Tuesday 17 September 2013

Sumaye 'afyatuka tena

14th September 2013
 Asema tofauti viwango vya elimu italiangamiza taifa
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameonya kuwa taifa linakabiliwa na tabaka litakaloibua mgawanyiko miongoni mwa jamii, kutokana na uwiano wa viwango usio sawa kwa shule zilizopo nchini.

Kwa siku za hivi karibuni, Sumaye aliyewahi kuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa, amekuwa mstari wa mbele kukosoa mambo kadhaa yanayoiathiri jamii.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa, wanaamini kwamba hatua hiyo ina mwelekeo wa kujijengea mazingira ya kugombea urais mwaka 2015, lakini binafsi hajawahi kutamka hivyo.

Amesema, ipo haja ya kuwapo jitihada za haraka kwa serikali kuchukua hatua ya kurekebisha hali hiyo na kuifanya jamii iendelee kuwa salama.

Alikuwa akizungumza jana kwenye mahafali ya tano ya darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya New Ero Montessori jijini Dar es salaam.

Sumaye, alisema imefikia wakati kwa serikali kuweka uwiano wa viwango ulio sawa ili watu masikini, pamoja na mambo mengine, wamudu gharama ya kuwasomesha watoto wao.

Alisema sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji kazi kubwa kuzirekebisha kwa maslahi ya nchi na watu wake.

Sumaye, alisema kuna umuhimu kwa wadau wa elimu wakiwamo wazazi, serikali na sekta binafsi, kuangalia njia mbadala ya kuokoa elimu badala ya kuchukua hatua kama za kupunguza viwango vya ufaulu hivyo kuwadidimiza Watanzania.
"Nchi yenye matabaka ya kielimu ni hatari, lazima serikali irekebishe viwango vya upatikanaji wa elimu ili watoto wapate elimu sawa na ubora unaokubalika," alisema Sumaye.

Hata hivyo, alipinga hatua iliyochukuliwa na serikali kupunguza ufaulu kwa wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu nchini.

Alisema hali hiyo inaweza kusababisha hatari kwa watakaofanikiwa kujiunga na masomo, kukosa sifa na kusababisha nchi kutopata wataalamu wanaotakiwa.

"Nchi yenye watu wenye elimu ya kutosha inakuwa na ushindani mzuri na nchi nyingine kimaendeleo, lakini kwa hatua hii, vijana wetu hawataweza kuweka ushindani huo na kusababisha taifa liwe la watu wajinga," alisema.

Aliipongeza shule hiyo kwa jitihada zake za kutoa elimu bora kiasi ambacho wazazi wenye watoto wao wanaamini kuwa hapo ni sehemu nzuri kwa utoaji elimu.

Aliwasihi wanafunzi wanaomaliza kuendeleza juhudi ya kusoma kwa kuwa huo ndio mwanzo wa safari ndefu ya `kusaka’ elimu kwa ajili ya manufaa ya nchi na jamii kwa ujumla.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Daniel Desire, alisema jumla ya wanafunzi 34 wamefanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka huu.

Alisema, shule hiyo uliyoanza mwaka 1999 imekuwa katika mchakato kubwa wa uboreshaji wa mazingira ya ufundishaji pamoja na kusomea wanafunzi, ikiwamo kuongeza madarasa, nyumba za walimu, kituo cha afya na ujenzi wa shule ya sekondari eneo la Bagamoyo.
 
CHANZO: NIPASHE