Wednesday, 4 September 2013

Kibanda, Mwigamba wajitetea


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando (katikati), akifurahia jambo na Meneja Uendelezaji Biashara, Theophil Makunga na Mwanasheria MCL, Doris Marealle nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, kabla ya kuanza kwa kesi ya uchochezi inayomkabili Makunga na wenzake wawili. Picha na Venance Nestory, 

Na Hadija Jumanne  (email the author)

Posted  Jumanne,Septemba3  2013  saa 20:21 PM
Kwa ufupi
Akitoa utetezi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mwigamba alidai makala hiyo ililenga kutoa maoni kwa kuwaelimisha askari wote nchini, ili wasivunje haki ya katiba kwa raia.


Dar es Salaam, Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya makala inayodaiwa kuwa ya uchochezi, Samson Mwigamba (38), amekana kuandika makala ya uchochezi alipokuwa akijitetea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu Dar es Salaam.
Mshtakiwa wa pili, Absalom Kibanda, ambaye alikuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media inayomiliki gazeti la Tanzania Daima, naye alisema makala hiyo ilikuwa sahihi ndiyo maana Serikali kupitia Idara ya Habari (Maelezo) haikutoa onyo kwao.
Mshtakiwa wa tatu, Meneja Uendelezaji Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Theophil Makunga, ambaye aliunganishwa kwenye kesi hiyo kutokana na gazeti hilo lilichapishwa Kiwanda cha Uchapaji cha Kampuni ya MCL, wakati alipokuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, atajitetea Septemba 23, mwaka huu.
Akitoa utetezi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mwigamba alidai makala hiyo ililenga kutoa maoni kwa kuwaelimisha askari wote nchini, ili wasivunje haki ya katiba kwa raia.
Akiongozwa na wakili wake, Nyaronyo Kicheere, Mwigamba alidai waraka alioandika ulilenga kutoa maoni kwa askari wasivunje haki ya katiba kwa raia katika mambo mawili; haki ya kuishi na haki ya kuandamana.
Naye Kibanda alidai makala hiyo haikuwa habari ya kawaida, bali ni maoni ya mwandishi, kama ambavyo msomaji yeyote anaweza kutoa gazetini.
Kibanda alidai makala hiyo ingekuwa na tatizo msajili wa magazeti nchini, angefungia gazeti au angeandika barua ya wito wa onyo. “Makala hiyo inaangukia katika kundi la maoni na haya ni maoni ya mwandishi,” alidai Kibanda na kuongeza:
“Makala hiyo ilikuwa ni mahususi kwa ajili ya kupasha na kuelisha jamii, lakini ni maoni siyo habari.” alidai.

source : Mwananchi