Posted Jumatano,Septemba25 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Tumetiwa moyo na ufafanuzi wa Rais ambao tunadhani haukuacha shaka yoyote kwa yeyote aliye na nia njema na nchi yetu.
Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa wiki alijikuta
katika wakati mgumu akiwa ziarani nchini Marekani alipolazimika kutumia
muda mrefu kukanusha madai kwamba operesheni ya kuwaondoa wahamiaji
haramu nchini imelenga kuwaondoa wakimbizi. Hatua hiyo ya Rais Kikwete
imekuja baada ya kuwapo kwa upotoshaji wa makusudi kuhusu uamuzi wa
Serikali kuwarudisha makwao wahamiaji wote walioingia nchini kinyume cha
sheria.
Upotoshaji huo wa makusudi ulianza taratibu mwezi
uliopita mara tu baada ya Rais Kikwete kuwapa wahamiaji hao haramu wiki
mbili kurudi makwao na kusema muda huo ukiisha ingeanzishwa operesheni
ya kuwaondoa watu hao kwa nguvu. Bila shaka Rais alipoondoka nchini
kuelekea Marekani hakuwa na chembe ya fununu kwamba upotoshaji huo
ungesababisha awekwe ‘kiti moto’ na moja ya Kamati za Bunge la nchi hiyo
kuhusu madai hayo.
Kinachotutatiza hapa siyo Rais wetu kutoa
ufafanuzi, isipokuwa kile kinachoonekana kama usahaulifu kwa upande wa
jumuiya ya kimataifa kwamba Tanzania kwa miongo mingi imekuwa kimbilio
kubwa la maelfu kwa maelfu ya wakimbizi kuliko nchi nyingine yoyote
barani Afrika. Hivyo, kufikiri kwamba Tanzania inaweza ghafla kubadili
sera yake ya kuhifadhi wakimbizi na badala yake kuwa moja ya nchi
zinazowanyanyasa, kuwatesa na kuwatenga ni jambo ambalo hakika haliingii
akilini. Tanzania sasa inahifadhi wakimbizi 264,000 kutoka Congo (DRC)
na Burundi katika kambi zilizopo mkoani Kigoma.
Tumetiwa moyo na ufafanuzi wa Rais ambao tunadhani
haukuacha shaka yoyote kwa yeyote aliye na nia njema na nchi yetu.
Kwamba Tanzania haijamfukuza mkimbizi hata mmoja, isipokuwa waliofukuzwa
ni wahamiaji haramu walioingia na kuishi nchini kinyume cha sheria na
taratibu za uhamiaji. Kama alivyosema mwenyewe, Tanzania haina sababu ya
kuwafukuza wakimbizi na kama ingelazimika kufanya hivyo, taratibu za
kimataifa zingefuatwa, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Umoja wa
Mataifa na mamlaka za nchi walizotoka.
Sasa hapo shida iko wapi? Hivi wapotoshaji wa
Operesheni hiyo wana ajenda gani? Kwamba ni haki kweli Tanzania iendelee
kubeba mzigo wa wakimbizi, huku pia ikiendelea kuwa kichaka cha
wahamiaji haramu ambao wanashutumiwa kwa vitendo vya ujambazi, utekaji
nyara mabasi, uvamizi wa misitu ya asili na hifadhi? Ni haki kweli
waachwe waendelee kuingiza maelfu ya mifugo katika maeneo tengefu na
kusababisha mmomonyoko wa ardhi? Ni haki kweli Watanzania waendelee
kuishi kama mateka na watumwa katika nchi yao kwa kuogopa kuwatimua
wahamiaji haramu wanaosababisha raia kuishi maisha ya zahama na hofu?
Sisi tunasema Rais Kikwete na Serikali yake
wasirudi nyuma mpaka hapo mhamiaji haramu wa mwisho atakapokuwa
ameondoka katika ardhi yetu. Tunaambiwa kwamba wahamiaji haramu 194
waliorudishwa makwao wamekataliwa na nchi zao na kurejeshwa tena nchini.
Tunasema watu hao wakabidhiwe kwa UN, kwani Tanzania tayari imetimiza
wajibu wake.
Pamoja na yote hayo, lazima tukubali ukweli kwamba
nchi yetu imefanywa shamba la bibi kutokana na udhaifu wa watendaji
katika ngazi zote za uongozi kuendekeza vitendo vya rushwa. Wahamiaji
haramu wengi hawakuingia nchini kwa kificho, bali walifanya hivyo mchana
kweupe na kwa baraka zote za baadhi ya viongozi wa vitongoji hadi
wilaya. Ni vyema sasa Serikali ikafunga ukurasa huo wa aibu wa wahamiaji
haramu kuiona nchi yetu kama haina wenyewe.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI