Na Mussa Juma
Posted Alhamisi,Septemba26 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Septemba26 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
“Wananchi wanataka amani kwani migogoro imeshasababisha vifo na mali nyingi kupotea sasa tunataka amani,”
Samunge. Wakazi wa Kata ya Samunge, wilayani
Ngorongoro Mkoa wa Arusha, jana walimpokea Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kwa mabango wakiomba Serikali iligawe Jimbo la Ngorongoro na ikomeshe
mapigano ya kikabila.
Wananchi wa Kijiji cha Yasimdito, wakiwamo
wanafunzi walisimama pembeni mwa barabara na mabango hayo na Waziri Mkuu
alilazimika kusimama na kuwataka wananchi hao kufafanua maudhui ya
mabango hayo.
Diwani wa Kata hiyo, Jackson Sandea alisema
wananchi hao ambao ni Wasonjo wamechoshwa na vita na Wamasai wa koo ya
Loita kugombea ardhi na kwamba wanataka mipaka ianishwe.
“Wananchi wanataka amani kwani migogoro imeshasababisha vifo na mali nyingi kupotea sasa tunataka amani,” alisema Sandea.
Kiongozi wa mila wa jamii ya Wasonjo (Batemi),
Mwanamiji Peter Dudui alisema tangu uhuru, jamii yao yenye watu wachache
haijawahi kuwa na mbunge wala kiongozi mwingine wa kuchaguliwa wa ngazi
ya wilaya au mkoa. “Waziri Mkuu, tunaomba tuwe walau na jimbo letu
kwani kutokana na uchache wetu, hatuwezi kupata mbunge. Pia tunaomba
kupatiwa huduma bora za maji na elimu,” alisema Dudui.
Waziri Mkuu alisema Serikali itafanyia kazi maombi ya wananchi hao ili kuhakikisha wanaishi kwa amani na kupata maendeleo.
“Nadhani kama hoja ni kupata huduma muhimu,
Serikali inaweza kutazama kama mnaweza kuwa na halmashauri mbili katika
wilaya hii,” alisema.
Kuhusu mgogoro wa ardhi, alizitaka pande zote
kumaliza uhasama na kwamba Serikali itaendelea kudumisha amani na
kuhakikisha vijiji vinapimwa.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI