Monday, 16 September 2013

Elimu ni maendeleo...ukiibeza umeumia!

15th September 2013
Yapo maeneo katika jamii ambayo hayastahili kuchezewa kabisa, elimu ni msingi mkubwa wa maendeleo katika taifa lolote duniani, unaweza kuangalia kwa nia ya kutathmini mfano wa mataifa yaliyoendelea, utagundua mara moja kuwa kigezo kikubwa na msingi wa maendeleo yao ni kutokana na mfumo thabiti wa elimu yao.

Huwezi kuongelea mafanikio ya teknolojia katika fani yoyote kama wananchi waliopo ni mbumbumbu!
Sina uhakika kama mitihani ya darasa la saba iliyofanyika nchini wiki hii haikupambana na kashfa ya uchakachuaji. Nina imani kuwa matatizo yaliyojitokeza kwenye mitihani ya darasa la saba mwaka jana, yalitoa funzo kubwa kwa wandaaji kufuata maadili ipasavyo.
Dhamira ya serikali ya kumsomesha kila mwanafunzi hadi kidato cha nne ni kwa ajili ya kuinua kiwango cha ufahamu wa wanafunzi ili wanapohitimu katika ngazi ya elimu hiyo, waweze kuwa tayari kujijengea taswira ya kujitegemea zaidi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi. Umri wa vijana wanaohitimu kidato cha nne unawaruhusu kupanga na kutambua nini jambo la msingi katika maisha ya baadaye.
Tumekuwa mashahidi wa kusikia vurugu za mitihani katika ngazi ya elimu ya sekondari, imekuwa kama jadi sasa kwamba kila mwaka matukio ya aina hiyo hujitokeza, lakini kwa mwaka jana, suala hilo ni kama lilivuka mpaka, kwa kuhujumu mitihani ya darasa la saba sasa kunaonesha dalili za kutaka kuzamisha kabisa elimu.
Na kumpelekesha mtoto ajiunge na elimu ya sekondari kwa njia za mizengwe mizengwe kutatuzalishia vijana wa kidato cha nne wasiokuwa tofauti na wahitimu wa darasa la saba.
Mwishoni mwa mwaka jana, Katibu Ofisi ya Rais, Sekretariet ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi aliwataka wahitimu na wale wote wanaopeleka maombi ya nafasi za kazi katika Sekretariet ya Ajira, kuwasilisha vyeti vyao halali na kuachana tabia ya kutumia vyeti vya kughushi.
Xavier alionya kuwa wanaobainika kughushi vyeti, watachukuliwa hatua za kisheria. Hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia ofisi yake kukamilisha utaratibu wa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wote watakaobainika kughushi vyeti wakati wa kupeleka maombi ya kazi.
Xavier alisema kazi ya kukagua vyeti vya kughushi ni ya kudumu kwa mujibu wa taratibu walizojiwekea na kwamba utaratibu huo utaendelea kufanyika kwa fani zote na kwa ngazi zote za nafasi za kazi.
Hali hiyo imesababishwa na mfumo dume wa kuzoea 'short-cut' ya kujitafutia sifa za elimu.
Inaanza katika elimu ya msingi ambako mchakato wa uchakachuaji wa mitihani ulijidhihirisha mwaka jana, na inawezekana kabisa wale waliobainika kujihusisha na ujanja huo ni sehemu tu ya jumla yao.
Miaka miwili iliyopita kuna baadhi ya waliodaiwa kuwa wasomi, wengine wakiwa maofisa wakuu serikalini waliotuhumiwa kuwa na vyeti kutoka vyuo vikuu visivyotambulika, uamuzi uliofanyika ni kuvifanyia uchunguzi vyeti hivyo ili kubaini uhalali wake.
Kinachosikitisha zaidi ni kwa namna gani vyuo vinavyotoa vyeti hivyo navyo visijulikane! Ni kweli zipo shule nyingi za sekondari zisizosajiliwa, lakini mwisho wa siku wahitimu wake hufanya mitihani katika shule zilizosajiliwa na vyeti vyao vikawa halali, sasa ni kwa mbinu gani vyuo vikuu vikasomesha watu kiwango cha elimu ya shahada bila vyuo vyenyewe kutambulika?
Utashangaa ni kwa nini watoto wa wenye uwezo kiuchumi wamejitokeza kuwa katika ushindani mzuri wa ajira katika sekta nyingi, inawezekana sababu mojawapo ni kwao kuwa na vyeti vizuri zaidi kitaaluma.
Inawezekana pia vyeti hivyo ni vya kutoka vyuo binafsi visivyosajiliwa rasmi. Watoto waliosoma kwa uwezo wa fedha za wazazi wao huwa hawafeli, wanaendelea kufaulu hata baada ya elimu ya vyuo vikuu!
Baadhi yao unawakuta na vyeti vikubwa vya taaluma zaidi ya moja, na kwa bahati mbaya sana inaonekana vyeti vinachukua uzito zaidi kuliko elimu aliyo nayo mwenye cheti.
Mitandao inachangia sana katika kuchakachua elimu za watu, unaweza kukumbana na mwenye cheti cha taaluma za wahudumu wa hoteli, kinachoonyesha mhusika alihitimu toka Chuo Kikuu Binafsi kiitwacho 'Blisstone University' kilichoko Kingstone huko Jamaica.
Ukiangalia maelezo yake binafsi (CV) utakuta mazoezi kwa vitendo aliyoyafanya katikati ya muhula wa mafunzo ilikuwa katika hoteli ya 'Birthcane Resort' huko huko Jamaica.
Ukichunguza zaidi utagundua mwenye cheti hicho hajawahi kusafiri nje ya nchi hii, maisha yake yote ni Dar es Salaam na kwao Magu.
Katika taasisi nyingi za umma na hata zile za binafsi, utafiti umeonesha kuwa waajiriwa wengi wazalendo wanafanya kazi chini ya kiwango, na ndiyo maana maeneo mengi ya kazi, na hasa waajiri binafsi, wanapata ugumu kutoa ajira kwa Watanzania.
Nafasi kubwa za ajira katika mahoteli, mabenki, migodini, nk. zimeshikwa na wageni, ambao kimsingi ni watendaji wanaofanya kazi kulingana na sifa zilizomo ndani ya vyeti vyao.
Mambo yote huimarika kama msingi wake ulikuwa imara, hata kwenye michezo, timu ya mpira ya taifa imekuwa ikiboronga kila wakati katika michezo ya kimataifa kutokana na kuwa na misingi mibovu ya maandalizi kwa wachezaji wake.
Unapoteua wachezaji katika timu kubwa kutokana na kuwaona katika michezo miwili au mitatu, unakuwa bado huna uhakika na viwango vyao, na pia unakosa uhakika wa ushindi.
Timu nzuri huandaliwa kwa muda mrefu, wachezaji wazuri waandaliwe tangu wakiwa wadogo. Elimu pia inatakiwa ienziwe kuanzia shule za msingi, hatutakuwa na wasomi wazuri kama tukiachia elimu ichakachuliwe kuanzia shule za Chekechea.
Maoni: 0762-233116 na 0715-047304  
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI