Wednesday 18 September 2013

Kafulila amwomba Rais Kikwete kuwasaidia wazawa wa Kigoma


Na Patricia Kimelemeta

Posted  Jumatano,Septemba18  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Tunamwomba Rais Kikwete kuingilia kati operesheni hii kwa sababu inasababisha wananchi wazawa kuingizwa kwenye mkumbo usiowahusu, jambo ambalo linaweza kusababisha migongano ya hapa na pale.

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuwachagua watu wenye utaalamu wa kuwabaini wahamiaji haramu ili waweze kuwabaini bila ya kunyanyasa wananchi wazawa.
Akizungumza katika mkutano wa Umoja wa Wananchi wa Mkoa wa Kigoma uliofanyika Dar es Salaam jana, Kafulila alisema, kitendo cha kuwakamata ovyo wananchi wa mkoa huo ambao ni wazawa ni cha udhalilishaji na kwamba kinapaswa kupingwa kwa nguvu zote.
“Tunamwomba Rais Kikwete kuingilia kati operesheni hii kwa sababu inasababisha wananchi wazawa kuingizwa kwenye mkumbo usiowahusu, jambo ambalo linaweza kusababisha migongano ya hapa na pale,” alisema Kafulila. Aliongeza, utaratibu unaotumika siyo mzuri, unasababisha malalamiko na mvutano, hivyo aliitaka Serikali kuwatumia wataalamu wenye ujuzi na mbinu zinazofaa zaidi.
“Zoezi hili mkoani Kigoma linahusisha hadi wazawa, huku wanaoendesha operesheni hiyo wakiwa hawana utaalamu, jambo linalosababisha usumbufu, Serikali inapaswa kuangalia utaratibu mpya.”
Mratibu wa umoja huo, Raymond Kulikiza alisema, hawapingi operesheni hiyo, lakini kitendo cha unyanyasaji kwa wananchi wa mkoa huo ndicho kinachowafanya walalamikie.

SOURCE: MWANANCHI