Sunday, 15 September 2013

PADRI ALIYEMWAGIWA TINDIKALI ZANZIBAR AHAMISHIWA MUHIMBILI...

Padri Anselmo Mwang'amba akiwa hospitalini.
Siku moja baada ya Padri wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Machuwi, Anselmo Mwang’amba kumwagiwa tindikali katika duka la mawasiliano ya intaneti la Sunshine, Mlandege mjini Unguja, amehamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mwang’amba ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Malezi kwa Vijana kilichopo Cheju wilaya ya Kati Unguja kinachomilikiwa na kanisa Katoliki, alifikishwa katika hospitali hiyo jana saa 3:00 asubuhi baada ya kusafirishwa kwa ndege ndogo ya Kampuni ya Coastal kutoka Zanzibar.
Alipofikishwa hospitalini hapo, Padri huyo alipokelewa katika kitengo cha dharura ambapo alipatiwa huduma katika kitengo hicho ikiwa ni pamoja na kufanyiwa vipimo mbalimbali kabla ya kuhamishiwa wodi namba 10 Kibasila.
Mara baada ya kuhamishiwa wodini, waandishi wa habari walitaka kumuona na kuzungumza naye, hata hivyo Padri Mwang’amba hakutaka kuzungumza kwa kile alichoeleza hana maelezo zaidi ya yale aliyozungumza baada ya kushambuliwa.
“Sina cha kuzungumza zaidi, naendelea vizuri kama mnavyoniona, nilichosema ni kile kile alichozungumza na mmeona katika magazeti,” alisema.
Muuguzi Mkuu katika jengo la Kibasila, Rutgard Rutabingwa alisema, “tumempokea mgonjwa wetu yuko katika hali nzuri, maendeleo yake yanaridhisha,” alisema.
Padri wa Kanisa Katoliki Minara Miwili lililopo eneo la Mji Mkongwe, Asenga Thomas ambaye ameambatana na Mwang’amba kutoka Zanzibar alisema maendeleo ya padri huyo ni mazuri na kwamba hata maumivu aliyokuwa anayasikia juzi baada ya tukio yamepungua.
“Ukiangalia hali ilivyokuwa baada ya tukio na leo (jana) utaona kuna tofauti kubwa, maumivu yamepungua, ndio maana hata usingizi amepata,” alisema.
Alisema Mwang’amba alishambuliwa juzi na watu wasiofahamika wakati akitoka katika duka  linalotoa huduma za mawasiliano ya intaneti.
“Alitoka nje baada ya kupigiwa simu na kijana wake mmoja, ghafla ndio alimwagiwa tindikali…inavyoonekana waliokusudia kufanya tendo hili walikuwa wanamfuatilia na walifahamu hiyo ni sehemu anayokwenda sana, ndio wakamvamia na kumjeruhi hivyo,” alisema.
Alisema inasikitisha kuona hali ya Zanzibar imegeuka hivyo watu wanashambuliana na kujeruhi wengine bila sababu za msingi, hali inayotishia amani na usalama wa wananchi wanaoishi visiwani humo.
 Daktari Abdalla Haidari wa hospitali ya Mnazi Mmoja amesema juzi kwamba Padri Mwang’amba amejeruhiwa usoni na kifuani kwa maji ambayo baada ya kuyafanyia uchunguzi wamebaini kuwa ni tindikali.
Tukio hili limekuja baada ya mwezi uliopita walimu wawili wa kujitolea, raia wa Uingereza walijeruhiwa kwa kumwagiwa tindikali katika maeneo ya mji Mkongwe, Shangani ambao ni Kate Gee (18) na Kristie Trup (18) walivamiwa na kujeruhiwa saa 1:00 usiku wakati wakienda kupata chakula cha usiku. Walikimbizwa Uingereza kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa muda katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Saalam.
Matukio mengine ya kushambuliwa ni pamoja la Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shekhe Fadhil Sulaiman Soraga aliyemwagiwa tindikali Novemba 6 mwaka jana, Sheha wa Shehia ya Tomondo, wilaya ya Magharibi Unguja, Mohamed Omar Said aliyemwagiwa tindikali Mei 23 mwaka huu.
Pia Padri Ambrose Mkenda aliyepigwa risasi na kujeruhiwa Desemba 26 mwaka jana na Padri Evaristus Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi  wakati akienda kanisani.
Kabla ya Padri Mwang’amba kupelekwa Dar es Salaam,  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein jana asubuhi alimtembelea hospitalini Mnazi Mmoja alikolazwa na kutoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kujitahidi kuimarisha uchunguzi wa  matukio ya watu kumwagiwa tindikali ili wahusika wapelekwe kwenye vyombo vya sheria.
“Hatuwezi kuviacha vitendo hivi viendelee... ni lazima Jeshi la Polisi lijitahidi kuwatafuta wahusika ili sheria ichukue mkondo wake,” alisisitiza Dk Shein.
Amekieleza kitendo hicho kuwa ni cha kikatili na kisichovumilika na kuongeza kuwa amesikitishwa na kitendo hicho na kumpa pole Padri Mwang’amba na kumuomba Mwenzi Mungu ampe nafuu haraka apone ili endelee kuitumikia jamii.
Akizungumza na waumini wa kanisa hilo nje ya Wodi alipolazwa Padri huyo, Dk. Shein aliwataka waumini hao kuwa na subira wakati Serikali ikichukua hatua kukabiliana na kitendo hicho.
“Ni jambo la kusikitisha kumfikisha binadamu wenzako katika hali kama hii ya majonzi. Hakuna anayetaka haya. Tuwe wastahamilivu Serikali tunachukua hatua,”aliwaambia waumini hao.  
Akizungumzia hali yake, Padri Mwang’amba alimueleza Rais kuwa ni nzuri na anaona vizuri lakini anatarajia kupata nafuu zaidi baada ya uvimbe kupungua sehemu za machoni.
“Hali yangu ni nzuri lakini natarajia uvimbe ukipungua nitaona vizuri zaidi,” alisema Padri Mwang’amba na kuongeza kuwa ilikuwa ni bahati kwake hakuathirika sana. 
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mohamed Saleh Jidawi akiwa amefuatana na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dk Jamala Adam Taibu amesema alipofikishwa katika hospitali hiyo Padri Mwang’amba alipatiwa huduma zote muhimu za matibabu zinazostahiki. 
Kuhusu majeraha aliyopata, Dk Jidawi alieleza kuwa kwa ujumla asilimia 30 ya mwili wa Padri Mwang’amba umeathirika na kidogo sehemu za macho.
Kwa upande wa Wakristo kisiwani Zanzibar wamesikitishwa na tukio la kumwagiwa kwa tindikali kwa Padri Mwang'amba wakati akitoka katika duka la intaneti la Sunshine la Mlandege.
Baadhi ya wakristo waliohojiwa ikiwemo wa kanisa la Machuwi ambalo Mwang'amba alifanya kazi kwa miaka mingi, walisema sasa maisha ya jamii ya wakristo Zanzibar yapo mashakani.
Modesta Nkala wa kijiji cha Kitumba Wilaya ya kati ambaye husali katika kanisa la Machuwi alisema amesikitishwa na tukio hilo ambalo walengwa wake wakuu wanaonekana watu wa jamii ya Wakristo.
“Tuliposikia taarifa za tukio hili tulikusanyika na kulia sana kwa sababu Padri Mwang'amba  tulifanya kazi naye kwa miaka mingi katika kanisa la Machuwi wilaya ya kati Unguja akiwa mtumishi wa mungu muaminifu,” alisema.
Padri Mwanga'mba alihamishiwa katika kituo cha kulea na kutunza vijana kilichopo Cheju ambacho kinaendeshwa na kanisa Katoliki mjini hapa.
Muumini mwingine wa kanisa la Machuwi, Bulabo Pascal alisema baadhi ya watu wanaonekana kuelekeza visasi vyao kwa Wakristo bila ya sababu za msingi ikiwa ni hujuma na ukatili usiokubalika.
“Tunaiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufutilia kwa karibu matukio ya vitendo vya hujuma vya watu kumwagiwa tindikali,”alisema.
Mpiga picha wa kujitegemea Martin Kabemba alisema matukio ya watu kumwagiwa tindikali hivi sasa yanaonekana ya kawaida  huku jambo la kushangaza hakuna mtu anayekamatwa.
Kiongozi wa kanisa katoliki Zanzibar, Askofu Augustino Shao alisema amesikitishwa na tukio hilo ambalo linaonesha vitisho kwa Wakristo waliopo Zanzibar.
Shao ambaye yupo nje ya Zanzibar alisema tukio la kumwagiwa kwa tindikali kwa Padri Mwang'amba lengo lake ni kudhoofisha juhudi za Wakristo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Mapema Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alielezea masikitiko yake kwa matukio ya vitendo vya watu kushambuliwa kwa tindikali ambayo vimeelekezwa kwa jamii moja tu na watu wenye itikadi moja.
Alisema lengo la Serikali ya umoja wa kitaifa ni kujenga mazingira ya  utulivu wa kisiasa, na vitendo vya vurugu na watu kumwagiwa tindikali vinakwenda kinyume na malengo hayo.
Padri wa kanisa katoliki Minara miwili liliopo eneo la Mji Mkongwe, Asenga Thomas ambaye alikuwa akishughulikia safari ya Padri Mwang’amba kwenda hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema amejeruhiwa vibaya sehemu za uso na kulazimikwa kusafirishwa.
Aidha alisema kanisa linatarajia kutoa tamko rasmi kuhusiana na tukio la kumwagiwa kwa tindikali kwa padri Mwang’amba.
Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Yussuf Ilembo alisema hadi sasa Jeshi la Polisi halijakamata mtu yeyote kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi zaidi unaendelea.