Kwa ufupi
Mansour aliwahi kuwa waziri asiyekuwa na Wizara
ya Maalumu katika utawala wa awamu ya saba ya Dk Ali Mohammed Shein,
pia aliwahi kuwa naibu waziri wa Wizara ya Kilimo kabla ya kuwa Waziri
wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi katika utawala wa Rais Mstaafu Amani
Abeid Karume.
Hii si mara ya kwanza kwa CCM kufukuza wanachama wake wa upande wa Zanzibar wanaoonekana kuwa na misimamo tofauti.
Miaka ya nyuma iliwafukuza aliyekuwa
Waziri Kiongozi Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu
wa Chama cha Wananchi (CUF).
Wiki iliyopita Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kilibariki rasmi kufukuzwa uanachama kwa mwakilishi wake wa Jimbo la
Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid kwa kile kilichoitwa usaliti kwa
chama hicho kwa kuunga mkono Muungano wa mkataba.
Kufukuzwa kwa Mansour, kunakuja baada ya CCM
Taifa kupokea uamuzi kutoka chama hicho Mkoa wa Mjini Magharibi,
Zanzibar ambapo mwanachama wake huyo anatoka ya kutaka afukuzwe kwa
madai ya kupinga sera ya Muungano wa Serikali mbili.
Wakati CCM ikimfukuza Mansour, imetengua uamuzi wa uongozi wa chama hicho Mkoa wa Kagera wa kuwafukuza madiwani wake wanane.
Wanane hao walifukuzwa na CCM Mkoa kufuatia
kukaidi agizo la mwenyekiti wao, Constancia Buhiye kuonekana kuhusika
katika mgogoro baina ya Meya Dk Anatory Amani na Mbunge wa Bukoba Mjini,
Balozi Khamis Kagasheki.
Mansour aliwahi kuwa waziri asiyekuwa na Wizara ya
Maalumu katika utawala wa awamu ya saba ya Dk Ali Mohammed Shein, pia
aliwahi kuwa naibu waziri wa Wizara ya Kilimo kabla ya kuwa Waziri wa
Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi katika utawala wa Rais Mstaafu Amani
Abeid Karume.
Kwa muda mrefu, mwanasiasa huyo ameonekana
kuchukizwa na kile anachokiita matatizo ya Muungano anayodai kuwa
yanaikandamiza Zanzibar, msimamo unaoungwa mkono na Wazanzibari walio
wengi wakiwemo baadhi ya wana- CCM, ingawa hakuna aliyekuwa tayari
kusimama wazi kueleza msimamo wake hadharani kama alivyofanya.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa CCM kufukuza wanachama wake wa upande wa Zanzibar wanaoonekana kuwa na misimamo tofauti.
Chama hicho kimewahi kufanya hivyo miaka ya nyuma
kwao Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Waziri Kiongozi, pamoja na
aliyekuwa Rais wa nane wa Zanzibar na makamu wa rais wa Jamhuri ya
Muungano, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi.
Vilevile, CCM imewahi kuwafukuza aliyewahi kuwa
Naibu Waziri wa Mambo ya ndani, Hamad Rashid Mohamed, Alhaji Pandu,
Machano Khamis Ally, Shabani Khamis Mloo, Hatibu Khasan na Sudi Yusuph
Mgeni.
Wakati ikiwafukuza wazanzibar, CCM haijawahi
kuwafukuza uanachama kiongozi au wanachama wake upande wa bara
wanaoonekana kutofautiana na msimamo wa chama.
Hali hii ya kuwa wepesi kufukuza uanachama wanachama na viongozi
wake wa Zanzibar, na kupata kigugumizi kwa wa upande wa bara imezua
hisia na mitazamo tofauti kwa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini
ambao waliopata fursa ya kuzungumzia hali hii wanasema, CCM inawaonea
wazanzibar.
Mtazamo wao
Wanahoji iweje CCM imekuwa na wepesi kuchukua
hatua kali, dhidi ya wanachama wake kutoka visiwani huku ikiwawia vigumu
kufanya vivyo hivyo kwa wanachama wake wa Tanzania Bara.
Mfano wa wazi na mwepesi ni ule wa madiwani wa
Mkoa wa Kagera ambao chama kupitia vikao vyake vya juu , NEC na CC
vilibatilisha uamuzi wa kuwafukuza licha ya uongozi wa CCM mkoa
kutangaza kuwafukuza uanachama na nyadhifa zao zote ndani ya chama.
Je, nini mtazamo wa Wazanzibari kuhusiana na hali
hii, Said Miraji ni mwenyekiti wa Chama cha ADC, anasema hali hiyo ni
ushahidi tosha kuwa CCM siyo chama cha Wazanzibari na kuwa hakioni shida
kumchukulia hatua kiongozi wa ngazi yoyote upande wa Zanzibar tofauti
na wale wa upande wa bara.Anasema Miraji kuwa yanayoonekana ndani ya
chama hicho ni kiashiria kuwa hakuna kuvumiliana ndani ya CCM hasa
upande wa Zanzibar na kwamba Wazanzibari hawatakiwi kupaza sauti zao kwa
yale wanayoyaamini.
“Hii inaashiria kuwa CCM siyo ya Wazanzibari,
jambo lolote dogo linalofanywa nao linafanywa kuwa kubwa, lakini jambo
hilo hilo likifanywa mwanachama wa bara linaonekana kuwa dogo na hakuna
hatua yoyote anayochukuliwa mhusika,” anasema nna kuongeza:
“Siwasemei, lakini wenyewe waone na wajiulize,
iweje wajumbe wa CC na NEC, wameshindwa kubariki uamuzi wa Mkoa wa
Kagera wa kuwafukuza madiwani, lakini suala la Mansour mwakilishi wa
jimbo na mtu mwenye historia kubwa sana katika visiwa hivi, anaonekana
hana thamani na anafukuzwa…hili wenyewe wana CCM wanapaswa
kulitafakari.”
Miraji anasema mitazamo tofauti ya mawazo
miongoni mwa wanachama ni kukuza ustawi wa demokrasia ndani ya taasisi
na kwamba ni vyema kuwe na utamaduni wa kuvumiliana, kuthamini mawazo ya
kila mtu hata kama hayaendani na matakwa na msimamo wa taasisi husika.
Miraji pia anaongeza kuwa kuzuia watu kutoa maoni
yao ya kile wanachokiamini au kukiwaza ni kuua demokrasia, na kwa
kawaida demokrasia ni lazima ianze ndani ya chama…CCM inapaswa ielewe
kuwa uhuru wa mawazo sio baina ya chama na chama isipokuwa ni kwa kila
mtu mmoja mmoja, popote pale alipo.
“Na hili sio jambo jipya maana hata marekani
mambo ya namna hii yapo, chama kinakuwa na msimamo wake lakini kiongozi
anasimama na kuunga mkono sera au mtazamo wa chama kingine kutokana na
utashi na mawazo yake….na hili likitokea hakuna kufukuzana, kwanini haya
yanatokea kwetu”
Kuogopana
Ambari Khamis, makamu mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi
Zanzibar anasema kinachoonekana ni kuwa kuna kuogopana kati ya CCM Bara
na CCM Zanzibar.
“CCM Taifa inaiogopa kamati maalum ya CCM Zanzibar, haiwezekani
kuweza kumfukuza mansour ikaogopa kumfukuza diwani…CCM ina hofu,
ukiwakatalia nao watawakatalia mambo kadhaa” na ndicho.
Ambari anasema kutokana na kuogopana huko, CCM
upande wa Zanzibar ikiamua jambo lake hata kama lina madhara kiasi gani
kwa chama, CCM bara inalazimika kulipitisha, na inasababishwa na ukweli
kuwa yapo mambo ambayo Bara inahitaji kuyafanya kuwa msimamo wa
watanzania na ukweli ni kuwa watanzania bara ndio wanaong’ang’ania zaidi
Muungano.
Hata hivyo, anasema kufukuzwa kwa Mansoor
hakumpunguzii kitu bali kunamzidishia heshima yake kwa Wazanzibari
kutokana na kuonekana dhahiri kusimamia kudai haki za Zanzibar za uchumi
na kupata mamlaka kamili.
Kauli ya Mansour Himid
Kwa upande wake, Mansour anaeleza kuwa hakuna jambo baya alilofanya na lililostahili kufukuzwa ndani ya chama hicho.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya
Kikwete aliwahakikishia Watanzania wote, narudia wote, uhuru wa kutoa
maoni kwa upeo wao, na waseme wanachotaka kukisema, Mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba vile vile naye akarejea yale yale
aliyosema Kikwete.
Vilevile, Dk Ali Mohamed Shein aliwahakikishia
Wazanzibari wote sio kwa tabaka wala chama, kwamba wanao uhuru wa kutoa
maoni yao” anasema.
Anaongeza mbali na kauli za viongozi hao katiba
zote mbili, ile ya Muungano na ya Zanzibar zinawahakikishia uhuru na
vile vile sheria nayo inawahakikishia uhuru wananchi wake wote
Kwa mtizamo wangu mimi, wakati tunaelekea kwenye
mchakatoi huu, huwezi kuwawekea masharti ya aina yoyote… nimemsikia Nape
anasema msimamo wa Chama ni serikali mbili, ni jambo la ajabu sana,
inabidi tujiulize, tujiulize sisi watanzania hatuna uhuru…kwa maana sasa
tunaambiwa watu wazima wa Zanzibar, kila anayeenda pale ni zidumu fikra
za mwenyekiti, ni serikali mbili ondoka…. uko wapi utu na heshima na
uhuru wetu,. Hatuwezi kuzuiwa kwa misingi hiyo” anasema.
Mansour anaongeza kuwa hata aliyekuwa makamu
mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa aliweka bayana pale alipobainisha kuwa,
licha ya sera za chama kuwa ni serikali mbili, lakini ni huru kila
mwanachama kutoa maoni anavyoona yeye ni sawa.
“Hili linaloendelea hivi sasa, tafsiri yangu naona
wapo watu hasa hapa Zanzibar ambao wana fikra za kidikteta na mawazo
mgando, wanataka kutuadhibu sisi tunaotofautiana na mawazo yao… mimi
sijaanza kusema leo, kuhusu msimamo wangu, narejea, mfumo huu wa
serikali mbili sikubaliani nao, siwezi kubadili msimamo huu maana
nitapoteza utu wangu na jamii itanisuta,” anasema.
source: Mwananchi
source: Mwananchi