Thursday 5 September 2013

Sophia Simba matatani UWT


Sophia Simba 
Na Mwinyi Sadallah  (email the author)

Posted  Jumatano,Septemba4  2013  saa 20:8 PM
Kwa ufupi
Tuhuma za ufisadi dhidi ya Salama na uteuzi wa kuendelea na wadhifa wake, kumezua sokomoko ndani ya UWT.


Zanzibar. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba, ameshutumiwa kwa kitendo chake cha kumteua Salama Aboud Talib kwenye nafasi ya Naibu Katibu Mkuu, wakati anatuhumiwa kwa ufisadi wa mali za jumuiya.
Taarifa za ndani ya jumuiya zilidai kuwa uteuzi wa Salama, anayeshika wadhifa huo kwa upande wa Zanzibar, umekiuka azimio la Kamati ya Utekelezaji lililotaka achunguzwe kutokana na tuhuma za ufisadi wa mali za UWT upande wa visiwani.
Salama kabla ya uteuzi huo wa sasa, alikuwa akishika wadhifa huo lakini katika awamu hiyo ya uongozi wake kulikuwa na tuhuma za ufisadi wa mali za jumuiya na kwamba Mwenyekiti Sophia Simba amemteua wakati akiwa bado anachunguzwa.
Malalamiko hayo yamejitokeza baada ya kukamilika kwa Baraza Kuu la UWT Taifa lililokutana katika ukumbi wa hoteli ya Dodoma, Agosti 26 mwaka huu wakiwa na ajenda ya kumwidhinisha Katibu Mkuu na manaibu wake Bara na Zanzibar.
Wakizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kuhifadhiwa majina yao, baadhi ya wajumbe wa baraza hilo walidai Salama hakustahili kurejeshwa kwenye nafasi hiyo, kwa kuwa tume ya uchunguzi dhidi yake bado haijakamilisha kazi yake.
Mmoja wa wajumbe alidai azimio la Kamati ya Utekelezaji iliyokutana mwezi uliopita, iliundwa tume ya kuchunguza tuhuma za ufisadi za mali za UWT Zanzibar dhidi ya Salama.
Alisema tume hiyo inawajumuisha Dk Aisha Kigoda, Zarina Madabida, Zainab Mwamidi na Mwanaidi Kassim ambao miongoni mwao walitakiwa kuchagua mwenyekiti wa tume hiyo ili kukamilisha kazi ya uchunguzi na kuwasilisha ripoti.
“Tulipokwenda kwenye Baraza Kuu tulikuwa na ajenda ya kumthibitisha Katibu Mkuu, Amina Makilagi na Naibu wake Grace Kiwele cha kushangaza mwenyekiti amepitisha na kumthibitisha Salama Aboud Talib, kinyume na maazimio ya kamati ya utekelezaji,”alisema mjumbe mmoja ambaye ni kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Sophia Simba alithibitisha kuteuliwa kwa Salama kushika wadhifa huo na kueleza kuwa umefanyika kwa kuzingatia utendaji na uchapakazi wake wa mhusika.
“Salama ataendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, uwezo wake ni mkubwa kiutendaji, tuhuma kama zipo ni kwa UWT kama jumuiya na si kwake tu,”alisisitiza mwenyekiti huyo.
Sophia alisema kufanyika kwa uteuzi huo hakusitishi mambo mengine kutoendelea ikiwamo tuhuma zinazolalamikiwa kufanyiwa uchunguzi.
Inaelezwa sababu ya kuundwa kwa tume ni baada ya kujitokeza tuhuma kuhusu mali za UWT, zikiwamo nyumba za kuoka mikate huko Unguja na Pemba na vitegauchumi vingine kutoinufaisha jumuiya hiyo.


“Mwenyekiti anaiburuta jumuiya, tumejipanga na hatutakubali aendeshe taasisi hii kama kampuni yake, mali za chama chetu zinatuuma. Tunataka tume ije na majibu ya tuhuma hizi,” alisema mjumbe mmoja kutoka mikoa ya Kanda ya Kati.
Kwa upande wake, Salama alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alikiri kuteuliwa tena katika wadhifa huo wa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na kwamba suala la kuundwa kwa tume ili kuchunguza mali, yeye halifahamu na kutaka waulizwe wajumbe wanaotoa shutuma hizo.
Makamu Mwenyekiti wa UWT kwa upande wa Zanzibar, Asha Bakari Makame alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na sakata hilo alisema hayuko tayari kuzungumzia jambo lolote la UWT.
”Sitaki kuzungumza lolote, nenda kaandike hivyohivyo kama ninavyokwambia sitaki, sitaki, sitaki,”alijibu Makamu huyo wa UWT.

source: Mwananchi