Friday 20 September 2013

Nape amwakia James Mbatia

Katibu wa itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akishiriki kuchimba msingi wa nyumba ya balozi wa shina Tawi la Isenge, wilayani Bariadi ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha watu kujitolea kukijenga chama hicho, mkoani Simiyu. Na Mpigapicha Maalumu 
Na Faustine Fabian, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Septemba20  2013  saa 9:14 AM
Kwa ufupi
Amtaka kujiuzulu ubunge aliopewa na Rais Kikwete, amshangaa kuungana na vyama vya Chadema, CUF kupinga kusainiwa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Siku chache baada ya Mwenyekiti  wa NCCR-Mageuzi na Mbunge wa Kuteuliwa, James  Mbatia kuungana na Chadema pamoja na CUF kupinga kusainiwa kwa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuendesha maandamano nchi nzima, Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye amekiita kitendo hicho kuwa cha kinafiki.
Nape alisema kitendo cha mbunge huyo kuungana na vyama vingine kupinga suala hilo  ni kumdhalilisha Rais Jakaya Kikwete aliyemteua kuwa mbunge kwa kumwamini kuwa mchapakazi, huku akiongeza kuwa kitendo hicho ni unafiki mkubwa.
Nape aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana kukagua utekelezaji  wa ilani ya CCM.
Alisema Mbatia aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa mbunge kutokana na kuonekana kuwa mchapakazi, huku akiongeza kuwa  kitendo alichokionyesha  mbunge huyo ni kumgeuka Rais kama kinyonga
Nape alienda mbali zaidi na kuongeza kuwa hatua ya mbunge huyo kuungana na wapinzani  siyo sahihi na haikubaliki hata kidogo, huku akimtaka kujiuzulu nafasi aliyopewa kwa heshima  na Rais,.
Katibu huyo mwenezi aliongeza kuwa viongozi wa Chadema wakiwemo Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, Dk Willbrod Slaa pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,Tundu Lisu, wamekuwa wakitumia matatizo ya Watanzania kama mtaji wao wa kisiasa na kwamba viongozi hao hawana aibu.

CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI