Kwa ufupi
Huyu mwandishi alifika ofisini akanieleza shida
yake na nimempa haya mabati kama mwananchi wa kawaida wa Kisarawe na
mkazi wa mkoa wangu huu, si kama mwanahabari.
Kibaha. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza
amemsaidia mwandishi wa habari wa Kampuni ya The Guardian, Amri
Lugungulo mabati 100 yenye thamani ya Sh1.5 milioni kwa ajili ya
kukamilisha ujenzi wa nyumba na kuweza kuondokana na adha ya nyumba za
kupanga.
Mwandishi huyo alikabidhiwa rasmi mabati hayo jana
katika ofisi ya mkuu huyo wa mkoa na kushuhudiwa na wanahabari wa
vyombo mbalimbali nchini. Mahiza pia amempa fedha taslimu Sh100,000 kwa
ajili ya kusafirishia mabati hayo kwenda wilayani Kisarawe anakojenga
nyumba yake mwandishi huyo.
“Huyu mwandishi alifika ofisini akanieleza shida
yake na nimempa haya mabati kama mwananchi wa kawaida wa Kisarawe na
mkazi wa mkoa wangu huu, si kama mwanahabari, maana mimi kama mkuu wa
mkoa wapo watu ambao huja kunieleza shida zao na kama nikiona upo
umuhimu zaidi ya kumsaidia nasaidia kulingana na hitaji la mtu baada ya
kuthibitisha ukweli wa shida yake,”alisema Mahiza.
Lugungulo ameshukuru kwa msaada huo, alisema
umemfikia kwa wakati kutokana na uhitaji aliokuwa nao ili aweze kuezeka
nyumba yake anayoijenga huko Tabata na aondokane na kero za nyumba za
kupanga anayoishi kwa zaidi ya miaka kadhaa sasa huko Buguruni, Dar
Salaam. Lugungulo amefanya kazi katika vyombo vya habari ikiwamo Daily
news,Uhuru na Mzalendo,Nipashe na sasa The GuardianSource: Mwananchi