Wednesday, 25 September 2013

Mwanachama wa Al-Shabaab aliyetoroka bado hajapatikana, mkuu wa gereza Mogadishu akamatwa

Polisi na askari wa Somalia wakiwalinda wanachama 15 wanaoshukiwa kuwa wa al-Shabab katika jela ya muda mjini Mogadishu mwaka 2012. [Na Abdurashid Abdulle Abikar/AFP]

Na Ali Adam, Mogadishu

Septemba 24, 2013
 
Wiki mbili baada ya mfungwa wa al-Shabaab Abdirahman Ali Abukar kutoweka kutoka Gereza Kuu la Mogadishu, mtoro huyo bado hajakamatwa na viongozi hawajaelezea jinsi gani alikimbia na jukumu gani -- kama lipo -- wa maafisa wa gereza katika mpango huo.
Polisi na askari wa Somalia wakiwalinda wanachama 15 wanaoshukiwa kuwa wa al-Shabab katika jela ya muda mjini Mogadishu mwaka 2012. [Na Abdurashid Abdulle Abikar/AFP]
Maafisa wa Somalia hapo tarehe 11 Septemba walimtia mbaroni mkuu wa gereza, Kanali Mohamed Hussein Ahmed Sabdow, na maafisa wanne wa Kikosi cha Magereza cha Somalia kwa tuhuma za kumsaidia Abukar kutoroka siku moja kabla.
Maafisa wengine wawili wanaoshukiwa kuchukua hongo ili kumsaidia mwanamgambo huyo kutoroka wamekwepa kukamatwa, afisa wa Kikosi cha Magereza cha Somalia Hassan Ibrahim aliiambia Sabahi.
Abukar, mwenye umri wa miaka 32, alitiwa mbaroni tarehe 7 Aprili, 2012, akiwa anamiliki ukanda wa mlipuko, ambao alikusudia kujilipua mwenyewe na kumuua aliyekuwa naibu kamanda wa Jeshi la Taifa la Somalia Jenerali Abdikarim Yusuf Aden Dhagabadan, Ibrahim alisema.
"Mtu huyu wa al-Shabaab aliwasiliana na Khalif Ali Nur, dereva wa Jenerali Dhagabadan, na kumuomba arahisishe mauaji aliyokuwa amepanga kwa kutoa pesa," Ibrahim alisema. "Dereva alitoa taarifa juu ya mpango huo na hivyo ndivyo jinsi alivyokamatwa."
Abukar alitoweka katika chumba chake gerezani tarehe 10 Septemba na mpango wa kumsaka ukaanza mara moja, lakini hakuonekana kamwe. Usalama tangu wakati huo umeimarishwa gerezani, Ibrahim alisema, ambako kiasi cha wanamgambo 100 wa al-Shabaab wamefungwa katika upande maalumu.

Maswali makubwa

Sabdow na maafisa wengine wanne waliokamatwa kwa tuhuma ya kusaidia kutoroka kwa Abukar na kukubali hongo wanashikiliwa katika makao makuu ya Idara ya Uchunguzi wa Jinai (CID).
Mkuu wa CID Jeneral Abdullahi Hassan Barise alikana maombi juu ya kutoa habari za kukamatwa kwa watu hao lakini alikiri kwamba CID inachunguza kesi hiyo na kusema kwamba umma utajulishwa matokeo yake mara uchunguzi utakapokamilika.
Brigedia Jenerali Hassan Hussein Osman, mkuu wa Kikosi cha Magereza cha Somalia, alisema kwamba kitengo chake kilikuwa kinachunguza jinsi utorokaji huo ulivyotokea.
"Baadhi ya maafisa wa ulinzi wa gereza wamekamatwa kuhusiana na kesi hii na uchunguzi unaendelea ili kujua ni nani aliyehusika na kutoroka kwa mwanachama wa kikundi kinachopinga amani," aliiambia Sabahi. "Yeyote atakayepatikana na makosa kwa uhalifu huu atafikishwa mbele ya sheria."
Jenerali Mstaafu Mohamed Nur Galal, aliyekuwa naibu wa waziri wa ulinzi wakati wa utawala wa Mohamed Siad Barre, alisema kuwa tukio hili linaonesha kutowajibika kwa upande wa vikosi vya usalama.
Askari wa Somalia hawahudumiwi, hali linayoweza kuwaweka katika mazingira hatari ya kupokea hongo na njia nyengine za rushwa, aliiambia Sabahi.
"Ni muhimu kuhudumia mahitaji ya walinzi katika vituo vya magereza ili waweze kutekeleza majukumu kwa sababu afisa mwenye njaa hawezi kulinda chochote na anakuwa katika hatari ya kupokea hongo," Galal alisema.

SOURCE: SABAHI ONLINE