Saturday, 14 September 2013

Serikali yaingilia kati Mama Maria kunyang’anywa viwanja

HATIMAYE Serikali imeingilia kati suala la mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere kunyang’anywa viwanja vitatu katika eneo la Msasani Dar es Salaam. Viwanja hivyo vipo maeneo tofauti ambapo kimoja kipo Mikocheni ‘B’ Plot 402 Block C na kingine kipo Msasani Beach Namba 778 ambacho kinadaiwa kugawanywa kwa watu wawili.


Habari za uhakika zilizopatikana jana mchana kutoka Msasani kwa Mwalimu Nyerere, zinasema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadik Meck Sadik alikutana na Mama Maria kujua ukweli wa mgogoro huo.

“Huwezi amini Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amefika hapa saa 9 mchana na moja kwa moja amekwenda ofisini kwa Mama Maria kuzungumza naye,

“Sijawahi kumuona anakuja hapa katika siku za karibuni, najua baada ya MTANZANIA kuandika ile habari ya mgogoro wa kiwanja, imemleta hapa,” kilisema chanzo chetu.

Habari zaidi zinasema RC Sadik katika mazungumzo yake na Mama Maria, alitaka kujua ukweli juu ya umiliki wa viwanja hivyo na kuona nyaraka halali.

“Moja ya suala kubwa lililotawala mazungumzo ya RC Sadik na Mama Maria, lilikuwa kujua mwanae John Nyerere kweli alikuwa mmiliki halali.

“Mama Maria ametoa nyaraka zote ambazo zinaonyesha John ndiye mmiliki halali wa viwanja hivi, jambo hili limemshutua RC Sadik,

Chanzo chetu, kiliiambia MTANZANIA kuwa RC Sadik ameahidi kushughulikia suala hilo mara moja katika siku chache zijazo,” kilisema chanzo chetu.

Habari za awali zilisema Kamishna wa Ardhi na maofisa ardhi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi wanajiandaa kutembelea viwanja hivyo.

Hatua ya maofisa kuamua kutembelea viwanja hivyo imefikiwa baada ya juzi watendaji hao kufanya upekuzi wa nyaraka mbalimbali wizarani hapo kutafuta ukweli.
SOURCE: MTANZANIA