Kuna watu huwa wanafikiria wenzao walio ughaibuni - Ulaya, Marekani
au hata Mashariki ya Kati - ni wachawi. Halafu kuna wengine walikuwa
wakisema kuwa labda waliotoka Tanzania na sehemu nyingine za Afrika
kwenda huko na kupata maendeleo, walibebwa au ni kubarikiwa tu.
Sawa, kubarikiwa kupo lakini hata Mungu alimwambia mwanadamu ajenge
nyumba imara, aweke mlango na usiku au wakati hayupo aufunge ndipo naye
ataweka mkono wake kumsaidia.
Kwa hiyo dhana iliyozoeleka kwamba
watu wanabebwa au wanaelea tu kwa nguvu ya wakubwa si sahihi, na
utashangaa msomaji wangu kuona wapo wanaojitesa mno hadi wakafanikiwa.
Njia
mojawapo ya kufikia hatua hiyo ni kujijengea mazoea ya kutafuta,
kupekua na kusoma kwa bidii badala ya kuketi na kufikiria mtu mwingine
atakuletea ngekewa hiyo. Kuna watu walikuja Ulaya kwa miezi michache ya
kozi fupi, na baada ya kufika hawakulala ‘hadi kikaeleweka’.
Waliangalia
taratibu zinataka nini, wakafungua mitandao na kutazama fursa zilizopo
kama masomo au nafasi za kazi na kuanza kuomba. Hadi sasa wapo
wanaoendelea kila siku kufungua macho na masikio kuhusu nafasi na
zinapojitokeza wanaharakisha kuziomba wakati wakiendelea na kazi.
Lakini
kwa hili naomba niwe wazi. Kinachosaidia zaidi wengi kupata nafasi hizo
ni kasi ya maendeleo pamoja na kuweza kurambaza haraka mtandao, lakini
na wenyewe wanavyojitahidi kukimbia na kasi yake hiyo.
Kwa mfano,
wakishahitimu kozi walizokuja kusomea, baadhi wana nafasi za kuongeza
tena nyingine, na wengine kuomba muda wa ziada wa kukaa ughaibuni na pia
kufanya kazi.
Lakini yote hayo yanatakiwa pia utonyaji, vifungua
macho au watu wa nchi au eneo moja waliotangulia kutoa ushirikiano, kwa
sababu hata kompyuta na mtandao vikiwa vizuri na kasi ya namna gani,
mtu hawezi kurambaza tu bila dira.
Kuna watu wenye roho zao nzuri
walioingia Ulaya na kuwaita wenzao kutoka nyumbani, ili watafute
maendeleo na kuyapeleka kwao. Lakini wapo wale wanaofikiria wanaweza wao
wenyewe kumiliki kila kitu.
Kwa mfano ni upenyo unaotolewa kwa
watu wetu baada ya kusoma kozi mbalimbali. Hakuna mtu atakayekuandikia
ubaoni au kukuimbia isipokuwa ndugu au rafiki yako anayejua. Kwa hiyo,
wale waliotangulia ndiyo wanaotarajiwa kuwasaidia waliopo na
wanaoendelea kuingia kwa kuwapa ramani halisi ikoje.
Nafasi
nyingi sana za kazi baada ya watu kupata digrii zao za pili hapa
Uingereza, zimepotea bure kwa muda mrefu sasa. Baada ya watu kujibana
kusoma na kufanya kazi kidogo au ndogo ndogo wakati wa kozi zao,
walikuwa na haki ya kupata mwaka au hata zaidi ya kuchapa kazi tu kwa
saa nyingi kadiri wanavyopenda na kujikusanyia 'mapaundi' kabla ya
kurudi nyumbani.
Lakini wapo baadhi ya watu wasiopenda
ushirikiano na watu wao kutoka nyumbani. Licha ya kujua kuwa Serikali ya
Uingereza ilitoa nafasi hizo kwa yeyote anayehitimu, wao walizichukua
bila kuwaambia wenzao wanapokuja. Kama kuna madoa ya ushirikiano hapa,
hili ni mojawapo na linatakiwa kurekebishwa haraka.
Wenzetu wa
Nigeria, Ghana na Afrika Magharibi kwa ujumla na hata Wafilipino,
wamejijengea wavu mzuri wa ushirikiano na wana mtandao mkubwa.
Wanasaidiana na kuhabarishana juu ya kila kinachoendelea tofauti na
wabongo.
Niliona na kucheka kwa uchungu siku jamaa mmoja kutoka
Tanzania alipojidai si ‘wa kwetu’, alipokataa salamu ya Kiswahili baada
ya mwingine kuambiwa na jamaa fulani kwamba huyo ni Mbongo.
Akishauchuna
kinamna hiyo akifika vijiweni anaungana na wenzake wa aina hiyo kwenye
stori za jinsi alivyomwepuka ‘wakuja’, na baadaye wanakuja kumcheka
alipomaliza miezi au miaka michache na kurudi Bongo mikono mitupu.
Jambo
hili linatakiwa lifanyiwe mabadiliko makubwa na walio nchini Uingereza
au na hata walio nyumbani, kwa kuwafunda kimtandao. Ungependa tujiulize!
Lakini je, nani wa kumfunga paka kengele?
SOURCE: JAMUHURI News paper.
Tunamshukuru mdau wa TASAO aliye turushia habari hii
|