbaya alipata ugonjwa wa na
kulazimika kufanyiwa upasuaji.
Anabainisha kuwa baada ya kupona aliambiwa akae
mwezi mmoja bila kufanya kazi, lakini bosi wake alimweleza kuwa akikaa
muda huo bila kufanya kazi, hatomlipa kwa kuwa amemwajiri ili afanye
kazi ndipo amlipe.
Anakumbuka kuwa pamoja na maneno hayo yeye alikuwa akidai
Sh500,000 kwa bosi wake huyo, lakini alipokumbusha aliambiwa kuwa
hatamlipa pesa hizo kwa kuwa Al- Riyami alikuwa akiwadai watoto wa
Majuto waliokuwa wakifanya kazi dukani, aliodai walimtia hasara, hivyo
Majuto akabaki hana kitu.
“Nikawa na njaa, huku nikiwa na familia. Nikaanza
kucheza nje ya mkataba, Al- Riyami akachukia na kutaka kunipeleka
mahakamani. Lakini, Mungu si Athumani, nikapata mtu wa kuokoa
jahazi,”anasema Majuto huku akiangua kicheko.
Anasema kuwa hata hivyo, kabla ya kupelekwa
mahakamani kwa mara ya kwanza akitakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha za
mkataba, Kampuni ya Azam Tv wakamwita kwa ajili ya kufanya naye kazi.
Anaweka wazi kuwa aliwaambia kuwa ana mkataba wa
Al-Riyami ulio na deni analotakiwa kulipa na Azam wakalipa deni na
kumchukua kwa mkataba mpya wa mwaka mmoja.
Chini ya mkataba huo Majuto ana uwezo wa kufanya kazi sehemu yoyote kwa masharti ya kutoa taarifa ili Azam wakimhitaji wampate.
Anaongeza kuwa alipata mkataba mnono wa Sh1
milioni papo hapo kila anaporekodi tangazo akipata pia mshahara wa
Sh200,000 kwa mwezi akiwezeshwa pia kwa bidhaa zinazozalishwa na Kampuni
ya Azam.
“Nagonga matangazo kwa ajili ya vipindi vya Tv
Azam vitakavyoanza kurushwa hivi karibuni. Huwezi kuamini jinsi maisha
yanavyobadilika uzeeni na ghafla,”anasema Majuto akifurahia, huku
akitingisha mguu.
Biashara
Kwa nini aliamua kucheza filamu za kawaida.
Mbali na uigizaji, Majuto anafanya biashara ya usafirishaji
abiria ndani ya Jiji la Tanga hutumia magari matatu anayomiliki maarufu
kwa jina la King Majuto The Super Star.
Hata hivyo anasema haikuwa rahisi kumiliki
biashara hiyo ambayo imetokana na uigizaji, kwani ilimbidi kupanga na
kujua afanye nini kwanza kabla ya kuamua kufanya biashara hiyo, huku
akilalamika kuwa hailipi kwa mji wa Tanga, tofauti na ilivyo kwa Dar es
Salaam.
“Lakini kwa kuwa ameamua kuishi Tanga, nakubali
matokeo. Hapo nyuma muda wa kukaa na familia yangu ulikuwa mdogo sana na
nilikuwa nakimbizana na maisha, lakini sasa nina angalau ka uwezo
kidogo waje wanaifuate wenyewe huku,”anasema Majuto.
Pamoja na daladala hizo Majuto pia anamiliki gari
aina ya Noah ambalo ndiyo gari lake la kutembelea, hata anapofanya
safari zake za kikazi.
Anasema kuwa kujiamini kuwa anaweza na kutaka
kubadilika kulingana na kipaji chake ndivyo vilivyomsukuma kuanza
kucheza filamu za kawaida.
“Njaa inakupa akili ya kufanya kitu tofauti ili
kuongeza kipato na ndiyo hiyo hiyo inanifanya nibadilike kama kinyonga.
Komedi mimi, filamu mimi, majukwaani mimi na bado hata ikija aina gani
ya uigizaji, naamini nitaweza kwa kuwa hiki ni kipaji cha kuzaliwa
nacho,”anasema Majuto.
Anaongeza kuwa mbali na njaa, katika tasnia ya
filamu kuna umuhimu wa kuwepo watu kama yeye, ambao watakuwa ni kama
washauri pale watakapoona kuna kitu kimekosewa.
Endelea kufuatilia sehemu ijayo ya makala kuhusu nguli King Majuto. Je, ataeleza nini kuhusu familia yake? Mama MajutoSOURCE: MWANANCHI