Saturday, 14 September 2013

Tafakuri Jadidi: Kwa kasi hii, Kikwete atavunja rekodi ya Obasanjo!

Na. Johnson Mbwambo
Toleo la 315 11 Sep 2013
KATIKA toleo lililopita nilijadili, miongoni mwa mambo mengine, hatari ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki endapo Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi zitaendelea na tabia ya sasa ya kuitenga Tanzania – tabia ambayo niliihusisha na kuharibika, kwa hivi karibuni, kwa mahusiano kati ya Rais Kagame na Rais Kikwete.


Tafakauri yangu hiyo ilikaribisha sms na emails nyingi kutoka kwa wasomaji wangu, lakini iliyonifikirisha zaidi ni ile ya msomaji wangu mwenye simu Na.  0713 228000 ambaye alihalalisha Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kukutana zenyewe bila Tanzania kuharakisha mipango yao ya maendeleo.  “Ndugu yangu Mbwambo, wa kulaumu ni Kikwete mwenyewe.

 Nadhani wenzake walishamuona hana maono ya mbali. Wakati wenzake wanakutana pamoja kuweka mikakati ya kikanda, yeye yuko nje ya nchi (Austria) akitembea.”  Nasema ujumbe huo ulinifikirisha upya kwa kuwa huko nyuma nilipata kujadili katika safu hii tabia hii ya Rais Kikwete kuzifurahia sana safari za nje; badala ya kukita juhudi zake katika kuisaidia nchi kujenga misingi ya kujitegemea.  Sina hakika mpaka sasa safari zake za nje zimefikia ngapi na zimegharimu kiasi gani cha mapesa ya walipakodi (hata jamiiforums naona sasa imechoka kuendelea kuorodhesha idadi yake), lakini nikumbushe tu kwamba kabla ya kwenda Austria alikuwa Malawi kwenye mkutano wa SADC na baada ya kurejea Austria alikwenda Kampala.

 Kwa ufupi, mwezi haushi bila Rais Kikwete kusafiri nje. Ikizingatiwa kuwa safari hizi zinachosha (jet-lag), na hasa zile za masafa marefu za kukatisha bahari, huwa najiuliuza kama arudipo anakuwa na nguvu za kutosha kupitia kwa makini mafaili nyeti ofisini kwake, na hata kufuatilia masuala nyeti kadha wa kadha.  Nayasema haya yote nikitambua wazi umuhimu wa kiongozi wa nchi kusafiri nje – kuvutia wawekezaji, kuhudhuria mikutano muhimu ya nje nk.

 Nayasema haya nikitambua pia kwamba Kikwete si kiongozi wa kwanza duniani kufanya safari nyingi za nje.  Kwa hakika, kumbukumbu zinatuonyesha kwamba tabia hii ya wakuu wa nchi duniani na viongozi wengine kusafiri nje kwa safari za kiserikali ilianza katika karne ya 20. Kinara wa kwanza alikuwa Rais Woodrow wa Marekani ambaye alisafiri kwa meli na kukaa Ulaya kwa miezi saba mara baada ya vita vya kwanza vya dunia kumalizika.  Rekodi zinaonyesha kwamba kiongozi barani Ulaya anayeshikilia nafasi ya kwanza kwa kusafiri sana duniani ni Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza ambaye katika miaka yake 61 ya umalia amefanya ziara za nje za kiserikali 261. 

Viongozi wengine katika miaka ya karibuni walioingia katika orodha ya waliosafiri sana safari za kiserikali ni pamoja na Hillary Clinton ambaye katika miaka yake minne ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alisafiri katika nchi 100, na hivyo kuvunja rekodi ya aliyemtangulia, Madelaine Albright, aliyesafiri katika nchi 96.

 Tusisahau kuwa mifano yote hiyo ni ya mataifa tajiri ambayo angalau yana fedha za kutosha kuhalalisha safari hizo za nje; lakini vipi kwa bara masikini la Afrika? Hakika, kope hupepesa anapotokea kiongozi wa Kiafrika kushabikia sana safari hizo za nje zinazogharimiwa kwa pesa za walipakodi!  Kama nilivyosema mwanzo, sina hakika kuwa Rais wetu Kikwete amefikisha idadi ya safari ngapi za nje, na pia sina takwimu za wenzake wa Afrika Mashariki - kina Kagame, Museveni, Nkurunzinza (achana na Uhuru ambaye kaupata urais majuzi tu) ili kulinganisha;  maana takwimu katika Afrika ni tatizo jingine kubwa linalotusumbua. 

Hata hivyo, angalau hakuna ubishi kwamba katika Afrika rekodi inashikiliwa na mtawala wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo. Ni maoni yangu kwamba kama Kikwete hatapunguza kasi yake ya sasa ya kusafiri nje, anaweza kuingia kwenye ‘ligi aliyocheza’ Obasanjo na anayoendelea kuicheza hata sasa ingawa ameshaachia urais!

  Rekodi zinaonyesha kuwa hadi Mei 29, 2007 wakati anakabidhi urais kwa rais mpya wa Nigeria, Obasanjo alikuwa amefanya safari za nje ya nchi hiyo zinazofikia 400! Hebu fikiria; safari 400 zinazolipiwa kwa fedha za walipakodi kwa kipindi kifupi tu cha utawala wake wa miaka minane (1999 -2007)!  Lakini huyo ndiye Obasanjo.

 Unaweza kusema kuwa ana ‘ugonjwa’ wa kupenda kusafiri nje ya nchi; maana tabia hiyo anaiendeleza hata sasa ingawa sio tena mkuu wa nchi.  Kuna utani, hivi sasa, barani Afrika, kwamba kama una ka-semina au ka-mkutano kako sehemu yoyote ile Afrika na unataka Obasanjo akafungue au akafunge kama mgeni rasmi, unachotakiwa kufanya ni kumtumia tu tiketi ya ndege na kumpangia hoteli nzuri ya kukaa – atakubali kuja!  Vyovyote vile; Obasanjo huwajibu wanaomshutumu kuwa alipenda mno kusafiri nje ya nchi alipokuwa rais kwamba, kama si safari zake hizo Nigeria isingekuwa ilivyo leo.

 Yaani, anahusisha kukua kwa uchumi wa Nigeria na safari zake hizo!  Sidhani kama msomaji wangu atapata taabu kukumbuka kuwa hoja hiyo hiyo ya Obasanjo ndiyo inayotumiwa na Rais wetu Kikwete kuwajibu kina sisi tunaolalamika kuwa anapenda sana kusafiri nje kuomba misaada badala ya kutumia muda wake mwingi hapa nchini kutujengea uwezo na utamaduni wa kujitegemea.  Na hiyo inanikumbusha moja ya kauli za Kikwete zenye utata (ukakasi) aliyoitoa kwenye mkutano wa kampeni ya urais, Oktoba 2010, mjini Mbeya. Kauli hiyo ni ile aliyoitoa kuwajibu wanaomshutumu kwamba anatumia mapesa mengi ya walipa kodi kufanya ziara nyingi za nje zisizo na ulazima.  Alisema maneno mengi kwenye mkutano huo kuhalalisha ziara hizo, lakini yaliyoniacha hoi ni haya: “Mimi nakwenda kule (Ulaya na Marekani) kuhemea. Nikirudi, narudi na vibaba.” 

Kama nilivyoandika kwenye safu hii wakati huo (2010), ningemwelewa Kikwete kama angeueleza umati ule kwa hali ya kusikitisha kwamba sisi Watanzania tunamwangusha kwa sababu hatuchapi kazi vya kutosha; kiasi cha kufikia hatua ya kujitegemea, na hivyo tunamfanya ajidhalilishe kwa kwenda Ulaya na Marekani kuombaomba hata mambo ambayo tungeyamudu wenyewe kujitafutia.  Ningemwelewa Kikwete kama angeielezea hali ile kwa uchungu na kwa masikitiko, na hata kutisha kwamba hatakubali tena kwenda Ulaya na Marekani kuombaomba mambo ambayo sisi wenyewe tuna uwezo nayo.  Lakini sivyo alivyofanya kwenye hotuba hiyo ya Mbeya, au hata sasa anapokosolewa kuhusu ziara hizo za nje. Hoja zake za utetezi anazitoa katika namna inayoonyesha kuwa anazifurahia ziara hizo za nje za kuomba misaada.

 Na hiyo ndiyo inayonitia shaka kwamba labda naye ana kale ‘ka-gonjwa’ ka kupenda kusafiri nje kanakomsumbua Obasanjo hata sasa miaka sita baada ya kuuacha urais! Kama naye ana ‘ka-gonjwa’ hako, basi, tutaendelea kumwona akisafiri sana Ulaya na Marekani hata baada ya kuuacha urais mwaka 2015!  Nikumbushe tena kwamba safari hizo za kuomba misaada na mikopo nje ya nchi zina faida, lakini sio faida kubwa kulinganisha na ile ya kuijengea nchi uwezo na utamaduni wa kujitegemea yenyewe. Tujiulize, je; kuna nchi dunia iliyopata kuendelea na kuondokana na umasikini kwa kutegemea misaada ya nje ya nchi? 

Ndugu zangu, kwa sasa, tunaweza kuikejeli siasa ya Ujamaa ya Mwalimu Nyerere, lakini ni upofu na ujinga kuitelekeza dhana yake ya Kujitegemea. Tutalia na kusaga meno siku Wazungu watakapotuchoka kabisa Waafrika.  Na siku hizo za Wazungu kutuchoka kabisa hazipo mbali. Juzi nilikuwa naangalia televisheni ya BBC wakati mtangazaji akiwahoji Wajerumani, mjini Berlin, kuhusu kupanda kwa gharama za maisha.

Wengi walizungumza kwa jazba wakiilaumu serikali yao kwa kutoa mapesa mengi ya walipakodi kusaidia kuinua uchumi wa Ugiriki badala ya kuyabakisha nyumbani yatatue matatizo yao mengi.  Sasa, kama Wajerumani wanachukizwa na hatua ya serikali yao kuzisaidia Ugiriki au Hispania ambazo ni majirani na ni Wazungu wenzao, vipi litakapokuja suala la kusaidia nchi za Kiafrika? Na hisia hizo za Wajerumani ndizo pia hisia za nchi nyingine za Ulaya. 

Kwa mtazamo wangu, hisia hizo za sasa za Wazungu ni maandiko ukutani kwa watawala wetu…. ni kengele ya uamsho kwa watawala wetu. Na uamsho wenyewe ni kwamba zama za Waafrika kutegemea misaada ya Wazungu zimepita.  Tena siku hizi mtawala hahitaji kusafiri na ndege kuvuka bahari ya Atlantic kuhudhuria mkutano wa kuomba msaada; maana siku hizi kuna utaalamu wa teknolojia ya kisasa ya kuendesha mkutano na mtu bila kuonana ana kwa ana - wenyewe wanaiita teleconference.  Sasa, kama kuna utaalamu huo, na ikizingatiwa kuwa ziara hizo za kuomba misaada zimepitwa na wakati; utitiri huu wa safari za nje kwa watawala wetu wa nini? 

Tafakari. -
 Source: http://www.raiamwema.co.tz