15th September 2013
Ni
nani anatuloga Watanzania, ingawa kwa baadhi yetu, kufikia hatua ya
ndugu wa nchi moja, kushamirisha vitendo viovu vinavyoathiri utu na
heshima ya binadamu?
Uovu dhidi ya ubinadamu unaofanyika, unatokana na utashi binafsi ama ‘nguvu za nje’ zinazotufanya kuonekana wajinga kiasi hiki?
Kwa maana safari ya kulijenga ‘taifa ovu’
lenye ‘waovu’ na matendo maovu, inazidi kusonga mbele, hakuna udhibiti
unaofanyika kiasi cha kuiaminisha jamii, kwamba tupo imara.
Katika siku za hivi karibuni, nchi imekumbwa na aibu, matendo maovu yanafanywa dhidi ya raia wasiokuwa na hatia, nchi imetulia!
Wapo wanaoamini kuwapo kwa vitendo viovu dhidi ya ubinadamu ndani ya Tanzania, kwa miongo kadhaa sasa. Inawezekana.
Wapo wenye orodha ya majina na picha za
raia waliowahi kutendewa uovu kwa kupigwa, kunyanyaswa, kuporwa mali na
wengine kufa, tena kwa namna ya kizembe.
Ingawa ni hivyo, lazima ikubalike kwamba
kwa muda mrefu, Tanzania imekuwa mahali salama pa kuishi. Amani na
utulivu vikawa miongoni mwa nguzo kuu za umoja wa kitaifa.
Tukalelewa hivyo, tukakua hivyo na kuishi
hivyo, japokuwa kwa kizazi ambacho kwa mujibu wa idadi ya miaka ya uhai
wao, sasa wanaondoka duniani kupitia ‘mauti ya haki’.
Kizazi kilichopo ndicho kinachoushuhudia
uovu ambao, kutokana na ukosefu wa takwimu sahihi, hakuna sababu ya
kuulinganisha na mwingine uliowahi kutokea kwa ‘kizazi kinachoondoka’.
Ninajua wazi kwamba jamii iliyo hai, haikosi kuwapo na tofauti za fikra, maneno, hulka, matendo na mengineyo.
Lakini uwapo wa tofauti hizo hauwezi kuwa sababu ya kuibua, kutenda na kuendeleza vitendo viovu dhidi ya ubinadamu na wanadamu.
Miongoni mwa matendo maovu yanayolikabili taifa ni kushambuliwa, kujeruhiwa na kuuawa kwa viongozi wa dini.
Inapotazamwa orodha ya viongozi hao,
Kanisa Katoliki hususani upande wa Zanzibar, linakuwa miongoni mwa
waathirika wakuu wa uovu huo.
Wapo viongozi wengine waliojeruhiwa,
wakiwa katika idadi inayoweza kulingana na wale wa Kanisa Katoliki ama
kuwa chini ya hao, lakini ukweli unabaki kwamba wote wanabeba uzito
unaolingana-matendo maovu dhidi ya ubinadamu.
Inawezekana mashambulizi, kujeruhi na
kuwaua viongozi wa dini kusihusishwe na tofauti za kidini, isipokuwa
ushiriki wa waovu kama wanavyoshiriki katika uovu mwingine.
Kwa maana haingii akilini, kwamba kwa
shambulizi la juzi la Padre Joseph Mwang’amba, anayehudumiwa kituo cha
malezi ya vijana wa Zanzibar, atendewe unayama huo!
Ni nani asiyetambua changamoto
zinawakabili vijana, kwamba ‘awe kipofu’ kiasi cha kukerwa na
utekelezaji wa majukumu ya Padre Mwang’amba, kiasi cha kummwagia
tindikali? Haingii akilini!
Kama nilivyokuwa nikielezea katika makala
zangu zilizopita, tukio kama hilo la juzi huko Zanzibar, linapaswa
kuhusishwa na mfumo unaochochea kushamiri kwa vitendo hivyo.
Kuangalia malezi wanayoyapata vijana ndani
ya familia, majirani na jamii inayowazunguka. Yanayotolewa kwa kadri
inavyostahili, haki na usawa?
Kwa maana kama wazazi na walezi
hawatatimiza wajibu wao ipasavyo, wakitegemea ‘dunia’ itafunza watoto
ama vijana, inakuwa mfano wa kufungua ‘mlango wa uovu’ nchini, kizazi
cha sasa kikaingia.
Mbali na wazazi ama walezi, viongozi wa
jumuiya za watu, wakiwamo watendaji na watumishi wa umma (serikali),
wanatekeleza wajibu na majukumu yao kwa raia na taifa?
Haiwezekani kwa nchi yenye viongozi
wasiokuwa na maono, mtazamo chanya na uthubutu wa ‘kulijenga taifa
imara’ lisilokuwa na matendo maovu kama kuwashambulia, kuwajeruhi ama
kuwaua wasiokuwa na hatia.
Upo msemo wa Kiswahili, kwamba ‘serikali
ina mkono mrefu’. Lakini inakuwaje mkono huo ushindwe kuzibaini mbinu,
mfumo na mtandao unaotumika katika utekelezaji wa matendo hayo?
Kwamba linatokea tukio la kwanza, la pili,
la tatu na kuendelea, yote yakiwa na `taswira’ inayofanana, kwamba
kikipatikana chanzo kimoja, mtandao mzima utajulikana, nini kinafanyika
kwa walio na mamlaka ya kulitekeleza hilo!
Ama ni kauli za kipropaganda, zinazopambwa
na ahadi za ‘tumejipanga, tutawasaka wahusika na kuchukua hatua kali
ili tukio kama hilo lisotokee tena.’
Zinapotolewa kauli kama hizo, watu
wanajisahau siku kadhaa, kunaibuka tukio jingine, inashangaza na kuikera
jamii, hata wengine kufikia hatua ya kufikiria ‘waingie kazini’
kujilinda na kuwadhibiti wanaowashambulia na kuzishambulia mali zao.
Wapo viongozi wa dini wanaoweza kuwa
sehemu ya kushamirisha uovu unaotendeka sasa, kutokana na muingiliano
wao dhidi ya walio katika utawala, wakashindwa kutimiza wajibu wao.
Viongozi wa dini wanapaswa kuwa huru,
wakishirikiana na watawala, walio katika utawala na wanasiasa kwa namna
ya ubinafsi, pale wanapoingia kwenye nyumba za ibada ‘kuziokoa’ roho zao
dhidi ya dhambi.
Lakini inapotokea kiongozi wa dini kuwa
mshirika wa karibu wa mtawala wa kidunia, walio katika utawala ama
wanasiasa, inakuwa vigumu kutimiza wajibu wao wa kuonya na kukaripia,
japo kwa unyenyekevu wote.
Kwa hali hiyo, safari ya amani, umoja na
mshikamano nchini ni kama imezongwa na miiba. Miiba inazidi kumea,
inasongea karibu na kutaka kuiathiri, isiendelee kumea.
Hapo ndipo ninapokitazama kizazi chetu,
ninakililia. Ninaitazama nchi yetu, ninaililia, kwamba miiba hiyo
inapozidi kusogea, nini hatima yake?
Si wakati wa kunyoosheana vidole, bali kupambana ili uovu unaotokea sasa, usiwe sehemu ya `utamaduni’ wa Mtanzania.
Kwa maana walio katika orodha, wakifikia
ukomo wa kupigwa, kujeruhiwa ama kuuawa, watawageukia walio katika
shirika nao, watawageukia ndugu na jamaa zao, watawatenda vivyo hivyo,
kwa mujibu wa historia ya mwanadamu.
Hali ikiwa hivyo, nchi haitakuwa salama, kwa wanaolengwa na hata watekelezaji wenyewe. Haipaswi kufika huko.
Tuchukue hatua!
Mashaka Mgeta ni Mhariri wa Makala
wa gazeti hili na mchambuzi wa masuala ya siasa. Anapatikana kupitia
simu namba +255754691540/716635612 ama barua pepe: mgeta2000@yahoo.com.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI